
Mapinduzi ya Gen Z huko Asia yaonesha nguvu ya vijana na mipaka yao
-
-

- Author, Tessa Wong
- Nafasi, Asia Digital Reporter
-
Ilikuwa ni harusi ya binti wa mwanasiasa mashuhuri wa Nepal iliyomchochea kwa mara ya kwanza Aditya kuingiwa na hasira. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 alikuwa akipitia mitandao ya kijamii mwezi Mei, alipokumbana na malalamiko kuhusu harusi hiyo ya kifahari ilivyozua msongamano mkubwa wa magari katika jiji la Bhaktapur.
Kilichomkera zaidi Aditya ni madai kwamba barabara kuu ilifungwa kwa saa kadhaa ili kuwapisha wageni wa hadhi ya juu (VIP), akiwemo Waziri Mkuu wa Nepal.
Ingawa madai hayo hayakuthibitishwa rasmi, na mwanasiasa husika alikana familia yake kutumia vibaya rasilimali za umma, Aditya tayari alikuwa amefikia kikomo.
“Hali hii haikubaliki kabisa,” alisema kwa msisitizo.
Katika miezi iliyofuata, alizidi kushuhudia kile alichokiona kuwa ni matumizi ya anasa yasiyo na kiasi yakiwemo picha za safari za kifahari, magari ya kifahari, majumba ya kifahari, na mikoba ya gharama kubwa yaliyowekwa na watoto wa wanasiasa katika mitandao ya kijamii.
Mmoja wao ni Saugat Thapa, mtoto wa waziri wa mkoa, ambaye alichapisha picha iliyoonesha mrundikano wa masanduku ya zawadi kutoka kwa chapa maarufu kama Louis Vuitton, Cartier na Christian Louboutin.
Masanduku hayo yalipambwa kwa taa na mapambo ya Krismasi, yakiwa yamepambwa kwa kofia ya Santa Claus.
Chanzo cha picha, Instagram / sgtthb
Hasira hii ilifikia kilele tarehe 8 Septemba, wakati Aditya na maelfu ya vijana wengine walipojitokeza mitaani jijini Kathmandu kupinga rushwa na ubadhirifu wa viongozi wa kisiasa.
Maandamano yaligeuka kuwa makubwa, na katika makabiliano kati ya polisi na waandamanaji, baadhi yao walipoteza maisha.
Siku iliyofuata, bunge lilivamiwa, ofisi za serikali zikachomwa moto, na hatimaye Waziri Mkuu KP Sharma Oli akajiuzulu.
Kwa jumla, watu wapatao 70 waliripotiwa kuuawa.
Chanzo cha picha, Sunil Pradhan/Anadolu via Getty Images
Hii ilikuwa sehemu ya shauku ya mabadiliko ambayo yameenea katika bara la Asia katika miezi ya hivi karibuni.
Maandamano haya si ya kipekee Nepal.
Katika miezi ya hivi karibuni, vijana wa kizazi cha Gen Z katika mataifa kama Indonesia na Ufilipino pia wameongoza maandamano dhidi ya rushwa na hali ya kukata tamaa kwao kuhusu mustakabali wa nchi zao.
Maelfu waliandamana Manila, huku wengine wakipaza sauti zao kwa mitandao ya kijamii, wakitumia kaulimbiu kama #IndonesiaGelap (Indonesia ya Giza) na #KaburAjaDulu (Kimbia Kwanza).
Serikali za mataifa haya zimeonya juu ya hatari ya maandamano haya kugeuka kuwa vurugu zisizodhibitika.
Lakini kwa vijana kama Aditya, haya ni matumaini ya enzi mpya ya raia wenye nguvu.
“Tumegundua kuwa hakuna jambo lisilowezekana kwa kizazi hiki cha wanafunzi na vijana,” alisema.
Malalamiko dhidi ya ‘nepo kids’
Vijana wengi nchini Nepal walianza kuwaita watoto wa wanasiasa “nepo kids” – yaani watu wanaofaidika kwa nafasi ya kifamilia na si kwa jitihada binafsi.
Kwao, hawa ni taswira ya rushwa iliyoenea na mfumo wa upendeleo usio wa haki.
Baadhi ya waliolengwa wamekanusha madai haya.
Saugat Thapa alisema “ni tafsiri potofu” kwamba familia yake ilikuwa fisadi. Wengine wamekaa kimya.
Lakini nyuma ya yote ni kutoridhika juu ya usawa wa kijamii na ukosefu wa fursa.
Chanzo cha picha, PRAKASH MATHEMA/AFP via Getty Images
Umaskini bado ni suala linaloendelea katika nchi hizi, ambazo pia zinakabiliwa na uhamaji mdogo wa kijamii.
Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa rushwa inapunguza ukuaji wa uchumi na huongeza ukosefu wa usawa.
Nchini Indonesia, rushwa imekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya nchi hiyo, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya dawa ya Kulevya na Uhalifu.
Tangu kuanza kwa mwaka huu, maandamano yamefanyika huko juu ya kupunguzwa kwa bajeti ya serikali na, pamoja na mambo mengine, wasiwasi juu ya matarajio ya kiuchumi huku mishahara ikidorora.
Mnamo Agosti, maandamano yalizuka kuhusu marupurupu ya makazi ya wabunge.
Heshtegi zilisambaa mitandaoni zikiwahimiza watu kutafuta fursa kwingineko kutokana na mbinyo wa uchumi.
Chanzo cha picha, Photo by ARUN SANKAR/AFP via Getty Images
Kwa vijana kama Zikri Afdinel Siregar wa Indonesia, ambaye ni mwanafunzi wa miaka 22, hasira yao imechochewa na hali ya maisha ya kila siku.
Wakati wabunge wa nchi hiyo walikuwa wakipokea posho ya makazi ya zaidi ya rupiah milioni 60 kwa mwezi (takriban mara 20 ya kipato cha kawaida), familia ya Zikri inayoishi Riau hupata takriban milioni 4 kwa mwezi kutokana na kilimo.
Zikri hulazimika kuendesha bodaboda ili kusaidia kulipia masomo na mahitaji yake.
“Watu bado wanahangaika kupata mahitaji ya msingi kama chakula, lakini maafisa wa serikali wanaendelea kunufaika zaidi,” alisema.
Chanzo cha picha, Ezra Acayan/Getty Images
Katika Nepal, mojawapo ya nchi maskini zaidi katika Asia, vijana wameonyesha kukatishwa tamaa sawa na kile wanachoona kuwa mfumo usio wa haki.
Miaka miwili iliyopita, katika hali iliyoshangaza taifa, kijana mmoja mjasiriamali alifariki baada ya kujichoma moto nje ya bunge.
Katika barua yake ya kujiua, alilaumu ukosefu wa fursa.
Mitandao, AI na uwezeshaji wa harakati
Siku chache kabla ya maandamano kuanza rasmi Nepal, serikali ilitangaza marufuku kwa majukwaa mengi ya mitandao ya kijamii kwa madai ya kutotekeleza agizo la usajili.
Vijana wengi walichukulia hatua hiyo kama mbinu ya kuwakandamiza.
Aditya na marafiki zake walikusanyika kwenye maktaba moja mjini Kathmandu na kutumia majukwaa ya akili mnembo (AI) kama ChatGPT, Grok, DeepSeek na Veed kutengeneza video 50 kuhusu rushwa na “nepo kids”.
Katika siku chache zilizofuata walizichapisha, nyingi TikTok ambayo haikuwa imepigwa marufuku – kwa kutumia akaunti nyingi na mitandao pepe ya faragha ili kukwepa kutambuliwa. Waliita kundi lao ‘Gen Z Rebels’.
Video ya kwanza, iliyowekwa kwenye TikTok, ilikuwa klipu ya sekunde 25 iliyokuwa na wimbo wa Abba The Winner Takes It All.
Ilionyesha picha kutoka harusi iliyomkera Aditya na kumalizia kwa ujumbe wa kuchochea:
“Nitaungana. Nitapigana dhidi ya rushwa na utawala wa mabwanyenye wa kisiasa. Je, na wewe je?”
Ndani ya saa 24, video hiyo ilikuwa imepakuliwa mara 135,000 hii ni kulingana na Aditya.
Chanzo cha picha, Navesh Chitrakar / Reuters
Majukwaa ya michezo kama Discord nayo yalitumika kupanga mikakati ya harakati, ambapo wanajadili hatua zinazofuata na kupendekeza nani wa kumteua kiongozi wa muda wa nchi.
Mitandao mingine kama Reddit ikatumika na zaidi ya watu elfu thelathini kufichua maisha ya kifahari ya viongozi.
Chanzo cha picha, Sunil Pradhan/Anadolu via Getty Images
Vijana kutumia teknolojia kwa ajili ya harakati za watu wengi sio jambo jipya – mwanzoni mwa miaka ya 2000 utumaji ujumbe mfupi wa maandishi ulichochea Mapinduzi ya pili ya Nguvu ya Watu nchini Ufilipino, wakati Arab Spring na Occupy Wall Street katika miaka ya 2010 ziliegemea sana Twita ambayo sasa inaitwa mtandao wa X.
Kinachotofautiana sasa ni ustaarabu wa hali ya juu wa teknolojia, pamoja na kuenea kwa matumizi ya simu za mkononi, mitandao ya kijamii, programu za kutuma ujumbe na sasa AI imerahisisha watu kukusanyika.
“Hivi ndivyo [Gen Zs] walikua navyo, hivi ndivyo wanavyowasiliana… Jinsi kizazi hiki kinavyojipanga ni dhihirisho la asili la hilo,” anasema Steven Feldstein, mwandamizi mwenzake katika Shirika la Carnegie kwa Amani ya Kimataifa.
Mshikamano mpya wa kikanda
Kwa kutumia mitandao, vijana wameunda mshikamano wa kuvuka mipaka.
Nembo ya fuvu maarufu miongoni mwa waandamanaji wa Indonesia sasa inaonekana katika mabango na akaunti za mitandao ya kijamii za waandamanaji wa Nepal na Ufilipino.
Hashtag #SEAblings (mchanganyiko juu ya ndugu katika Asia ya kusini mashariki au karibu na bahari) imekuwa maarufu, ikiashiria mshikamano wa kikanda wa vijana wanaopinga rushwa.
Chanzo cha picha, Getty Images
Ni kweli kwamba Asia hapo awali imeona mawimbi kama hayo ya mshikamano wa kisiasa katika eneo lote, kutoka kwa ghasia za Myanmar na Ufilipino mwishoni mwa miaka ya 1980 hadi Muungano wa Chai ya Maziwa ulioanza mnamo 2019 na maandamano ya Hong Kong, kulingana na Jeff Wasserstrom, mwanahistoria katika Chuo Kikuu cha California Irvine. Lakini anasema wakati huu ni tofauti.
“[Siku hizi] picha [za maandamano] zinaenda zaidi na kwa kasi zaidi kuliko hapo awali, kwa hivyo una picha nyingi zaidi za kile kinachotokea katika maeneo mengine.”
Teknolojia pia imezua hisia. “Unapoiona kwenye simu yako – jumba la kifahari, magari ya haraka – inafanya [ufisadi] kuonekana kuwa wa kweli,” anasema Ash Presto, mwanasosholojia wa Ufilipino katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia.
Athari hiyo inajulikana zaidi miongoni mwa Wafilipino, ambao ni miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii zaidi duniani, anaongeza.
Vifo, uharibifu – sasa nini kinafuata?
Maandamano haya yameleta madhara makubwa nje ya mitandao ya kijamii.
Majengo ya serikali kuchomwa, biashara kuporwa, na viongozi kuvamiwa majumbani mwao.
Nchini Nepal, jengo kuu la serikali, Singha Durbar, liliteketezwa kwa moto.
Zaidi ya watu 70 waliuawa nchini humo, huku watu 10 wakiripotiwa kupoteza maisha Indonesia.
Chanzo cha picha, PRABIN RANABHAT/AFP via Getty Images
Wakati marais wa mataifa haya wakilaani vurugu na kuonya dhidi ya “uhaini na ugaidi”, Rais wa Indonesia Prabowo Subianto alikemea uharibifu huo.
Polisi nao wameshutumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi.
Nchini Ufilipino, Rais Ferdinand Marcos alisema waandamanaji walikuwa sahihi kuwa na wasiwasi kuhusu ufisadi, lakini akawataka wawe na amani.
Wakati huo huo waziri wa Ufilipino Claire Castro alionya kwamba watu wenye “nia mbaya [ambao] wanataka kuivuruga serikali” walikuwa wakitumia hasira ya umma.
Waandamanaji, hata hivyo, wamewalaumu “waingiaji” kwa vurugu hizo na katika kesi ya Nepal wengi wanadai kuwa idadi kubwa ya vifo ilitokana na msako mkali wa polisi (ambao serikali imesema wataichunguza)
Chanzo cha picha, BAY ISMOYO/AFP via Getty Images
Miongoni mwa hayo yote, serikali pia zimekubali wasiwasi wa waandamanaji na wakati mwingine zilikubali matakwa fulani.
Indonesia imefuta baadhi ya motisha za kifedha kwa wabunge, kama vile posho ya nyumba yenye utata, pamoja na safari za nje ya nchi.
Na nchini Ufilipino, tume huru imeundwa kuchunguza uwezekano wa matumizi mabaya ya fedha za kuzuia mafuriko, huku Rais Marcos akiahidi kuwa hakutakuwa na “ng’ombe watakatifu” katika uwindaji huo.
Swali sasa ni je, nini kinafuata ghadhabu hiyo?
Chanzo cha picha, Navesh Chitrakar / Reuters
Maandamano machache ya kidijitali yametafsiri mabadiliko ya kimsingi ya kijamii, wachunguzi wa mambo wanasema – hasa katika maeneo ambayo matatizo kama vile rushwa yanasalia kuwa yamejikita zaidi.
Sababu kuu ni kwamba harakati hizi nyingi ni za mtandaoni, hazina viongozi rasmi, jambo linalosaidia kuepuka ukandamizaji, lakini pia linatatiza kupanga mikakati ya muda mrefu.
“Mitandao ya kijamii haijaundwa kwa mabadiliko ya muda mrefu. Inategemea hasira, ‘hashitegi’, na mitindo ya mtandaoni,” anasema Dkt. Steven Feldstein kutoka taasisi ya Carnegie Endowment.
“Unahitaji kundi lenye dira ya kisiasa, mkakati wa wazi, na uongozi wenye maono.”
Chanzo cha picha, Paula Bronstein/Getty Images
Hali hii tayari iliwahi kushuhudiwa Nepal mnamo 2006, wakati mapinduzi yaliyoongozwa na vijana yalipoondoa mfumo wa kifalme, lakini baadaye nchi ikaingia katika mzunguko wa serikali nyingi na uchumi usiokuwa thabiti.
Narayan Adhikari, mwanzilishi wa shirika la Accountability Lab, anaonya kuwa kizazi kilichopita kilipoteza maadili kwa kujifanya sehemu ya mfumo waliokuwa wakipinga.
“Hatutarudia makosa ya waliotutangulia”
Aditya ana matumaini kuwa kizazi chake kitaandika historia mpya.
“Tunajifunza kutokana na makosa ya kizazi kilichopita. Wao waliwabudu viongozi wao kama miungu.
Sisi hatufuati mtu yeyote bila mpango
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid