Chanzo cha picha, AFP
-
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita umekuwa mchungu kwa serikali kadhaa za Afrika zilizo katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Katika chaguzi ziliofanyika katika eneo hili hasa zile zilizokuwa katika mazingira ya kidemokrasia, chama tawala kilipoteza idadi kubwa ya viti au kuondolewa madarakani kabisa.
Kumeshuhudiwa mabadiliko katika nchi 6 ikiwemo Malawi ambayo Rais Lazarus Chakwera amekubali kushindwa dhidi ya mpinzani, Peter Mutharika.
Akihutubia taifa Jumatano kabla ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa rasmi, Rais Chakwera aliliambia taifa lake kuwa anafanya hivyo kwa kuheshimu nia yao ya kutaka mabadiliko ya serikali.
Matokeo ya awali kabisa yalionesha mpinzani wake, Rais wa zamani Peter Mutharika ameongoza vyema, akijizolea karibu asilimia 66 ya kura zilizohesabiwa kufikia Jumanne. Chakwera alikuwa amepata 24%.
Tanzania, Cameroon, Guinea-Bissau Jamhuri ya Afrika ya Kati ni miongoni mwa nchi zinazokwenda kwenye uchaguzi mkuu kuanzia wiki chache zijazo. Lakini katika miaka ya hivi karibuni ukiacha Malawi nchi hizi zingine tano zimeshuhudia wapinzani wakifanya vizrui dhidi ya vyama tawala.
Botswana
Moja ya mambo ya kushangaza zaidi ya chaguzi zilizofanyika mwaka jana 2024 ni kwamba nyingi zimesababisha kushindwa kwa serikali ambazo hapo awali zilionekana kuwa na nguvu kubwa ya madaraka – ikiwa ni pamoja na katika nchi ambazo hazijawahi kupata mabadiliko ya juu.
Chama cha Botswana Democratic Party (BDP) ambacho kilikuwa kimetawala nchi hiyo tangu uhuru mwaka 1966 kilisambaratishwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Pamoja na kupoteza mamlaka, chama cha BDP kilishindwa kufikia idadi ya wabunge 38 kama ilivyokuwa awali katika bunge lenye wabunge 69, na kikakaribia kufutwa kabisa.
Baada ya kushinda viti vinne pekee, BDP sasa ni moja ya vyama vidogo zaidi bungeni na kinakutana na changamoto kubwa ya kubaki na uhusiano wa kisiasa.
UDC inayoongozwa na Duma Boko iliongeza zaidi ya mara mbili ya mgao wake wa viti – kutoka 15 hadi 36.
Kutokana na hali ya mdororo wa kiuchumi (uliosababishwa kwa kiasi kikubwa na mdororo wa mapato kutokana na mauzo muhimu ya almasi), maisha marefu ya BDP na mtindo wa utawala wa Rais Mokgweetsi Masisi uliwakasirisha wapiga kura vijana.
Masuala makuu ya kampeni yalikuwa ni pamoja na uchumi, ukosefu wa ajira, kima cha chini cha mshahara na utoaji wa huduma za kijamii.
Senegal
Chanzo cha picha, AFP
Kwa upande wa Senegal, mabadiliko ya kisiasa yalikuwa ya kushangaza kama ilivyokuwa nchini Botswana, ingawa kwa njia tofauti.
Majaribio ya rais aliye madarakani kwa udanganyifu nje ya katiba yalikabiliwa na mchanganyiko wa uhamasishaji wa upinzani na uhuru wa mahakama, huku maandamano ya mitaani yakiongeza shinikizo kwa utawala wa Rais Macky Sall.
Katika maandalizi ya uchaguzi huo, utawala wa Rais Sall ulitumia mbinu mbalimbali kuzuia vuguvugu la vijana maarufu (African Patriots of Senegal for Work, Ethics and Fraternity – PASTEF) linaloongozwa na kiongozi wa upinzani, Ousmane Sonko.
Kufungwa kwa wanaharakati wa vijana, kwa mfano Sonko mwenyewe na Bassirou Faye, na jaribio la kuchelewesha uchaguzi kuliashiria hatua ya mabadiliko katika harakati za Senegal kuelekea demokrasia zaidi.
Wiki chache kabla ya uchaguzi, viongozi wa upinzani Bassirou Diomaye Faye na Ousmane Sonko walikuwa wakiteswa gerezani, huku serikali ya rais Macky Sall ikitumia vibaya mamlaka yake ili kuepuka kushindwa.
Shinikizo la ndani na kimataifa lililosababisha Faye na Sonko kuachiliwa huru tarehe 14 mwezi Machi, lilimsaidia Faye kushinda urais katika duru ya kwanza, huku mgombea wa serikali akishinda asilimia 36% pekee ya kura.
Somaliland
Chanzo cha picha, AFP
Jamhuri iliyojitenga kupata kutambuliwa kimataifa kama serikali huru, Somaliland, ilifanya uchaguzi wa amani ambao ulisisitiza madai yake kuwa chombo thabiti cha kidemokrasia.
Chama tawala, Kulmiye – kilichokuwa madarakani tangu 2010 na kinachoongozwa na Rais Muse Bihi Abdi tangu 2017 – kiliwania dhidi ya chama kikuu cha upinzani cha Waddani, ambacho kiongozi wake Abdirahman Mohamed Abdullahi alipata asilimia 64 ya kura na kuwa Rais wa sita wa Somaliland. Bihi Abdi alipata asilimia 35 ya kura.
Matatizo ya kiuchumi, siasa za kijiografia na siasa za kimila zilifanya iwe vigumu kwa chama kilicho madarakani kuwashawishi wapiga kura kukipigia upatu kuendelea kukaa madarakani.
Ushindi wa Waddani unaonyesha uthabiti wa kidemokrasia wa Somaliland. Na viongozi wote walihaidi kufanya juhudi eneo hilo la Somalia litambulike kimataifa.
Ghana
Chanzo cha picha, AFP
‘Mwaka wa uchaguzi’ambao ulikuwa ni mwaka 2024 ulihitimishwa na Ghana, mwezi Desemba.
Demokrasia ya nchi hiyo imesifiwa kama mfano katika eneo ambalo demokrasia imeshuka.
NPP iliyo madarakani ilijitahidi kuzoea usawa wa fedha na madeni ya miaka ya hivi karibuni.
Mchanganyiko wa migogoro ya kisiasa na kimazingira ilitumika kama msingi wa kampeni za uchaguzi.
Rais wa zamani, John Dramani Mahama, aliongoza chama kikuu cha upinzani cha NDC.
Wakati huo huo Makamu wa Rais Mahamudu Bawumia aliongoza chama tawala.
Vyama viwili vikubwa vilipigana uchaguzi kwa misingi ya rekodi zao serikalini.
Kwa uchumi ulioporomoka, ukosefu wa ajira kwa vijana na mfumuko wa bei, chama cha upinzani cha NDC kilitumia changamoto hizo kupata wingi wa wabunge (viti 183 dhidi ya 88 vya NPP).
Vyama tawala vilivyosuasua japokuwa vilishinda
Hata katika hali ambapo serikali tawala hazijashindwa katika uchaguzi,sifa na udhibiti wao wa kisiasa umesuasua sana.
Kama ilivyokuwa kwa chama cha SWAPO hivi punde, chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini kiliendelea kuwa madarakani, lakini kutokana na kampeni mbaya, kilishuka chini ya asilimia 50 ya kura katika uchaguzi wa kitaifa kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa utawala wa wazungu wachache mwaka 1994.
Hali hii ilimlazimu Rais Cyril Ramaphosa kuunda serikali ya mseto na kugawa nyadhifa 12 za baraza la mawaziri kwa vyama vingine, ikiwa ni pamoja na nyadhifa muhimu kama ile ya Mambo ya Ndani.
Kwa matokeo hayo, eneo ambalo limekuwa maarufu kwa serikali zinazoshikilia madaraka kwa miongo kadhaa sasa linaona mwaka mmoja wa siasa za vyama vingi na ushindani mkali.
Hata hivyo, hali hii iliepukwa na nchi ambazo uchaguzi haukuwa huru wala wa haki, kama vile Chad na Rwanda, au zile ambapo serikali zilishutumiwa na upinzani na makundi ya haki za binadamu kwa kutumia mbinu za udanganyifu na ukandamizaji ili kuepuka kushindwa, kama ilivyokuwa nchini Msumbiji.
Kwanini wapigaji kura wanavipa kisogo vyama tawala barani Afrika?
Kurudi kwa demokrasia huria barani Afrika, pamoja na utekelezaji wake, kumezua mjadala miongoni mwa wachambuzi wa siasa.
Kwa mujibu wa takwimu za Afrobarometer, wananchi wengi wa Afrika wanaunga mkono mfumo wa vyama vingi.
Hata hivyo, wapo wanaohoji mafanikio ya demokrasia hiyo, hasa kutokana na ukosefu wa manufaa ya moja kwa moja kwa raia wa kawaida.
Changamoto za kila siku kama vile ukosefu wa ajira kwa vijana, kutoimarika kwa viwanda, na huduma duni za kijamii zimechangia kwa kiasi kikubwa hali ya kutoridhika.
Kwa upande mwingine, siasa zimeendelea kuwanufaisha viongozi wa kisiasa kwa kuimarisha hadhi na mali binafsi, huku sehemu kubwa ya jamii ikiendelea kuishi katika hali duni.
Hii imeifanya demokrasia huria ionekane kupoteza uhalali wake miongoni mwa watu wengi.
Nchini Botswana, Mauritius na Senegal, ongezeko la wasiwasi wa raia kuhusu rushwa na matumizi mabaya ya madaraka lilisababisha kupungua kwa imani kwa serikali.
Mtazamo kwamba serikali zilikuwa zikishughulikia vibaya uchumi ulikuwa na uzito mkubwa kwa sababu watu wengi walikabiliwa na mwaka mgumu kifedha.
Mbali na kushindwa kwa serikali katika maeneo mengine, hasira ya kiuchumi ilikuwa ni chanzo kikuu kilichosababisha maandamano ya vijana nchini Kenya yaliyotikisa serikali ya Rais William Ruto mnamo Julai na Agosti.
Mabadiliko ya mkakati: Upinzani wajifunza na kuimarika
Pamoja na changamoto zilizopo, kadri demokrasia inavyozidi kuota mizizi Afrika, vyama vya upinzani vinaendelea kujifunza na kubadilika kwa kila mzunguko wa uchaguzi.
Hali hii imewalazimu kuimarisha mikakati yao, hasa katika kukabiliana na vyama tawala vyenye mwelekeo wa udikteta.
Katika baadhi ya nchi kama Botswana, Mauritius, Ghana, na Senegal, vyama vya upinzani na harakati za kiraia zimeweza kuunganisha nguvu za kidemokrasia na kuhimiza ushiriki wa wananchi kwa mafanikio.
Ushindi wa demokrasia katika nchi hizi unaashiria uwezekano wa kuimarika kwa vyama vya upinzani barani kote.
Kadri uelewa wa raia unavyozidi kuongezeka, wapiga kura wanakuwa wakosoaji zaidi na wanauliza maswali kuhusu uhalisia wa utekelezaji wa ahadi za kampeni.
Wanataka kujua lini, kwa vipi, na kwa rasilimali zipi chama fulani kitatekeleza manifesto yake.
Kwa kiasi fulani, mlolongo wa mapinduzi ya kijeshi uliojitokeza katika maeneo ya Afrika Magharibi na Kati unaweza kufasiriwa kama matokeo ya kushindwa kwa vyama vya upinzani kuandaa na kuhamasisha raia waliokata tamaa ili kufanya mabadiliko kupitia sanduku la kura.