Watanzania wametakiwa kukichagua Chama cha Mapinduzi (CCM) kutokana na uimara wa viongozi wake kuisimamia Serikali kufanya mambo makubwa ikiwamo maboresho ya miundombinu ya maji, umeme, barabara na afya.
Hayo yamesemwa jana Oktoba 26,2025 katika Kata ya Makurunge, Wilaya ya Kisarawe na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani, Dk Chakou Tindwa, wakati wa kuhitimisha kampeni za ubunge za mgombea wa Jimbo la Kisarawe Dk Seleman Jafo.
Dk Tindwa amesema kuwa ametembelea nchi mbalimbali jirani na kubaini kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya barabara, umeme, maji, afya, elimu na huduma nyingine za kijamii. Akieleza kuwa hilo linatokana na CCM.
Amesema wananchi wa Kisarawe wanapaswa kuendelea kuiamini CCM kwa kumchagua mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, mgombea ubunge wa Kisarawe, Dk Seleman Jafo na diwani wa kata hiyo, Wakili Aidan Kitale, ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya CCM Kanda ya Mashariki, Sophia Simba, amesema Tanzania inaweka historia kwa mara ya kwanza kwa mgombea mwanamke kuwania urais, jambo linalodhihirisha usawa wa kijinsia ndani ya chama hicho.
Kwa upande wa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Dk Seleman Jafo, ameahidi endapo atachaguliwa, ataendelea kusimamia miradi ya maendeleo ikiwemo kuhakikisha vitongoji 79 vinapata huduma ya umeme, maji ya uhakika, pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, elimu na afya.