Wito wa kuususia Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) pamoja na makampuni yenye mfungamano na nchi hiyo ya kifalme unazidi kuongezeka kwenye mitandao ya kijamii, ukichochewa na hasira zinazotokana na uungaji mkono wa serikali ya Abu Dhabi kwa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.

Kampeni hiyo, ambayo ilikuwa ikisambaa katika duru za ndani ya Sudan na za raia wa nchi hiyo wanaoishi nje ya nchi ilipata kasi mpya baada ya RSF kuuteka mji wa el-Fasher ulioko Darfur Kaskazini mnamo Oktoba 26.

Kutekwa kwa ngome ya mwisho ya Vikosi vya Jeshi la Sudan (SAF) katika eneo hilo kuliambatana na mauaji mengi, huku picha za kutisha zikionyesha wapiganaji wa RSF wakijivunia kuwaua raia, wakiwemo wanawake, watoto na wazee, sambamba na kuonekana raia wakiukimbia mji huo.

Picha za setilaiti zimeonyesha mitaa yenye madoa ya damu na uharibifu mkubwa, matukio ambayo yamechochea hasira mitandaoni.

Imekuwa ikiripotiwa sana kwamba Abu Dhabi ndiye mfadhili mkuu wa RSF, kwa kuwapatia wapiganaji wa vikosi hivyo silaha na vifaa.

Katika mjibizo waliotoa kuhusiana na suala hilo, baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakiiomba Marekani, ambayo ni mmoja wa wauzaji wakuu wa silaha wa Imarati, iiwekea vikwazo vya silaha nchi hiyo na kuiwekea vikwazo pia RSF na uongozi wake.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakitoa wito pia kwa watu kughairisha safari za kwenda Dubai, kususia bidhaa za Imarati, na kufikiria upya kufanya biashara na makampuni yenye makao yao huko UAE.

“Acha kwenda Dubai na Abu Dhabi, susia UAE kwa uhalifu wao nchini Sudan,” ameandika mtumiaji mmoja wa mitandao ya kijamii.

Japokuwa Muungano wa Falme za Kiarabu unakanusha kwamba unaviunga mkono Vikosi vya Usaidizi wa Haraka katika vita vya ndani nchini Sudan, lakini ushahidi mwingi umetolewa kuthibitisha tuhuma hizo dhidi ya Abu Dhabi.

Mnamo Januari 2024 duru za habari ziliripoti kuwa, Imarati ilikuwa ikiipatia RSF silaha kupitia mtandao tata wa usambazaji ulioenea kwenye nchi kadhaa za Afrika kuanzia Libya, Chad, Uganda na hadi kwenye maeneo yaliyojitenga ya Somalia…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *