Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesisitiza kwamba ustawi wa sekta yake ya nyuklia ya amani nchini Iran unalenga kuimarisha ustawi wa taifa, si kupata silaha.
Ametoa matamshi hayo leo Jumapili katika mkutano wake na mameneja wakuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) baada ya kutembelea maonyesho ya mafanikio ya karibuni ya nyuklia katika nyanja za huduma za afya, dawa, na uzalishaji wa dawa za mionzi.
Pezeshkian amesema propaganda na simulizi zenye upendeleo vinalenga kuonyesha kwamba shughuli za nyuklia za Iran zinafanana na zile za kutengeneza mabomu ya atomiki. “Hata hivyo, tasnia ya nyuklia ni mkusanyiko mkubwa wa uwezo wa kisayansi na viwanda, na ni sehemu ndogo tu ya matokeo yake yasiyo ya kawaida na yasiyo ya kibinadamu yanahusiana na utengenezaji wa mabomu,” amesisitiza Rais Pezeshkian.
Amesema: “Nia na dhamira yetu katika kupanua tasnia hii ni kukidhi mahitaji ya watu na kuboresha ustawi wa nchi yetu, si kutengeneza silaha.”
Rais wa Iran pia ameeleza kuwa kutumia teknolojia za kisasa na kuingia katika uwanja wa ushindani wa kimataifa ni muhimu kwa nchi yetu wakati ambapo mataifa ya kibeberu yanataka kuyanyima mataifa huru fursa ya kupata teknolojia ya kisasa.
Rais Masoud Pezeshkian amesisitiza zaidi kwamba uhasama dhidi ya Iran na mauaji ya wanasayansi wake yanatokana na wasiwasi wa madola makubwa kuhusu kujitegemea kisayansi na kiteknolojia kwa nchi hii.

“Tumetangaza mara kwa mara kwamba kutengeneza silaha za nyuklia si ajenda yetu—na wao (madola makubwa duniani) wanajua hili. Hata hivyo wanatumia madai ya uongo kama kisingizio cha kuzuia maendeleo ya Iran,” amesema Rais Pezeshkian.
Mwezi Juni mwaka huu Marekani iliingia katika vita vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kulipua maeneo matatu ya nyuklia ya Iran katika ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Katika kujibu uchokozi huo, Vikosi vya Jeshi la Iran vililenga maeneo ya kimkakati katika maeneo yaliyokaliwa mabavu huko Palestina na kambi ya anga ya jeshi la Marekani ya Al-Udeid nchini Qatar, ambayo ndiyo kambi kubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani eneo la Asia Magharibi.