h

Chanzo cha picha, Getty Images

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) nchini Tanzania imetangaza kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, utakaohusisha nafasi ya Rais, wabunge na madiwani, utafanyika siku ya Jumatano, tarehe 29 Oktoba 2025.

Akizungumza katika uzinduzi wa ratiba ya uchaguzi huo jijini Dodoma leo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa rufaa Jacob Mwambegele, amesema maandalizi ya uchaguzi huo yameanza rasmi na kuainisha tarehe muhimu katika kalenda ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, utoaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais utafanyika kati ya Agosti 9 hadi 27, 2025. Aidha, ameongeza; “Tarehe 27 Agosti 2025 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa kiti cha rais na makamu rais, uteuzi wa wagombea ubunge na uteuzi wa wagombea udiwani”, alisema Jaji huyo.

Kwa upande wa kampeni, Tanzania Bara itakuwa na kipindi cha kampeni kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28, huku Tanzania Zanzibar kampeni zikiendeshwa kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 27, ili kupisha upigaji wa kura ya mapema.

“Tarehe 29 Oktoba, 2025 siku ya Jumatano itakuwa ndio siku ya kupiga kura”, alisema Mwambegele, kuhusu uchaguzi huo unaolenga kuwapa wananchi fursa ya kidemokrasia kuchagua viongozi wao wa ngazi mbalimbali.

Uchaguzi huu utakuwa wa mfumo wa kupiga kura moja kwa kila nafasi, yaani kwa Rais, mbunge na diwani, kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Vyama vinavyoshiriki na msimamo wa CHADEMA

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Uchaguzi wa mwaka huu unatarajiwa kushirikisha vyama 18 kati ya 19 vya siasa vyenye usajili kamili. Chama Kikuu cha Upinzani, CHADEMA, kimesema hakitashiriki katika uchaguzi huo kwa madai ya kutokuwepo kwa mazingira ya uchaguzi huru na wa haki.

CHADEMA imesisitiza kuwa haitashiriki hadi marekebisho ya msingi ya mfumo wa uchaguzi yafanyike. Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kwa sasa anashikiliwa gerezani akikabiliwa na mashtaka kadhaa likiwemo la uhaini.

Vyama vilivyothibitisha ushiriki wao kwa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi tarehe 12 Aprili 2025, ni pamoja na chama tawala CCM, CUF, ACT-Wazalendo, ADC, TLP, UDP, CHAUMMA, CCK, DP, MAKINI, SAU, AAFP, UMD, NCCR, NLD, UPDP, NRA na ADA-TADEA.

Katika uchaguzi mkuu uliopita wa wa mwaka 2020, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli wa CCM, alitangazwa mshindi kwa zaidi ya asilimia 84 ya kura.

Uchaguzi huo ulikumbwa na shutuma kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani na mashirika ya haki za binadamu, yaliyodai kuwepo kwa ukiukwaji wa haki za wapiga kura na ukandamizaji wa demokrasia. Hata hivyo tume ya Uchaguzi wakati huo (NEC), ilisisitiza uchaguzi ulikuwa huru na ulifuata utaratibu na sheria.

Tangu wakati huo, kumekuwa na wito kutoka kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi kutaka kufanyike mageuzi ya kisiasa, hasa kwenye mfumo wa uchaguzi, jambo ambalo linazidi kuwa ajenda kuu kuelekea uchaguzi wa mwaka huu wa 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *