
Chanzo cha picha, Facebook
-
- Author, Leilah Mohammed
- Nafasi, BBC Swahili
Iwapo wewe ni mgeni katika ukanda wa Afrika ya Mashariki basi ninapotaja majina haya mawili , ni vigumu kuelewa kwa nini yametajwa katika sentensi moja.
John Heche na Edwin Sifuna, wametengwa na mipaka ila kimsingi viongozi hawa wawili huenda wakatajwa kama pacha wa siasa za uwajibikaji katika mataifa yao binafsi na vile vile Afrika Mashariki.
Unaweza kujiuliza ni kwa nini mwandishi huyu aliamua kuwaweka wawili hawa kwenye kapu moja, vuta kiti nikupe maelezo kisha utafanya uamuzi ikiwa wana tofauti nyingi zaidi ya wanavyofanana.
Ujana na uongozi wa siasa pinzani
Edwin Sifuna ambaye ni Seneta wa jimbo la Nairobi nchini Kenya, ni moja wapo ya Makatibu wakuu wenye umri mdogo katika chama kikubwa cha upinzani nchini Kenya – ODM. John Heche naye ni mbunge wa zamani wa eneo bunge la Tarime nchini Tanzania – na kwa sasa yeye ndiye Naibu mwenyekiti wa chama kikubwa cha upinzani Tanzania – CHADEMA.
Wawili hao wanapishana na mwaka mmoja tu kwenye umri huku Heche akiwa na miaka 44 naye Sifuna akiwa na umri wa miaka 43.
Viongozi hawa wawili wamevalia njuga majukumu yao katika vyama vyao husika kwa ujasiri, kila mmoja akitetea sera za chama chake na kuonekana kutozungumza kwa pande zote za midomo yao kama inavyoshuhudiwa na wanasiasa wengine.
Ujasiri katika siasa za uadilifu na uwajibikaji

Chanzo cha picha, Sifuna facebook
Katika hafla ya mazishi ya aliyekuwa mlinzi wa Raila Odinga – George Oduor yaliyofanyika katika kaunti ya Siaya nchini Kenya, Seneta Sifuna alichukuwa fursa aliyopewa kuwahutubia waliofika – kumkosoa Rais William Ruto na kumpa alichokitaja kama ushauri wa jinsi ya kulirekebisha gari la taifa kwenye barabara salama.
‘ Bishop ametuambia hapa kwamba kazi yako ni ngumu sana, lakini saa zingine mheshimiwa Rais, wanasema waswahili kwamba mwiba wa kujidunga hauambiwi pole. Kuna watu katika serikali yako Rais ambao kazi yao ni kujipiga handball. Sasa kama wale ambao wanazuia Watoto kutoshiriki katika mchezo wa kuigiza huko Nakuru, naomba kama wanasumbua ‘read them the riot act’ waingie laini, kwa sababu tunajuwa kazi yako ni ngumu,’ alisema Sifuna ambaye alishangiliwa na waliokuwepo.
Na kwa kuwa Rais Ruto pia sio muoga wa kukashifiwa hadharani, alimjibu Sifuna kwa kumueleza kwamba yeye ni mwanchama mwanzilishi wa ODM na kwamba hakuna kipya atakachokisema Sifuna ambacho hakijui yeye.
Kwa upande wake John heche hajakosa kutumia kila fursa anayopata kuikosoa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika siasa za Tanzania.
‘Sisi kama Chadema tulimsikiliza Rais alipokuwa akilihutubia Bunge. Alikuwa anazungumzia jambo zito kwa lugha rahisi sana .Jambo la watu kutekwa ni jambo kubwa sana. Alizungumza kama ni jambo dogo sana, watu kupotea. Hakuna namna mtu mzima anaweza kupotea kwake bila ya kutojulikana , mbuzi na kondoo wanapotea nyumbani wala sio binadamu.
Rais alitaka suala la kaka yetu Ali Kibao aliyepotea kushughulikiwa haraka sana na ripoti kutolewa, ila hadi sasa hatujasikia lolote kumhusu wala kutoka kwa vyombo vya dola,’ alisema Heche katika kikao cha wanahabari.
Matamshi yaliyowaweka pabaya na uongozi

Chanzo cha picha, Instagram
Edwin Sifuna anaonekana kuwa mlengwa wa vigogo wa chama cha ODM ambao kwa sasa hawafurahii matamshi yake yanayoonekana kukosoa uamuzi wa kinara wa chama chake kuingia katika mkataba wa makubaliano na chama tawala cha Rais William Ruto – UDA.
Sifuna amenukuliwa na vyombo vya habari nchini Kenya akisema kwamba yupo tayari kuondolewa katika wadhifa wa Katibu Mkuu kwa sababu ya msimamo wake wa kutomuunga mkono Rais William Ruto.
Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho na Gavana wa HomaBay Gladys Wanga amemsuta mara kadhaa Sifuna kwa kuonekana kutoa matamshi ambayo anasema , ‘ni ya kibinafsi na wala sio msimamo wa chama.’
Sifuna naye amesisitiza kwamba, ‘Siwezi kuunga mkono kiongozi ambaye maadili yake yanatiliwa shaka. Nitashikilia msimamo wangu dhidi ya serikali hii na ningeenda kuwakumbusha wale wanaonikosoa ndani ya chama kwamba nina haki ya kuzungumza ninachokihisi, Nataka ileleweke sitaunga mkono mpango wa chama kuunga mkono azimio la Rais William Ruto kuwania Urais kwa awamu ya pili mwaka wa 2027,’ Alisema Sifuna.
Katika upande wa pili John Heche hakusita kumkosoa aliyekuwa mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe kuhusiana na tofauti za misimamo yao chamani.
Akizungumza baada ya kuchukua na kurejesha fomu ya kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho , Heche alisema anamuheshimu sana Freeman Mbowe kama baba yake wa kisiasa na mlezi wake, akisisitiza kuwa hata katika mazingira ya ushindani hatoweza kumkosea heshima kwa namna yoyote ile.
“Mimi ninamuheshimu sana Freeman Mbowe na ninampenda. Kwangu yeye ni baba wa kisiasa ambaye amenijenga hadi hapa nilipo. Siwezi kusema lolote baya juu yake. Lakini leo nasema rasmi, Mwenyekiti Freeman Mbowe, kwa heshima, tutakwenda kwenye uchaguzi, na tutakushinda kwa njia ya kidemokrasia,” alisema Heche.
Ni viongozi wenye kuleta sura ya vijana katika siasa za upinzani

Chanzo cha picha, Sifuna facebook
Mwaka 2013 Edwin Sifuna alijitosa kwenye ulingo wa siasa za Kenya kwa kujiunga na chama cha CORD kama mshauri wa masuala ya kimkakati. Miaka mitatu baadaye alivuka na kujiunga na muungano wa NASA ambao Raila aliutumia kuwania Urais dhidi ya Rais Kenyatta mwaka wa 2017.
Naye Sifuna alijaribu kuwania kiti cha ubunge cha Kanduyi ila alishindwa kupata tiketi ya chama cha ODM. Jaribio lake kuwania Useneta wa Nairobi lilifanikiwa aliposhinda kiti hicho kwenye uchaguzi wa Agosti 2022 na kuwa kijana wa pili kuuwakilisha mji mkuu wa Nairobi katika bunge la Seneti baada ya Johnson Sakaja.
‘Kenya ni nyumbani na wala sina mipango ya kuhama. Ikiwa wakazi wa Nairobi watanipa nafasi nyingine 2027, ningependa kuendelea kuwafanyia kazi kama mjumbe wao katika bunge la Seneti ambapo tunaangazia jinsi wanavyopata huduma kutoka kwa usimamizi wa kaunti zetu 47,’ alisema Sifuna katika mahojiano kwenye runninga moja nchini Kenya.
Kwa upande wake, John Heche alianzia siasa zake za upinzani mnamo 2010 alipochaguliwa kuliwakilisha baraza la wilaya ya Tarime kama diwani kabla ya kuliwakilisha eneo bunge la Tarime katika bunge la kitaifa mjini Dodoma.
Kwa sasa sio mbunge ila amekuwa akiendeleza masuala ya uongozi wa chama , mara kwa mara akijipata pabaya na serikali ya Tanzania kwa kuandaa mikutano ya hadhara pasipo na kufuata kanuni zilizowekwa kuhusiana na mikutano ya hadhara nchini humo.
Kampeni ya ‘No Reform No Election’ na Maandamano ya Gen Z
Katika mwezi mmoja uliopita kumekuwa na hashtag mbili zilizosambaa katika mitandao ya kijamii nchini Tanzania. Ya kwanza ni #NoReformsNoElections na #OktobaTunatiki.
Heche amekuwa msitari wa mbele kuendeleza injili hiyo ya kuwataka raia wa Tanzania kukataa kushiriki kwenye uchaguzi ambao anahisi sio mchezo unaowapa wachezaji wote nafasi sawa ya ushindani.
‘Hatutakubali kuhusishwa na hali ambayo inaonekana kutoweka usawa kwa wote’ alisema Heche.
Kwa upande wake Sifuna amekuwa mstari wa mbele kukashifu mauaji na kutekwa kwa vijana nchini Kenya katika muda wa mwaka mmoja hasa kutokana na maandamano ya kupinga sera zinazotolewa na serikali ya Rais William Ruto.
‘Vijana hawana kazi, wanaumia, wakizungumza wanapigwa au kuuawa, siwezi kukubaliana na hilo kamwe,’alisema Sifuna.
Sifuna na Heche wana sikio la vinara wao

Chanzo cha picha, Facebook
Kinara wa CHADEMA Tundu Lissu ambaye kwa sasa anakabiliwa na shtaka la uhaini nchini Tanzania hajasita kumuunga mkono naibu wake John Heche kila anapopata nafasi.
Na wanapokutana mahakamani Heche akihudhuria kesi dhidi ya kinara wake, wawili hao huzungumza kwa kina na kukumbatiana sana.
Katika hali ile ile, Raila Odinga ambaye ni kinara wa ODM amewasuta wakosoaji wa Sifuna kwa kusema, ‘Wachaneni na Sifuna. Ana Uhuru wa kujieleza kuhusiana na masuala ya kitaifa na ya chama. Anapozungumza, juweni ni msimamo wa chama cha ODM,’ alisema Odinga katika hafla ya mazishi mjini Kakamega, magharibi mwa Kenya mwezi jana.
Haya yalijiri wakati ambapo katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi Kenya -COTU – Francis Atwoli alizomewa kwa kumkashifu Sifuna kuhusiana na matamshi yake ya kumsuta Rais William Ruto na kumtaja kama kiongzi ambaye hawezi kuaminiwa.

Chanzo cha picha, Raila Facebook
Je, wana tofauti yoyote?

Chanzo cha picha, John Heche Facebook
Kwa wanaowajuwa kwa undani wanaweza kutaja ni jinsi gani ambapo wawili hawa wanatofautiana.
Lakini kwetu sisi ambao tunawajuwa kutokana na maisha yao ya hadharani hasaa ya siasa, wanaonekana kunadi sera za uwajibikaji na uadilifu, wote wakiwa wenye kusema wanayoyasema bila uoga wa kitakachowapata au ujumbe wao utakavyopokelewa.
Vijana hawa wawili ndio wanaanza safari yao ya uongozi katika vyama vyao na wanaonekana kuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa vijana ambao ni wafuasi wa vyama vyao.
Wote wanatangaza injili ya mabadiliko katika uongozi: Heche akisema kwamba dawa kubwa inaohitajika kutibu maradhi ya Tanzania ni mabadiliko ya kikatiba.
Naye Sifuna akisema kwamba dawa inayoweza kutibu maradhi ya Kenya ni Raila Odinga kumfanya Willliam Ruto kuwa Rais wa kwanza katika historia ya Kenya kuhudumu kwa awamu moja pekee na kuondolewa kupitia njia halali ya kura.
Hawa ndio sura ya siasa za siku za usoni Afrika Mashariki?
Wawili hawa ni wazuri katika kujadili hoja mbali mbali bungeni. Alipokuwa mbunge, Heche alichambua vikali mradi wa reli ya kisasa Tanzania SGR ambayo alihisi haikutekelezwa kwa kuwazingatia raia.
Sifuna naye ameshambuliana na Maseneta wenza katika bunge la Seneti akikosoa miradi kadhaa ya serikali ikiwemo bima ya kitaifa ya SHA ambayo amesema mara kadhaa inaonekana kuwaumiza Wakenya kuliko kuwafaa.
Jibu hilo linaweza kupatikana kupitia kura, na kwa sasa, halitojulikana Tanzania kwa kuwa CHADEMA hawatoshirki uchaguzini kwa kususia kutekeleza masuala muhimu kwenye sheria za uchaguzi, na kwa Kenya miaka ni miwili iliyosalia mbivu na mbichi kujulikana.
Imehaririwa na Seif Abdalla