S

Chanzo cha picha, URT/SALUM

Tume huru ya Taifa ya uchaguzi nchini Tanzania (INEC) imeteua rasmi majina ya wagombea 17 wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025. Hatua hii imekuja baada ya wagombea hao kutoka vyama 17 kurejesha fomu na kukidhi masharti ya kikatiba na kisheria.

CHADEMA, chama kikuu cha upinzani, hakitashiriki uchaguzi huu kikisisitiza kuwa marekebisho ya mfumo wa uchaguzi ni sharti yafanyike kwanza ili kuwe na uchaguzi huru na wa haki.

ACT-Wazalendo pia haitakuwa na mgombea baada ya Luhaga Mpina kuenguliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufuatia pingamizi lililotolewa na mwanachama wa chama hicho, Monalisa Ndala.

Sababu kuu iliyoelezwa ni kwamba Mpina alipata uanachama Agosti 5, 2025, nje ya muda wa kisheria wa kuchukua fomu za kugombea ndani ya chama, ambapo ilipaswa kuwa kabla ya Mei 25, 2025.

Aidha, mgombea wa chama cha ADC Wilson Elias pia amethibitishwa na Tume.

Wagombea waliothibitishwa na Tume ni kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo Rais aliyepo madarakani, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amethibitishwa kugombea urais akiwa na Balozi Dkt. Emanuel Nchimbi kama mgombea mwenza.

a

Chanzo cha picha, Ikulu

Chama Cha Wananchi (CUF) kimemsimamisha Gombo Samandito Gombo akiwa na mgombea mwenza Husna Mohamed Abdalla. NCCR-Mageuzi kitawakilishwa na Haji Ambar Khamis pamoja na Dkt. Eveline Wilbard Munisi, huku chama cha CHAUMMA kikiwasimamisha Salum Mwalimu na Devotha Mathew Minja.

Katika chama cha UDP, mgombea ni Saum Hussein Rashid, mgombea mwenza ni Juma Khamisi Faki. Chama cha TLP amethibitishwa Yustas Mbatina Rwamugira na Amana Suleiman Mzee. Chama cha DP amepitishwa Abdul Juma Mluya akiwa na Sadoun Abrahman Khatib, wakati chama cha TADEA kimemsimamisha Georges Gabriel Bussungu kuwania urais na Ali Makame Issa kama mgombea mwenza.

Kwa upande mwingine, chama cha UMD, Tume imemthibitisha Mwajuma Noty Mirambo akiwa na mgombea mwenza Mashavu Alawi Haji. UPDP amepitishwa Twalib Ibrahim Kadege na Abdalla Mohamed Khamis. NRA ameteuliwa Hassan Kisabya Almas kuwania urais na Hamis Ali Hassan mgombea mwenza, huku chama cha MAKINI kikiwa na mgombea urais Coaster Jimmy Kibonde na mgombea mwenza Azza Haji Suleiman.

Chama cha NLD kitawania urais kupitia Doyo Hassan Doyo pamoja na Chausiku Khatib Mohamed kama mgombea mwenza, wakati SAU kimemsimamisha Majalio Paul Kyara kupeperusha bendera ya chama hicho na Satia Mussa Bebwa. CCK kimempitisha David Daud Mwaijojele na mgombea mwenza Masoud Ali Abdala, huku chama cha AAFP kikiwa na Kunje Ngombare Mwiru kama mgombea urais pamoja na Chumu Abdallah Juma, mgombea mwenza.

s

Chanzo cha picha, Almasi

Kwa mwaka huu, idadi ya wagombea wa urais imeongezeka hadi 17, ikilinganishwa na wagombea 15 walioteuliwa na Tume ya uchaguzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Hata hivyo, hakutarajiwi kuwa na ushindani mkubwa, hasa kutokana na kutoshiriki vyama viwili vikubwa vya upinzani, CHADEMA na ACT Wazalendo. CHADEMA haishiriki kabisa uchaguzi wa mwaka huu, wakati ACT chenyewe baada ya mgombea wake urais, Mpina kuenguliwa, na ambacho kinasema kitakwenda Mahakamani kitashiriki kwenye ngazi ya ubunge na udiwani, na urais kwa upande wa Zanzibar.

Katika uchaguzi wa mwaka 2020, Tume ya uchaguzi ilipitisha wagombea 15 wa urais ambapo Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wa CCM aliibuka mshindi kwa kura milioni 12.5, akifuatwa na Tundu Lissu wa CHADEMA aliyepata kura milioni 1.9. Ukiacha Chadema iliyoshiriki, vyama vingine vyote vya upinzani hakuna kilichofikisha kura laki moja.

Shughuli za uteuzi wa wagombea urais 16 na wagombea wenza, zilifanyika katika ofisi za NEC zilizopo Njedengwa, jijini Dodoma, chini ya Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele. Hii ni hatua ya mwanzo rasmi ya safari ya kuelekea kupata kiongozi wa nafasi ya juu kabisa katika nchi.

.
Maelezo zaidi:
,

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *