
Chanzo cha picha, Global Publishers
-
- Author, Na Sammy Awami
- Nafasi,
Agosti 29, 2025 Mahakama kuu kanda ya Manyara imefuta amri ya Msajili wa Vyama Vya Siasa ya kuzuia ruzuku ya Chadema na kutowatambua Katibu Mkuu, Manaibu wake na wajumbe watano wa kamati kuu waliothibitishwa na Baraza kuu Januari 22, 2025 baada ya uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama, chini ya uongozi mpya wa Mwenyekiti wake Taifa, Tundu Lissu.
Uamuzi huu unafuatia hatua ya Msajili aliyochukua mwezi Mei mwaka huu kutangaza kutengua na kutoutambua Sekretarieti ya uongozi wa chama hicho na kusitisha kutoa ruzuku kwa chama cha Chadema kwa madai ya kwamba kikako kilichowaidhinisha hakikuwa na akidi halali na inayotakiwa ambayo ni zaidi ya asilimia 50% ya wajumbe. Chadema walipingia hili Mahakamani maamuzi haya Msajili kama ambavyo ACT Wazalendo nao wako Mahakamani sasa kupinga uamuzi mwingine wenye nguvu uliofanywa na Msajili.
Kwa upande ACT Wazalendo pigo walilolipata kwa mgombea wao wa urais, Luhaga Mpina kuwekewa kizingiti na Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume Huru ya Uchaguzi kutomteua itakuwa imewakumbusha kesi waliyoshiriki kuifungua miaka kadhaa iliyopita wakipinga Sheria ya Vyama vya Siasa. Yanayotokea sasa, yanaleta mjadala kuhusu nguvu kubwa na mamlaka ya Msajili wa vyama vya siasa.
Wasiwasi wa Chadema, ACT Wazalendo na Wanaharakati
Maamuzi makubwa kama haya ya kutengua uongozi wa vyama, kuzuia wagombea kutogombea yanayofanywa na ofisi ya Msajili ndio yaliibua wasiwasi mwaka 2019, na kuwasukuma Wenyeviti wa zamani wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, CHADEMA, Freeman Mbowe, CHAUMMA, Hashim Rungwe, Kiongozi wa wakati ule wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe, na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA wa wakati ule Salum Mwalim kufungua kesi kwa niaba ya vyama vingine 10 katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ)
Katika kesi hiyo, vyama hivyo vya siasa vililalamika kwamba Sheria ya Vyama vya Siasa iliyokuwa imetiwa saini na rais wa wakati ule John Pombe Magufuli ilikuwa inafanya shughuli za siasa kuwa jina.
Kwa sehemu walikuwa wanalalamikia mamlaka mapana ambayo sheria hiyo ilikuwa imempa Msajili wa Vyama vya Siasa ikiwa ni pamoja na kile walichokiita uwezo wa Msajili kuingilia shughuli za kila siku na michakato ya ndani ya vyama vya siasa.
Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) iliamuru serikali ya Tanzania kurekebisha Sheria ya Vyama vya Siasa, ikiitaka kuondoa vifungu vinavyokiuka makataba ulioianzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Hata hivyo serikali bado haijafanyia marekebisho sheria hiyo.
Kutoka kuwa ‘msajili’ mpaka kuwa ‘mdhibiti’

Chanzo cha picha, Global Publishers
Tangu ukiwa katika hatua za mswaada, asasi za kiraia pia ziliikosoa sheria hiyo. Kundi lililojumlisha Twaweza, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Baraza la habari Tanzania (MCT), Centre for Strategic Litigation, Chama cha Waandishi wa Habari wa Maendeleo Zanzibar na Tanganyika Law Society lilisema sheria hiyo itakwenda kubadili majukumu ya msingi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Mswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa, 2018 unabadilisha jukumu la msingi la Msajili wa vyama vya siasa kutoka kuwa “msajili” mpaka kuwa “mdhibiti,” Kundi hilo liliandika katika uchambuzi wake wa mswaada huo
Asasi hizo pia ziliainisha kwamba sheria hiyo itakwenda kumpatia Msajili mamlaka makubwa ya kudai taarifa orodha ya wanachama, taarifa ya fedha ya chama, na taarifa yoyote itakayohitajika. Mbali na hapo, wakasema sheria inampa pia Msajili mamlaka ya kuingilia masuala ya ndani ya uongozi wa chama, kama orodha ya wanachama, kuweka vikwazo kwenye katiba za vyama, na masuala ya kinidhamu ya ndani ya chama.
Mapendekezo ya kupunguza ‘udhibiti’ wa Msajili
“Ingawa vyama vya siasa vinapaswa kudhibitiwa, lakini vilevile, katika demokrasia changa, vinahitaji kulelewa”, hii ilikuwa sehemu ya maoni ya LHRC wakati wa mchakato wa marekebisho ya sheria ili kupunguza nguvu na udhibiti wa Msajili ambao sasa unaonekana, kwa mujibu wa vyama vya siasa.
Kuenguliwa kwa Mpinga kuwania urais, ACT wanasema Msajili hana mamlaka ya kutengua uteuzi wake ndani ya chama. Inasubiriwa maamuzi ya kesi yao waliyofungua dhidi ya Msajili na Tume ya taifa ya uchaguzi kupitia Serikali. Kwa maamuzi ya wiki hii ya Mahakama Kuu kanda ya Manyara kubatilisha uamuzi wa Msajili kutengua Sekretarieti ya Chadema alioutoa mwezi Mei, yanathibitisha u]mahitaji ya jicho lingine kwenye nguvu na mamlaka ya Msajili, je ni ya ulezi na usajili au udhibiti?
Asasi za kiraia wakati huo zilipendekeza vifungu kadhaa vya sheria hiyo vibadilishwe ikiwa ni pamoja na kumpunguzia Msajili mamlaka na kumbakizia uwezo wa kushauri na kupendekeza miongozo ya chama pekee.
“Kifungu cha 4 (5)(e) kinapaswa kubadilishwa kumuondolea Msajili mamlaka ya kuingilia mapato na matumizi ya rasilimali za vyama vya siasa badala yake aandae miongozo itakayowezesha vyama kujisimamia na kuwajibika bila yeye kuingilia,” ziliandika asasi
Changamoto ya mahakama hiyo ya kikanda ya EACJ ni kwamba mara nyingi serikali huweza kupuuza maamuzi yake pasipokuwa na madhara yoyote.
Wakati madhaifu ya Tume Huru ya Uchaguzi ndio yamekuwa yakimulikwa zaidi kama kikwazo kikubwa katika mfumo wa uchaguzi nchini Tanzania, si wengi waliotarajiwa kwamba ofisi ya Msajili ingeweza kuibuka na kuwa mwiba kiasi hiki kwa chama kinachotaka kushiriki katika uchaguzi.
