Serikali za Afrika zinashirikiana na Shirika la Kimataifa la Kufadhili Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ili kusaidia mataifa ya bara hili kupunguza uagizaji wa vyakula kutoka nje na kufanikisha usalama wa chakula. 

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Rais wa IFAD, Alvaro Lario, amesema serikali nyingi barani Afrika zimekuwa zikitegemea mbinu na teknolojia kutoka kwa shirika hilo ili kuwawezesha wakulima wadogo kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza utegemezi wa chakula cha kuagizwa. 

Mahitaji mengi na umaskini bado upo barani Afrika. Serikali nyingi hazina uwezo wa kutosha kwa sababu zinatumia kati ya asilimia 10 hadi 25 ya mapato yao kulipa madeni. Hii ndiyo sababu tunahimiza sekta binafsi kujitegemea. Tunashirikiana na serikali ili kuzifadhili na kuhakikisha sekta binafsi zinajisimamia

Aliongeza kuwa bara la Afrika lina uwezo wa kujitegemea na kufanikisha usalama wa chakula, iwapo kutakuwepo na utashi wa kisiasa kutoka kwa viongozi wake. 

Upungufu wa chakula barani Afrika 

Kwa mujibu wa Lario, mmoja kati ya kila watu watano barani Afrika anakabiliwa na ukosefu wa chakula, hali ambayo ni ya juu mno ikilinganishwa na maeneo mengine duniani. 

Tunaamini nguvu zaidi zinapaswa kuelekezwa hapa. Kwa sasa dunia imejikita zaidi kwenye masuala ya vita, lakini bado tuna changamoto kubwa ya chakula. Takribani watu milioni 800 duniani hawana chakula, na Afrika inachukua sehemu kubwa ya tatizo hili. Ni lazima tuwekeze zaidi na kuhakikisha kila mmoja anakabili changamoto hii, na sisi kama IFAD tumeongeza ufadhili kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa

Uwekezaji wa IFAD barani Afrika 

Kwa sasa, zaidi ya asilimia 60 ya uwekezaji wa IFAD unafanyika barani Afrika, na matarajio yake ni kuwafikia watu milioni 100 katika kipindi cha miaka ijayo. Kupitia ushirikiano na serikali, mashirika ya wakulima wadogo, Benki ya Maendeleo ya Afrika, na wadau wengine, IFAD inalenga hasa vijana na wanawake wanaojihusisha na kilimo ili kuwapa kipato na ujuzi wa kisasa. 

Picha ya Kongamano la usalama wa chakula Barani Africa mwaka 2025.
Picha ya Kongamano la usalama wa chakula Barani Africa mwaka 2025. FLICK STUDIOS 2024

Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi 

Lario pia aligusia changamoto za mabadiliko ya tabianchi, akieleza kuwa kwa kila dola 45 zinazowekezwa na IFAD, sehemu kubwa inatengwa kwa miradi ya kukabiliana na athari zake ikiwemo mafuriko, ukame na vimbunga. 

Katika Kongamano la Usalama wa Chakula lililofanyika Dakar, Senegal, IFAD ilieleza kuwa wakulima wadogo wamepata mafunzo na ushirikiano utakaowezesha kuongeza uzalishaji wa chakula, hatua inayotarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha usalama wa chakula barani Afrika. 

Teknolojia na vijana 

Kadri hali inavyobadilika, IFAD inasema inawekeza zaidi kwenye teknolojia na uvumbuzi wa kisasa ili kuwavutia vijana kuingia kwenye sekta ya kilimo na kuifanya iwe ya kibiashara na yenye manufaa makubwa zaidi. 

Usalama wa chakula barani Afrika unabaki kuwa changamoto kuu kutokana na umaskini, mabadiliko ya tabianchi, na utegemezi wa vyakula kutoka nje. IFAD, kupitia ushirikiano na serikali, sekta binafsi, na mashirika ya wakulima wadogo, inalenga kuimarisha kilimo kwa vijana na wanawake, kuongeza uzalishaji, na kukuza teknolojia za kisasa. Hatua hizi, zikichangiwa na utashi wa kisiasa na uwekezaji endelevu, zinaweza kufanikisha ndoto ya bara la Afrika kujitegemea kwa chakula na kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *