
Kampuni ya uwekezaji ya Qatar ya Al Mansour Holding inakusudia kuwekeza dola bilioni 21 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo Doha ni mpatanishi wa mzozo mashariki mwa nchi hiyo, serikali ya Kongo imetangaza mnamo Septemba 3. Sheikh Mansour bin Jabor bin Jassim Al Thani, mwanzilishi wa kampuni hii na mwanachama wa familia ya kifalme nchini Qatar, alizuru juzi Jumanne Kinshasa akiwa katika ziara yake barani Afrika.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Wakati ujumbe wa Qatar, ukiongozwa na mmoja wa binamu za Emir, Sheikh Mansour Bin Jabor Bin Jasim Al Thani, ulikuwa Kinshasa, DRC, Jumanne, Septemba 2, haukukutana na Rais Félix Tshisekedi. Ulimkabidhi Waziri Mkuu Judith Suminwa barua ya nia ya kuahidi uwekezaji wa dola bilioni 21. Sekta kadhaa zinahusika: madini, kilimo, uvuvi, ufugaji wa mifugo, na hata afya ya umma. Mtaalamu wa siasa kutoka Kongo Christian Moleka amemweleza Paulina Zidi, mwandishi wa RFI nchini humo, kwamba hii ingewakilisha “mpango mkubwa” kwa DRC.
“Kwa DRC, uwekezaji wa dola bilioni 21 ni mkubwa sana, ni jambo kubwa. Baada ya yote, ni barua ya dhamira tu. Nchi bado inahitaji kuwa na uwezo wa kuchukua uwekezaji huu. Kongo pia inahitaji kujadiliana na IMF na Benki ya Dunia, kwa sababu kunaweza kuwa na athari za deni kwa nchi. Lakini itakuwa ni msukumo mkubwa kwa nchi na uwezekano wa ushindi wa kidiplomasia kwa Rais wa Jamhuri. Kama kesho mpango huu wa uwekezaji huu utakamilika, tutakuwa na mkutano katika ngazi ya juu serikalini na ikiwezekana kusainiwa kwa maelewano madhubuti zaidi ya utekelezaji wa ufadhili huo.”
Ziara hii ya binamu wa Amiri wa Qatar nchini DRC ni sehemu ya ziara pana zaidi barani humo. Siku moja kabla, Al Mansour alikuwa Gabon, na wiki moja kabla ya hapo, nchini Burundi, Tanzania, na Botswana, kila wakati kukiwa na uwekezaji wenye thamani ya dola bilioni kadhaa.
Baada ya kuondolewa kwa misaada ya Marekani
Ahadi hizi kubwa za kifedha kutoka Qatar zinakuja wakati nchi za Kiafrika zinakabiliwa na kupunguzwa kwa misaada ya Marekani tangu Donald Trump aingie madarakani, na huku mashariki mwa DRC ikishikiliwa na kuibuka tena kwa kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda, ambalo limeteka maeneo makubwa ya nchi hiyo.
Majaribio ya kidiplomasia ya kutatua mzozo huo yote yameshindwa hadi uingiliaji wa ghafla wa Qatar, ambao ulifanikiwa kuwaleta pamoja Rais wa Kongo Félix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame huko Doha katikati ya mwezi Machi. Nchi hizo mbili pia zilitia saini makubaliano ya amani huko Washington mwishoni mwa mwezi Juni. Mnamo mwezi Aprili, mazungumzo yalianza huko Doha kati ya Kinshasa na M23. Bado yanaendelea hadi leo, lakini bila kuzaa matunda yoyote ya kweli katika uwanja wa mapigano licha ya matamko ya kutia moyo kutoka kwa pade hasimu.