Washirika 26 wa nchi za Magharibi wamejitolea rasmi kupeleka wanajeshi “baharini, au angani” kwenda Ukraine siku moja baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema.

Imechapishwa:

Dakika 3 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Kufuatia mkutano wa kilele wa nchi 35, uliopewa jina la “Muungano wa Walio Tayari,” rais wa Ufaransa amesema kwamba msaada wa Marekani kwa jeshi lao utakamilika katika siku zijazo.

Rais Donald Trump hivi majuzi alionyesha kwamba uungwaji mkono wa Marekani “huenda” ukachukua aina ya usaidizi wa anga, na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema alijadiliana na kiongozi wa Marekani “ulinzi wa juu zaidi wa anga ya Ukraine.”

Hata hivyo, matumaini ya makubaliano ya kumaliza mapigano hayo yamefifia tangu Vladimir Putin na Trump kukutana Alaska mwezi uliopita.

Trump pia alisema Umoja wa Ulaya unapaswa kushirikiana na Marekani kukomesha uagizaji wa mafuta na gesi ktoka Urusi, ili kuzima “chombo cha vita ya Urusi kwa njia za kiuchumi,” kulingana na nakala ya mazungumzo ya simu ya Rais wa Finland Alexander Stubb.

Umoja wa Ulaya wenye wanachama 27 umeweka lengo la kukomesha uagizaji wote wa mafuta na gesi ifikapo mwisho wa mwaka 2027. Afisa wa Ikulu ya White House amebainisha kuwa Urusi ilipokea Euro bilioni 1.1 (pauni milioni 954; dola bilioni 1.3) katika mauzo ya mafuta kutoka EU katika mwaka mmoja, ingawa takwimu halisi ilikuwa kubwa zaidi.

Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer amesema washirika wa nchi za Magharibi sasa wana “dhamira isiyotetereka” kwa Ukraine, ikiungwa mkono na Marekani, na lazima kuishinikiza Urusi kukomesha vita, kulingana na msemaji wa Downing Street.

Nchi chache zimeahidi waziwazi kupeleka wanajeshi ardhini nchini Ukraine iwapo makubaliano yatafikiwa, na Marekani tayari imefutilia mbali hatua hiyo. Wanadiplomasia wa Ulaya wamependekeza kwamba ushiriki wa kijeshi katika hatua hii unaweza kuimarisha matamshi ya Putin dhidi ya nchi za Magharibi.

Moscow imeweka wazi kuwa hakuna vikosi vya Magharibi vinavyopaswa kutumwa nchini Ukraine na imesisitiza kuwa ni miongoni mwa nchi zilizotoa dhamana, wazo lililokataliwa na Kyiv na washirika wake.

Katika maoni yaliyochapishwa na vyombo vya habari vya serikali ya Urusi, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema: “Je, dhamana ya usalama ya Ukraine inaweza kutolewa na vikosi vya kijeshi vya kigeni, vikiwemo vya Ulaya na Marekani? Hapana kabisa.”

Wakati huo huo, Urusi imeendelea kutuma wanajeshi nchini Ukraine licha ya majaribio ya hivi majuzi ya mazungumzo ya kusitisha mapigano, Macron amelaumu.

Katika ghasia za hivi punde, maafisa wawili wa kutegua mabomu waliuawa katika shambulio la Urusi kaskazini mwa Ukraine siku ya Alhamisi.

Ukraine na washirika wake wanaamini usitishaji mapigano unapaswa kufikiwa kabla ya jaribio lolote la makubaliano mapana ya amani, ingawa Urusi haikubaliani nayo.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema baada ya mkutano huo kuwa kipaumbele cha kwanza ni kupata usitishaji vita katika mkutano uliohudhuriwa na Volodymyr Zelensky, na kisha kutoa “dhamana kali za usalama.”

Siku ya Alhamisi, maafisa wakuu wa Zelensky walikutana mjini Paris na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff.

Putin alipendekeza wiki hii kwamba Zelensky anaweza kusafiri kwenda Moscow kwa mazungumzo, wazo ambalo Kyiv aliliita “halikubaliki.” Kiongozi wa Ukraine alisema hii inaashiria Urusi haikutaka kwa dhati mkutano huo ufanyike.

Siku ya Alhamisi Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte alisema kwamba Urusi haina mamlaka ya kura ya turufu juu ya kutumwa kwa wanajeshi wa nchi za Magharibi nchini Ukraine: “Kwa nini tunavutiwa na maoni ya Urusi kuhusu wanajeshi wa Ukraine? Ni nchi inayojitawala. Si juu yao kuamua.”

Bw. Trump aliambia CBS News siku ya Jumatano kwamba bado amejitolea kufikia makubaliano ya kumaliza vita na akathibitisha kwamba ana uhusiano mzuri na Putin na Zelensky.

“Nadhani tutatatua hili,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *