
Msemaji wa jeshi la Israel ametangaza leo Jumamosi asubuhi kuanzishwa kwa “eneo la kibinadamu” huko Al-Mawasi, kusini mwa eneo la Palestina, akiwataka wakaazi wa mji wa Gaza kuhamia huko kabla ya shambulio la ardhini. Jeshi linahakikisha kuwa eneo hilo lina hospitali, chakula, na mahema.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Jeshi la Israel limetoa wito kwa wakaazi wa Mji wa Gaza siku ya Jumamosi, Septemba 6, kuhama hadi katika “eneo la kibinadamu” lililotengwa na Israel kusini zaidi katika Ukanda wa Gaza, kwa kutarajia shambulio lijalo la ardhini katika mji huo mkubwa zaidi katika ardhi ya Palestina.
“Kuanzia sasa na kuendelea, na ili kuwezesha kuondoka kwa wakazi wa jiji hilo, tunatangaza eneo la [pwani] la Al-Mawasi [kusini mwa Ukanda wa Gaza] kuwa eneo la kibinadamu,” ujumbe umeandika kwa Kiarabu “kwa wakaazi wa Mji wa Gaza na wote walioko” uliotumwa kwenye mitandao ya kijamii na Kanali Avichay msemaji wa jeshi la Israel kwa watu wanaozungumza Kiarabu.
“Chukueni fursa hii kuhamia eneo la kibinadamu bila kuchelewa na kujiunga na maelfu ya watu ambao tayari wamekwenda huko,” ujumbe huo unaongeza, wakati Umoja wa Mataifa unakadiria idadi ya watu waliopo katika eneo la Mji wa Gaza karibu milioni moja na kuonya juu ya “maafa” yanayokuja ikiwa mashambulizi ya Israel dhidi ya mji huo yatapanuka.
Wakati Hamas ilikubali mwezi Agosti mapendekezo ya makubaliano ya usitishwaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka huko Gaza yaliyowasilishwa na wapatanishi [Misri, Marekani, na Qatar], serikali ya Israel sasa inalitaka vuguvugu hilo la Palestina kuweka chini silaha zake, kuwaachilia mateka wote linalowashikilia, na kuachia udhibiti wa usalama wa Ukanda wa Gaza kwa Israeli, miongoni mwa mambo mengine.
“Hakuna mahali salama,” kulingana na Wapalestina
Katika taarifa nyingine, kwa Kiingereza, jeshi la Israel limeandika kwamba “eneo la kibinadamu” lililotangazwa kwa kutarajia “upanuzi wa operesheni [yake] ya ardhini huko Gaza” ni pamoja na “miundombinu muhimu ya kibinadamu kama vile hospitali, mabomba la maji na vifaa vya kuondoa chumvi, pamoja na usambazaji wa chakula, mahema, dawa na vifaa vya matibabu kwa eneo hilo.”
Anathibitisha kwamba “juhudi za usaidizi wa kibinadamu kwa eneo […] zitaendelea kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa, pamoja na upanuzi wa operesheni ya ardhini.”
Tangu kuanza kwa vita vilivyochochewa na shambulio la Hamas katika ardhi ya Israel kutoka Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, jeshi la Israel limefanya mashambulizi mengi ya mabomu katika maeneo ambayo ilikuwa imetangaza kuwa “ya kibinadamu” na “salama” kwa wakazi, likidai kuwalenga wapiganaji wa Hamas wanaojificha kati ya raia.
Makumi ya Wapalestina waliohojiwa katika Jiji la Gaza na shirika la habari la AFP katika wiki kadhaa zilizopita wamesema mara kwa mara kwamba “hakuna mahali salama” katika Ukanda wa Gaza na kwamba wangependelea kufia huko badala ya kuhamishwa tena.