
Rais wa Marekani, Donald Trump amesema siku ya Jumanne uamuzi wa Israel wa kushambulia Qatar ulifanywa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na sio na rais wa Marekani kutoka chama cha Republican ambaye ameongezea kwamba uamuzi uliochukuliwa na pande mmoja kushambulia Qatar hautumiki kwa masilahi ya Marekani au Israeli.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Israel ilijaribu kuwaua viongozi wa kisiasa wa Hamas kwa shambulio la anga nchini Qatar siku ya Jumanne, na kuzidisha hatua yake ya kijeshi katika Mashariki ya Kati. Shambulio hilo limelaaniwa pakubwa katika Mashariki ya Kati na kwingineko kama kitendo ambacho kinaweza kuzidisha hali ya wasiwasi katika eneo ambalo tayari linakabiliwa na mgogoro mkubwa.
Trump amesema alimuagiza mjumbe wa Marekani Steve Witkoff kuitahadharisha Qatar kwamba shambulio linakuja, lakini muda ulikuwa umekwisha kusitisha shambulio hilo. Hata hivyo, Qatar imepinga madai hayo kutoka kwa Ikulu ya White House, ikidai kuwa ripoti za shambulio hilo ni za uongo na kwamba simu kutoka kwa afisa wa Marekani ilikuja huku milipuko ikisikika katika mji mkuu wa Qatar, Doha.
“Shambulio la upande mmoja dhidi ya Qatar, taifa huru na mshirika wa karibu wa Marekani, ambayo inafanya kazi kwa bidii na kuchukua hatari na sisi kujadili amani, hakuendelezi malengo ya Israel au Marekani,” Trump ameandika kwenye Jukwa lake la Truth Social.
“Hata hivyo, kuangamiza Hamas, ambayo imenufaika kutokana na masaibu ya wale wanaoishi Gaza, ni lengo linalofaa.”
Hamas imesema wanachama wake watano waliuawa katika shambulio la Israel huko Doha, akiwemo mtoto wa kiongozi wa Hamas aliye uhamishoni Gazan Khalil al-Hayya.
Washington inachukulia Qatar kama mshirika mkubwa wa Ghuba. Qatar imekuwa mpatanishi katika kujaribu kusuluhisha makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la wapiganaji wa Kipalestina huko Gaza, kuachiliwa kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas, na mpango wa Gaza baada ya mzozo.
Baada ya shambulio hilo, Trump alizungumza na Netanyahu na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani.
Alimhakikishia kiongozi huyo wa Qatar kwamba “jambo kama hili halitatokea tena katika ardhi yao,” Trump amesema, akiongeza kuwa alijisikia “vibaya sana” kuhusu shambulio hilo dhidi ya Qatar.
Trump baadaye amewaambia waandishi wa habari mjini Washington kwamba “hajafurahishwa” na shambulio la Israel nchini Qatar.
“Sijafurahishwa na hilo,” Trump amesema. “Sio hali nzuri, lakini nitasema hivi: Tunataka mateka warudi, lakini hatujafurahishwa na jinsi ilivyofanyika leo.” Wakati Trump akitoa matamshi hayo, waandamanaji wanaounga mkono Palestina walikusanyika karibu na hapo wakiimba “Palestina huru” na “kukomesha mauaji ya halaiki.”
Uchokozi wa Israel unaoungwa mkono na Marekani dhidi ya Gaza tangu mwezi Oktoba 2023 umeua makumi ya maelfu ya watu, wakimbizi wa ndani wa Gaza, na kusababisha mgogoro wa njaa. Wataalamu kadhaa wa haki za binadamu na wasomi wanasema uchokozi wa kijeshi wa Israel dhidi ya Gaza ni sawa na mauaji ya halaiki.
Israel inadai kuwa hatua yake ilikuwa ya kujilinda kufuatia shambulio la mwezi Oktoba 2023 lililofanywa na wanamgambo wa Hamas wa Palestina ambapo watu 1,200 waliuawa na zaidi ya 250 walishikiliwa mateka, kwa mujibu wa hesabu za Israel. Israel pia ilishambulia Lebanon, Syria, Iran na Yemen wakati wa mzozo wa Gaza.