Hivi karibuni wanamgambo wa Boko Haram waliongeza mashambulizi yao nchini Nigeria na kuwaua zaidi ya watu 500 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025. Wachambuzi wanasema serikali ya Nigeria inahitaji kuweka mkakati mpya katika kukabiliana na kitisho hicho kinachoongezeka.
Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na shirika lisilo la kiserikali la Utawala Bora barani Afrika lenye makao yake makuu nchini Afrika Kusini, inaonyesha kwamba kuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha kuwa wanamgambo wa Boko Haram wameanzisha tena mashambulizi yao Nigeria baada ya kupungua kwa miaka kadhaa.
Kulingana na Tume ya Haki ya Binaadamu ya Nigeria, takribani watu 2,266 waliuawa na majambazi au waasi nchini Nigeria katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025, na kuipita idadi ya vifo kama hivyo katika mwaka wote wa 2024.
Malik Samuel, mtafiti mwandamizi wa Utawala Bora Afrika ameiambia DW kwamba wanashuhudia uvamizi wa usiku, sio tu dhidi ya raia, bali pia dhidi ya wanajeshi, na kwamba wanaona mashambulizi na utekaji nyara yakifanika kwenye barabara kuu na katika mashamba.
Katika shambulizi la hivi karibuni huko Darul Jaman, kaskazini mwa Nigeria, watu wapatao 60 waliuawa. Mwezi Machi, mwaka 2025 Niger ilitangaza kujiondoa kwenye Kikosi cha Pamoja cha Kimataifa MNJTF, ambacho kimepewa mamlaka ya kulinda mipaka katika ukanda wa Ziwa Chad. Awali kikosi hicho kilianzishwa na Nigeria mwaka 1994, lakini sasa kimetanuka na kupitisha mbinu ya kimataifa zaidi kwa kushirikiana na nchi jirani za Niger, Cameroon, Chad na Benin.
Wakati Niger ilipojiondoa mwaka huu, iligusia haja ya kuzingatia katika kulinda nchi yake, hasa mali zake ambazo ni mafuta na madini ya urani.
Wachambuzi wanaamini kuwa uamuzi wa Niger, kujiondoa ndani ya MNJTF, umefanya mpaka wa pamoja kati ya Nigeria na Niger kuwa na upenyo, hivyo kuwaruhusu wanamgambo kuongeza silaha zao na mashambulizi yao.
Akizungumza na DW, Oluwole Ojewale, Mratibu wa Uangalizi wa Uhalifu wa Kikanda wa Afrika ya Kati kwenye Taasisi ya Mafunzo ya Usalama yenye makao yake nchini Senegal, amesema mchakato wa usafirishaji na mipango umekuwa rahisi kwa Boko Haram katika suala la kusafirisha silaha na risasi katika eneo lao.
Utekaji nyara kwa ajili ya kudai fidia
Kwa kuongezea baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa kuna ushindani mkubwa wa rasilimani za kijeshi ambazo awali zilijazana kwenye eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria, kutokana na changamoto nyingine za kiusalama, ikiwemo mapigano kati ya wakulima na wafugaji, utekaji nyara na ujambazi. Ojewale anasema hali hiyo inaifanya jamii kuwa hatarini zaidi kwa mashambulizi ya Boko Haram.
Umoja wa Mataifa unaeleza kuwa zaidi ya watu 40,000 waliuawa na wengine wapatao milioni 2 wameyakimbia makaazi yao tangu mgogoro huo ulipozuka miaka 15 iliyopita.
Kwa miaka mingi, jeshi la Nigeria limeweka mikakati ya pande nyingi kukabiliana na uasi wa Boko Haram. Majaribio ya hivi karibuni yamejumuisha mashambulizi ya anga, ufuatiliaji wa mpaka na ushirikiano wa jumuiya. Msemaji wa Jeshi la Nigeria, Brigedia Jenerali Tukur Gasau, ameiambia DW kuwa hali ya usalama kaskazini mashariki kwa sasa imeimarika. Kulingana na Brigedia Jenerali Gasau, sehemu kubwa ya magaidi hao imeangamizwa.
Malik Samuel anapendekeza kuwa serikali inahitaji kuimarisha ushirikiano wake na watendaji wa serikali na wasio wa serikali ili kukabiliana na changamoto za kiusalama. Kwa upande wake Ojewale amehamasisha usalama wa mipakani na ushirikiano wa kimataifa.
Pia amependekeza jumuiya za kikanda kuingilia kati kama vile Jumuia ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, akisema uwekezaji katika usalama, na Umoja wa Afrika ndiyo suluhisho la haraka la mgogoro huo.