Mapema Jumatano Poland ilitangaza kuwa pamoja na washirika wake wa Jumuiya ya NATO wamedungua droni za Urusi zilizovamia anga yake, na kulitaja tukio hilo kama “kitendo cha uchokozi”, wakati Urusi ikiendeleza mashambulizi ya anga dhidi ya Ukraine.

Kupitia mtandao wa X, Waziri Mkuu wa Poland, Donald Tusk, amesema anga ya Poland ilivamiwa na idadi kubwa ya droni za Urusi na zilikuwa tishio la moja kwa moja zilidunguliwa.

“Hii ni mara ya kwanza kwa droni za Urusi kudunguliwa juu ya anga ya eneo la nchi mwanachama wa NATO, ndiyo maana washirika wetu wote wanachukulia hali hii kwa uzito mkubwa. Lakini hatujarekodi vifo vyovyote.”

Jeshi la Poland limesema linaendelea na msako katika maeneo yalipoanguka mabaki ya droni na kutoa ilani kwa wananchi kutokukaribia, kugusa au kuhamisha vitu vyovyote watakavyoviona, kwani vinaweza kuwa hatari na kuwa na kemikali hatarishi.

Zelensky akosoa “Uchokozi wa Urusi”

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema ndege za Urusi kuvuka mpaka na kuingia Poland si ajali, bali ni uchokozi.Picha: Tetiana Dzhafarova/AFP/Getty Images

Zelensky amesema kitendo cha ndege za Urusi kuvuka mpaka na kuingia Poland si ajali, bali ni “kielelezo hatari” cha uchokozi, na kwamba ni ishara ya makusudi ya Urusi kudhalilisha nchi mwanachama wa Umoja Ulaya na Jumuiya ya NATO.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amelaani vikali uvamizi wa anga wa Urusi nchini Poland, akisema ni jambo lisilokubalika. Spika wa Bunge la Umoja wa Ulaya Roberta Metsola amesema:

“Poland ina haki kamili ya kujilinda. Bado tunachunguza kilichotokea. Tumeona kauli ya Waziri Mkuu na serikali ya Poland. Lazima ieleweke, kwamba Poland ina haki zote za kujilinda dhidi ya mashambulizi yoyote.  Umoja wa Ulaya, unapaswa kujibu vipi uchokozi huu? Tunasimama pamoja. Hii si tu nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya, bali pia ni nchi mwanachama wa NATO. Na hapa ndio uwezo wetu wa pamoja wa ulinzi na usalama unapotakiwa kuwajibika, kuonyesha utayari wetu wa kukabiliana na vitisho vya mashambulizi kama haya.”

Belarus iliionya Poland na Lithuania

Poland 2025
Belarus iliwajulisha Poland na Lithuania kuhusu droni za Urusi, hatua iliyosaidia Poland kuchukua hatua za haraka.Picha: Dominika Zarzycka/SOPA Images/ZUMA/picture alliance

Katika tukio jengine, Belarus pia ilidungua baadhi ya droni zilizopotea njia kutokana na vita vya kielektroniki kati ya Urusi na Ukraine. Mkuu wa Majeshi wa Belarus, Meja Jenerali Pavel Muraveiko, amesema nchi yake iliwajulisha Poland na Lithuania kuhusu ndege hizo, na kwamba hatua hiyo ilisaidia Poland kuchukua hatua za haraka.

Kwa upande wa Umoja wa Ulaya, Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amependekeza kutumia fedha zilizozuiwa za Urusi kufadhili mkopo wa fidia kwa Ukraine, bila kugusa mali zenyewe. Amesema ni Urusi inayopaswa kulipa gharama za vita inavyoendeleza.

Tukio hili linaweza kujumuishwa katika mijadala ya kuimarisha vikwazo dhidi ya Moscow. Nchi za Ulaya zinatumai kumshawishi Rais wa Marekani, Donald Trump, kujiunga nao katika kuweka vikwazo baada ya mazungumzo ya amani ya mara kwa mara kushindwa kufikia muafaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *