Haya yanajiri wakati wa mashambulizi dhidi ya Ukraine, akionya kuwa hali hiyo inakaribia kuwa “mgogoro wa wazi.” Haya yanajiri huku wizara ya Ulinzi ya Urusi ikikanusha kuilenga Poland.
Tusk amesema droni 19 za Urusi ziliingia kinyume cha sheria katika anga ya Poland, huku jeshi lake la Poland pamoja na washirika wake wakifanikiwa kudungua droni tatu. Ingawa hakuna mtu aliyejeruhiwa, vyombo vya habari vya ndani vilionyesha picha za nyumba iliyoharibiwa katika kijiji cha Wyryki, mashariki mwa Poland, kufuatia athari ya droni.
Tusk amesema ameanzisha matumizi ya Kifungu cha 4 cha Jumuiya ya NATO, kinachoruhusu mwanachama yeyote kuomba mashauriano ya dharura iwapo anaona usalama wake, uhuru wa kisiasa au mipaka yake ya kieneo iko hatarini — na hii ni mara ya nane katika historia hatua hiyo kuchukuliwa.
Urusi yaendelea na mashambulizi Ukraine
Tukio hilo lilitokea wakati Urusi ikiendeleza mashambulizi makubwa nchini Ukraine, ikiwemo katika jiji la Lviv lililo karibu na mpaka wa Poland. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ameutaja uvamizi wa anga ya Poland kama “mfano hatari” kwa Ulaya na kwamba haikuwa ajali, akitoa wito kwa washirika wa Magharibi kuchukua hatua kali.
Baraza la Jumuiya ya kujihami ya NATO, ambalo ndilo chombo kikuu cha maamuzi ya kisiasa ndani ya muungano huo, lilibadilisha muundo wa kikao chake cha kila wiki siku ya Jumatano na kukifanya kikao hicho kufanyika chini ya Kifungu cha 4 cha mkataba wa NATO.
Msingi mkuu wa muungano huo wa kijeshi ni kwamba shambulio dhidi ya mwanachama yeyote linachukuliwa kama shambulio dhidi ya wote.
Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, alisifu kile alichokiita “muitikio wa mafanikio makubwa” wa muungano huo, akiiambia vyombo vya habari kuwa ulinzi wa anga wa NATO umetimiza wajibu wake ipasavyo.
“Kama nilivyosema, bado tunaendelea kufanya tathmini, lakini bila shaka, iwe ni kwa makusudi au la, kitendo hiki ni cha uzembe na pia ni cha hatari sana. Kwa Putin, ujumbe wangu ni wazi: Sitisha vita dhidi ya Ukraine, sitisha vita vinavyozidi kuongezeka, ambavyo vielekezwa kwa raia wasio na hatia na miundombinu ya kiraia. Acha kuingia kwenye anga ya washirika wa NATO. Fahamu tuko tayari, tuko macho, na tutalinda kila eneo la nchi za NATO.”
Hata hivyo wizara ya Ulinzi ya Urusi imekanusha kuilenga Poland, kwa kusema hakukua na nia ya kulenga maeneo yake na iko tayari kuzungumza na Warsaw.