
Jeshi nchini Poland limesema mapema hivi leo kwamba limezidungua droni za Urusi zilizokiuka anga yake wakati wa mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine. Droni hizo zilizodunguliwa zililenga kulishambulia eneo la magharibi mwa Ukraine linalopakana na Poland.
Kufuatia tukio hilo, Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba amepokea ripoti kutoka kwa Kamandi ya Utendaji ya Jeshi kuhusu kudunguliwa kwa droni hizo za Urusi zilizoingia kwenye anga la nchi hiyo.
Tusk ameweka wazi kwamba nchi yake iko tayari kujibu mashambulizi yoyote au uchochezi wowote wa Urusi na kwamba wanajiandaa kwa matukio mbalimbali yanayoweza kujiri kutokana na vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.
Katika upande mwingine, Msemaji wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Allison Hart amesema baraza la jumuiya hiyo limefanya mkutano mapema leo na kujadili jinsi watakavyoweza kuchukua hatua kuhusu droni za Urusi zilizoingia Poland usiku wa kuamkia leo.