Wataalamu wa katiba na siasa wanasema Nepal inaweza kukumbwa na machafuko ya kisiasa na kikatiba kwa muda mrefu iwapo hakutakuwepo na makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Ripoti ya mwandishi wa DW, Lekhanath Pandey, inachunguza nini kitakachofuata baada ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Khadga Prasad Oli, na inasomwa studioni na Najjat Omar.))

Waziri Mkuu wa Nepal, Khadga Prasad Oli, alijiuzulu Jumanne baada ya kufanyika maandamano makubwa ya kupinga serikali, hatua iliyozidisha sintofahamu ya kisiasa kwenye taifa hilo maskini katika eneo la milima ya Himalaya.

Katika barua yake ya kujiuzulu, Oli alisema kuwa amechukua hatua hiyo kwa kuzingatia hali tete ya kisiasa nchini, ili kusaidia kutafuta suluhisho la amani kwa mujibu wa katiba.

Maandamano hayo yalifikia kilele baada ya waandamanaji kuchoma moto nyumba za viongozi wakuu wa kisiasa, kama ya Rais Ram Chandra Poudel na ile ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Ramesh Lekhak.

Nepal Kathmandu | Militäreinsatz nach Protesten
Wanajeshi wa Nepal wakishika doria karibu na ofisi ya Waziri MkuuPicha: Navesh Chitrakar/REUTERS

Wataalamu wa katiba wanasema, hakuna kifungu bayana katika katiba ya Nepal kinachoeleza hatua za kuchukuliwa katika hali kama hii. Profesa Bipin Adhikari wa Chuo Kikuu cha Kathmandu anapendekeza Rais kuunda serikali ya makubaliano ya kitaifa, ambapo Waziri Mkuu achaguliwe na bunge kwa mujibu wa katiba ya mwaka 2015, huku matakwa ya vijana wa kizazi cha Gen Z yakizingatiwa kwa kuwapa nafasi ya uwakilishi katika mazungumzo.

Mtaalamu wa siasa C.D. Bhatta kutoka shirika la Friedrich Ebert Foundation (FES) Nepal anasema kuwa uhalali wa vyama vikuu vya siasa nchini humo umepotea. Kwa sasa, kila upande unajaribu kutumia fursa ya machafuko hayo ili kujipatia nafasi ya kuongoza serikali.

Bhatta alisisitiza kuwa suluhisho pekee ni kuunda serikali ya kiraia inayoungwa mkono na Jeshi la Nepal, hadi pale uchaguzi mpya utakakofanyika. Hali hii, amesema, ndiyo njia pekee ya kuhakikisha utulivu na usalama wa taifa.

Nepal, nchi isiyo na bandari inayopakana na mataifa mawili makubwa—India na China—imekumbwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa na kuyumba kwa uchumi kwa zaidi ya miongo miwili.

Majengo ya serikali yachomwa moto

Machafuko ya sasa yalianza baada ya serikali kutangaza marufuku ya matumizi ya mitandao 26 ya kijamii ambayo haijasajiliwa ndani ya nchi, ikiwemo Facebook, X (zamani Twitter), YouTube, LinkedIn na WhatsApp, kwa madai kuwa hazijatimiza masharti ya kuanzisha ofisi ya mawasiliano nchini humo.

Wakosoaji wameitaja hatua hiyo kuwa ni jaribio la kukandamiza uhuru wa kujieleza na kuzuia sauti za upinzani. Maandamano hayo, yanayoongozwa na vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 30, hayana viongozi rasmi. Waandamanaji wanapinga kile wanachokiita ufisadi sugu na maisha ya kifahari ya watoto wa viongozi wa kisiasa, huku vijana wengi wakikabiliwa na ukosefu wa ajira bora.

Maelfu ya waandamanaji walimiminika katika mitaa ya Kathmandu na kuizingira bunge. Vikosi vya usalama vilifyatua risasi, na kuwaua watu 19 pamoja na kujeruhi takriban wengine 150. Mashirika ya haki za binadamu, likiwemo Amnesty International Nepal, yamelaani matumizi ya nguvu kupita kiasi na kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru na wa haki.

Kufuatia shinikizo kubwa, serikali ililazimika kuondoa marufuku ya mitandao ya kijamii siku ya Jumanne asubuhi, kabla ya Waziri Mkuu Oli kutangaza kujiuzulu kwake.

Hata hivyo, maandamano yameendelea licha ya kutangazwa kwa amri ya kutotoka nje kwa muda usiojulikana jijini Kathmandu.

Jeshi la Nepal limewataka wananchi kudumisha utulivu, huku mataifa jirani na washirika wa kimataifa kama India, Australia, Ufaransa, Ujerumani, Marekani, Korea Kusini na mengine yakitoa wito wa kuepuka machafuko zaidi na kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa msingi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *