Visa vya udanganyifu wa imani za kiroho katika eneo la Kilifi pwani ya Kenya vimeonekana kujirudia ambapo wahubiri wanadaiwa kutumia imani potofu kidini kuwadhibiti wafuasi wao kwa kuwashawishi kutokula na kunywa hadi kufa kama njia ya pekee ya kukutana na Mungu.

Baadhi ya viongozi wanasema hali hii inachochewa zaidi na kukosekana kwa elimu ya kutosha na udhaifu wa usimamizi wa serikali, hali inayowaacha wananchi wengi katika hatari ya kupoteza maisha.

Visa vya waumini kufunga kula na kunywa hadi kufa, si jambo geni tena kwa jamii za pwani ya Kenya hasa katika Kaunti ya Kilifi. Wokovu umekuwa ukisababisha vifo vya mamia ya waumini walioahidiwa kwenda mbinguni na viongozi wao wa kidini.

Miili iliyofukuliwa msituni Kwa Binzaro huko Kilifi imezusha mjadala na kuleta kumbukumbu ya yaliyojiri Shakahola mwaka 2023.

Cha kushangaza ni kuwa makaburi hayo yamepatikana hatua chache na nyumbani kwa mhubiri anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya Shakahola, Paul Mackenzie.

Serikali yaahidi kuimarisha udhibiti wa makanisa na taasisi za kidini

Zero Kahindi ambaye ni kiongozi wa vijana Kilifi nchini Kenya anaeleza kuwa kujirudia kwa kisa hiki ni ishara tosha kuwa serikali imeshindwa kuwadhibiti viongozi wa kidini wenye kusambaza imani potofu, na pia wananchi kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu dini jambo linalosababisha urahisi wa kuwashawishi kujiua.

“Tunakosa sana ufahamu, na ufahamu wa vitu mbalimbali na tuna matarajio mengi kwa hali zetu za kiuchumi na za kiimani, ndio maana unapata watu wanaweza kubebwa kwa urahisi sana na kuamini vitu bila kuuliza.”

Baadhi ya viongozi Kilifi wanadai kuwa umasikini wa kupindukia unawaacha wakaazi kudanganywa kwa urahisi na wahubiri wenye mvuto wanaoahidi kuwapatia miujiza. Kauli hii inapingwa na watetezi wa haki za binaadam kama Enos Opiyo, kutoka shirika la Dream Achievers Youth Organisation Pwani ya Kenya.

Nini huwashawishi watu kufuata imani zenye utata za kidini?

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

“Kuna watu ambao wameuza mali yao ili kuingia kwa madhehebu haya kwa hivyo si ufukara upande wao,lakini huenda ikawa ni tamaa ya wale viongozi wa kidini ambao si wa kidini, dini safi lakini ile dini potovu”

Anindo Temba kutoka Kaunti ya Vihiga magharibi mwa Kenya, ndiye anayeshukiwa kuongoza madhehebu yanayowashawishi watu kufunga hadi kufa katika msitu wa Kwa Binzaro kaunti ya Kilifi.

Anindo mwenye umri wa miaka 30, anaishi katika eneo la Kaoeni ambako kuna nyumba mbili. Waumini kutoka sehemu mbalimbali za Kenya walikuwa wakipokelewa katika nyumba hizo kabla ya kufundishwa kujiunga na imani hizo zenye utata.

Kufikia sasa miili ya takribani watu 34 imefukuliwa huku washukiwa 11 wakikamatwa, wakiwemo wale wanaotajwa na maafisa wa upelelezi kuwa viongozi wakuu wa makundi ya kiimani ya siri yanayowashawishi wafuasi wake kujiingiza kwenye ibada hatari.

Wachunguzi wameonya kuwa bado kuna makaburi zaidi yanayosubiri kuchunguzwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *