Kadri idadi ya vifo vya wanajeshi wa Korea Kaskazini wanaopigana upande wa Urusi nchini Ukraine inavyoongezeka, utawala wa Pyongyang umeamua kuweka wazi kuhusu idadi ya vifo hivyo na hata kujaribu kutumia simulizi za kujitoa muhanga kama nyenzo ya propaganda ili kuimarisha utii na mshikamano wa wananchi wake.
Korea Kaskazini inafanya hivyo ikilenga pia kumuonyesha mshirika wake Moscow kwamba inatuma wapiganaji waaminifu na jasiri.
Idadi ya vifo miongoni mwa wanajeshi wa Korea Kaskazini wanaopigana upande wa Urusi katika vita dhidi ya Ukraine inaendelea kupanda, na utawala wa Pyongyang unavitumia kama nyenzo ya propaganda kuimarisha utiifu wa wananchi wake.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, vyombo vya habari vya taifa vilirusha makala ya televisheni kuhusu wanajeshi wa Korea Kaskazini walioko Ukraine, ikiwemo simulizi za wanajeshi wawili vijana — Yun Jong-hyuk mwenye umri wa miaka 20 na Woo Wi-hyuk mwenye miaka 19 — ambao walijilipua kwa bomu ili kuepuka kukamatwa. Kifo chao kiliwasilishwa kama “sadaka ya kishujaa”
Korea Kaskazini yatuma zaidi ya wanajeshi 10,000 kusaidia Urusi
Wachambuzi wanasema simulizi kama hizi huimarisha ushawishi wa serikali, kwa kuwa raia hawana vyanzo mbadala vya habari. Min Seong-jae, Profesa wa Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Pace, Marekani, amesema serikali hutumia mafunzo ya kifikra kama njia ya kuelimisha wanajeshi wa sasa na vizazi vijavyo.
Vipindi hivyo vya televisheni pia vilionyesha matukio mengine ya wanajeshi waliouawa wakijitoa mhanga, jambo lililoenea zaidi baada ya askari wawili waliojeruhiwa kujisalimisha kwa majeshi ya Ukraine. Kwa mujibu wa Min, picha za wanajeshi wakijilipua zinaendana na simulizi la muda mrefu la serikali kuhusu “uaminifu wa hali ya juu.”
Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini pia vimeonyesha kiongozi Kim Jong Un akiinama mbele ya picha za wanajeshi waliokufa, akiwafariji familia zao na kuonekana kulia mazishini. Min anaeleza kuwa picha hizi zimetengenezwa kuonyesha mshikamano na kuwasilisha ujumbe kwamba kujitoa muhanga ni ushujaa, si hasara.
Siku mbili baada ya makala hiyo kurushwa, Idara ya Ujasusi ya Korea Kusini (NIS) ilikadiria kuwa kati ya wanajeshi 13,000 waliopelekwa na Pyongyang kupigana kwa niaba ya Urusi, tayari 2,000 wameuawa. Wachambuzi wanasema ujumbe huu unalenga si tu hadhira ya ndani bali pia washirika wa Moscow, kuonyesha kwamba Korea Kaskazini inatoa wanajeshi jasiri kwa vita hivyo.
Katika nchi zilizo huru zaidi, picha kama hizo zingepunguza morali na kuzua maswali magumu kuhusu sababu ya kuwatuma vijana kufa ugenini. Lakini kwa Korea Kaskazini, udhibiti mkali wa taarifa unafanya simulizi hizi kuonekana kama alama ya kujivunia mshikamano wa taifa.
Erwin Tan, Profesa wa Siasa za Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Hankuk, Seoul, anasema huenda baadhi ya wanajeshi walilazimishwa kujiua baada ya kutuhumiwa kukimbia mapambano au kufanya vibaya vitani. Kwa mtazamo wake, video hizo zinaweza pia kuwa onyo kwa wanajeshi wengine kwamba “woga na uzembe havitavumiliwa.”
Propaganda ya hivi karibuni imeenda mbali zaidi kwa kudai kwamba wanajeshi wa Korea Kaskazini walipelekwa Ukraine kwa sababu Marekani, Korea Kusini na Japani walituma vikosi upande wa Kyiv. Kwa raia wa Kaskazini, waliokuzwa katika simulizi za kudumu za “maadui wa milele,” vita vya Ukraine vinapewa sura ya mapambano ya moja kwa moja ya kujilinda.
Kwa mujibu wa Min, simulizi hizi huchochea hisia za kisiasa za kujivunia, kulipiza kisasi na kustahimili, na huficha ukweli kwamba wanajeshi wa Korea Kaskazini wanakufa kwa maslahi ya Moscow, si ya taifa lao.