Matamshi yaliyotoloewa na Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Al Thani kabla ya kutoa hotuba kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo yanadhihirisha kuongezeka kwa ghadhabu miongoni mwa mataifa ya Ghuba juu ya shambulizi hilo la Israel, lililowaua watu sita.
Sheikh Al Thani amekiambia kituo cha utangazaji cha CNN cha nchini Marekani kwamba alifanya mazungumzo na moja ya familia za mateka asubuhi ya siku ya shambulizi na kusema familia hizo zina matarajio makubwa mno na mazungumzo yanayoendelea Qatar ya kusitisha mapigano.
Akasema kile alichokifanya Netanyahu siku ya Jumanne ni kuua kabisa matumaini yoyote ya kuachiliwa kwa mateka hao. Mataifa ya Qatar na Misri wamekuwa wapatanishi wanaojaribu kuratibu makubaliano ya kusitisha vita huko Gaza
Viongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas pia wako mjini Doha kwa miaka kadhaa kwa sehemu kufuatia ombi la Marekani ili kuhamasisha kufikiwa makubaliano kati ya kundi hilo na Israel.
Qatar kuandaa mkutano wa kilele kujadili shambulizi hilo
Serikali ya Qatar tayari imemuandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pamoja na Korea Kusini ambayo mwezi huu ni mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wakilaani vikali shambulizi hilo la Doha huku Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Safadi, akiishutumu Israel kwa kuendeleza uchokozi.
“Pia tunatuma ujumbe kwa ulimwengu: mashambulizi hayo yanathibitisha kwamba serikali ya Israel inaendeleza uchokozi, inaendelea kukiuka sheria za kimataifa, kupuuza sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na kutoheshimu mamlaka ya nchi nyingine. Sasa ni wakati wa ulimwengu kuchukua hatua na kutumia zana za kisheria za kimataifa ili kuzuia tabia ya uchokozi ya Israel.”
Muda mfupi uliopita, taarifa zilisema Doha itakuwa mwenyeji wa mkutano wa dharura wa kilele wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu utakaofanyika siku ya Jumapili na Jumatatu ijayo ili kujadili shambulizi hilo hii ikiwa ni kulingana na barua ya mwaliko kutoka shirika la habari la Qatar.
Israel yadai kudungua roketi kutoka Yemen
Katika hatua nyingine, Jeshi la Israel limesema leo kwamba limedungua roketi iliyofyatuliwa kutoka Yemen, hatua iliyosababisha ving’ora yya usalama kuwaka katika baadhi ya maeneo ya nchi. Jeshi hilo limesema mifumo ya kujilinda angani ilifanikiwa kudungua roketi hiyo na hakukuwa na majeruhi wala uharibifu vilivyoripotiwa.
Jana Jumatano Israel ilianzisha raundi nyingine ya mashambulizi makubwa nchini Yemen na kuwaua karibu watu 35, siku chache baada ya waasi wa Houthi kuushambulia uwanja wa ndege wa Israel kwa droni.
Shambulizi hilo la Israel pia limewajeruhi zaidi ya watu 130, hii ikiwa ni kulingana na Wizara ya Afya inasimamiwa na waasi wa Houthi, na juhudi za kufukua vifusi ili kuwasaka waliofukiwa zinaendelea. Wengi waliuawa kwenye mji mkuu Sanaa ambako makao makuu ya jeshi na kituo cha mafuta vilishambuliwa.