Viongozi wa Ulaya wameonyesha kila hatua za kuiunga mkono kikamilifu Poland baada ya nchi hiyo kuripoti siku ya Jumatano kwamba ilidungua zaidi ya dazeni moja ya ndege zisizo na rubani za Urusi zilizoruka juu ya anga yake, jambo hilo limezua hofu ya kuongezeka kwa vita vya Urusi nchini Ukraine.
Tukio hilo linaashiria mara ya kwanza kwa ndege zisizo na rubani za Urusi kudunguliwa katika eneo la nchi mwanachama wa NATO.
Hatua hiyo inaonesha kuwa nchi wanachama wa muungano huo wa kijeshi zinaweza kuijibu Urusi kwa kuzingatia vitisho vya nchi hiyo vinavyozidi kuongezeka.
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk, amekitumia Kifungu cha 4 cha mkataba wa NATO, ambacho kinaruhusu kufanyika mashauriano iwapo nchi yoyote mwanachama itahisi kutishiwa eneo lake, uhuru wake wa kisiasa au usalama wake.
Hata hivyo Urusi imekanusha kuhusika na vitendo vya uvunjifu wa sheria kwa droni zake kuingia kwenye anga ya Poland huku Wizara ya Ulinzi ya Urusi ikitangaza kuwa Moscow haikuwa na mipango ya kulenga miundombinu ya nchini Poland.
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk amewataka raia wa Poland wasiamini na wasifuate taarifa potofu na kwamba wajiepushe na kuzisambaza zaidi taarifa kama hizo kutoka Urusi.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura kwa ombi la Poland. Mkutano huo wa dharura umeitishwa kwa ajili ya kujadili hali iliyojitokeza ya Urusi kukiuka sheria na kuruhusu droni zake kuingia katika anga ya Poland.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametoa wito kwa nchi za Ulaya kuijibu Urusi kwa vitendo na sio kwa maneno matupu baada ya ndege zisizo na rubani za Urusi kuingia katika anga ya Poland.
Zelensky amesema, “Kwa bahati mbaya, Urusi haijapokea majibu makali kutoka kwa viongozi wa kimataifa haijapokea majibu kwa vitendo. Kuna kauli za kutosha lakini bado kuna uhaba wa hatua. Urusi inapima jinsi majeshi ya nchi za NATO yanavyofanya kazi, kile wanachoweza na ambacho hawawezi kufanya.”
Kwa upande wake China imesema inatarajia mzozo unaokua kati ya Urusi na Poland ungetatuliwa kwa njia ya “mazungumzo”. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Lin Jian amesema China inazihimiza pande zote zinazohusika kusuluhisha mizozo kwa njia ya mazungumzo na mashauriano.
Vyanzo: DPA/RTRE/AFP