Israel imewaamuru wakaazi wanaoishi huko Gaza City kuondoka wakati ikizidisha vita vyake dhidi ya kundi la Hamas lakini usalama mdogo, kukosa mahala pa kwenda na hata chakula ambavyo pengine wangepata kwenye maeneo mengine, kwa ujumla vinawafanya Wagaza kufanya maamuzi magumu.
Mmoja wa wakaazi hao Abu Ahmed ambaye yeye na familia yake walikuwa wanajiandaa kukimbia kwenye mji huo alikuwa akilalamika kwamba ni karibu miaka miwili sasa, hawajawahi kupumzika, kutulia ama hata kulala vizuri kwa sababu wamekuwa ni watu wa kuhamahama kila wakati, akamalizia kwa kusema wamechoka sana.
Pamoja naye nia Alfet al-Jamal ambaye hana makazi amesema hema lake limeharibiwa na sasa hajui atafanya nini. ”Hema langu limechanika, ntafanyaje sasa jamani? Nataka kwenda upande wa kusini, lakini huko kwenyewe kunashambuliwa na mabomu. Mbali na hilo, mazingira hayaruhusu kuhamia huko kwa sababu hatuna pesa. Tunatumaini kwamba mataifa yote ya Kiarabu yatatutetea.”
Israel iliwaua watu 18 kwenye eneo hilo leo Alhamisi hii ikiwa ni kulingana na vyanzo vya tiba vya eneo hilo, ikiwa ni pamoja na watu 11 waliouawa kwenye mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Gaza City na watano kwenye eneo moja lililopo kwenye kambi ya wakimbizi iliyoko ufukweni na wengine wawili waliokuwa wakitafuta chakula karibu na Rafah.
Israel imerejea tena kuishambulia Nasser
Vikosi vya ardhini vya Israel vimekuwa vikifanya mashambulizi kwenye baadhi ya maeneo ya Nasser mwanzoni mwa vita Oktoba 2023, lakini kombora lililoangushwa usiku wa jana liliwatia hofu wakaazi kwamba huenda vifaru vikaingia hivi karibuni kukidhibiti kitongoji hicho.
Wiki iliyopita, vikosi vya Israel vimekuwa vikifanya operesheni yake kwenye vitongoji vitatu vya mashariki mwa Gaza City vya Shejaia, Zeitoun na Tuffah na kupeleka vifaru kwa muda mfupi kwenye mji wa Sheikh Radwan unaopakana na Nasser. Jeshi hilo limesema hadi sasa linadhibiti asilimia 40 ya Gaza City.
Ukosoaji waongezeka dhidi ya Israel
Ukosoaji umeendelea kutolewa dhidi ya Israel. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, David van Weel amesema ameiagiza wizara yake kuandaa agizo la kuzuia uingizwaji wa bidhaa zinazozalishwa kwenye makaazi ya walowezi kwenye eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu, kufuatia mipango ya Israel kwenye Ukingo wa Magharibi na mashambulizi yake huko Gaza na kwamba hatua hizo zianze kutekelezwa mara moja
Mwezi uliopita, mtangulizi wake Casper Veldkamp alijiuzulu kwa sababu hakuwa na uungwaji mkono wa kutosha wa bunge kuhusiana na hatua zaidi dhidi ya Israel.
Mtendaji Mkuu wa Shirika la ndege la Ryanair la nchini Uingereza Michael O’Leary naye amesema huenda wasirejeshe safari zao nchini Israel kutokana na machafuko yanayohusiana na vita huko Gaza. Awali lilisema litarejesha safari pengine kuanzia Oktoba 25.
Na Waziri wa Michezo wa Uhispania Pilar Alegria jana Jumatano amesema timu za Israel zinapaswa kuzuia kushiriki michuano mbalimbali sawasawa na hatua zilizochukuliwa dhidi ya timu za Urusi baada ya kuivamia Ukraine mwaka 2022, akiangazia kile kinachoonekana kama “undumila kuwili”.