Kampuni ya utengenezaji viberiti ya nchini Kenya – Match Masters Limited – imewasilisha shauri la dharura katika Mahakama ya haki ya Afrika Mashariki dhidi ya serikali ya Tanzania, ikipinga ushuru wa forodha ulioanzishwa na nchi hiyo mwezi Julai kupitia sheria ya fedha ya mwaka huu 2025.
Ushuru huo unajumuisha bidhaa zinazotoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kampuni hiyo inadai huo ni ukiukwaji wa mktaba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo kongwe Barani Afrika.
Kampuni hiyo yenye makao yake makuu nchini Kenya ambao ni watengenezaji wa viberiti vya Kasuku, Tinga na Paka, imebainisha kwamba kwa Tanzania kuondoa tozo ya bidhaa zake za viberiti, huku ikitoza ushuru kwa viberiti vinavyotengenezwa Kenya, hatua hiyo inakiuka ibara ya 75 kifungu kidogo cha nne na ibara ya 75 kifungu kidogo cha sita ya mkataba wa Afrika Mashariki.
Vifungu hivyo vinatoa zuio la vikwazo vipya vya kifedha katika bishara ya ndani ya jumuiya hiyo, na pia zinakataza hatua za kibaguzi dhidi ya bidhaa kutoka nchi wanachama.
Match Masters yataka ushuru ufutwe
Mkurugenzi mtendaji wa wa kampuni hiyo Raj Shah, ameiambia DW kwama, wanaitaka Tanzania kusitisha mara moja vikwazo hivyo katika biashara.
“Kwa bahati mbaya baadhi ya tozo zilizowekwa na sheria mpya ni za kibaguzi dhidi ya wazalishaji wa bidhaa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tozo hizo zinazosimamiwa na sheria ya Tanzania zinatoa taswira kwamba bidhaa za Kenya ni sawa na zile zinazotoka Kenya au nchi za Ulaya kitu ambacho sio sahihi.”
Shah ameongeza, “Kwa msingi huo, tunaiomba serikali ya Tanzaniaa ifanye mapitio ya sheria hiyo ya fedha na kuendelea kusimamia ahadi zake kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tumeiomba Mahakama kutoa zuio la dharura dhidi ya tozo hii ya kibaguzi, kwa sababu inakwenda kinyume na makubaliano yote ambayo nchi zetu zimeridhia.”
Tanzania ilipitisha sheria mpya ya fedha mwezi Julai mwaka huu 2025, huku baadhi ya vifungu vyake vikilalamikiwa na Mataifa jirani wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwamba vinakiuka misingi ya kibishara na soko huria ambayo Tanzania kama ilivyo nchi zingine wanachama imeridhia.
Wanasema kampuni hiyo ya Viberiki kama inatambulika katika nchi mwanachama inahaki ya kisherika kufungua mashtaka.
“Kama kampuni hiyo imesajiliwa katika nchi mwanachama wa Jmuiya ya Afrika Mashariki, inaweza ikasikilizwa hiyo haina shida. La pili, mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na itifaki zake zimeweka bayana kwamba, wananchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na bidhaa, hakutakuwa na vizuizi ama vikwazo ama ubaguzi, kutakuwa na soko huria,” amesema Denis Moses Olushangai, wakili wa kujitegemea.
Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki imethibitisha kupokea shauri hilo japo haijabainika ni lini hasa litatolewa maamuzi.