Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utaamua kupitia sanduku la kura kama unaunga mkono makubaliano yaliyokuwa yakifahamika kama “Azimio la New York,” linalolenga kufufua upya mpango wa kuwa na suluhisho la mataifa mawili ya Israel na Palestina bila uwepo wa Hamas.
Azimio hilo linalokusudia kuleta usuluhishi wa amani Palestina na utekelezaji wa suluhisho la nchi mbili linalitaka kundi la Hamas liwaachilie huru mateka wote. Linaeleza pia kuwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linayalaani mashambulizi yaliyofanywa na Hamas dhidi ya raia Oktoba 07.
Zaidi linatoa wito wa hatua ya pamoja katika kuvimaliza vita Gaza ili kupata haki na suluhisho la kudumu kwa kuzingatia utekelezaji wa suluhisho la nchi mbili, Palestina na Israel.
Ujerumani kuunga mkono azimio la New York
Ujerumani imesema italiunga mkono azimio hilo japokuwa haiamini kama ni wakati sahihi wa kuitambua Palestina kama taifa.
Nchi nyingine zilizoweka wazi kuwa zitaiunga mkono Palestina kuwa taifa ni pamoja na Ubelgiji, Ufaransa, Australia Uingereza na Canada.
Hayo yanajiri wakati Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman al-Thani akitazamiwa kufanya mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump kujadili shambulio la Israel la hivi karibuni mjini Doha.
Katika mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika mjini New York kati ya Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman al-Thani na Rais wa Marekani Donald Trump watajadili pia kuhusu yalikofikia mazungumzo ya kusitisha vita Ukanda wa Gaza.
“Juhudi zetu zimethibitisha kuwa ushirikiano na Marekani pamoja na Misri zimeleta matokeo yanayooonekana. Zilisababisha mateka 148 wakaachiliwa huru na misaada ikaingizwa Gaza. Zilileta mwanga wa matumaini: Lakini kushambulia eneo letu wakati tukifanya juhudi za usuluhishi kumeonesha nia ya Israel. Ni kufifisha matarajio yoyote ya amani na kuongeza madhila kwa Wapalestina.”
Kwa mujibu wa Wizara ya mambo ya Kigeni ya Marekani, al Thani atakutana pia na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio na mjumbe maalum Steve Witkoff.