Medvedev amesema kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba kutelekeza wazo la kuiwekea Ukraine ulinzi wa anga na kuyaruhusu mataifa ya NATO kuzidungua droni za Urusi kunamaanisha kwamba muungano huo wa kijeshi sasa utakuwa moja kwa moja vitani na Urusi.

Yote hayo yanajiri baada ya kudunguliwa kwa droni za Urusi zilizoingia katika anga ya Poland wiki iliyopita ambapo NATO ilituma ndege za ziada za kivita kwenye eneo hilo la Mashariki mwa Ulaya. Hatua hiyo imesababisha majadiliano mapya kuhusu kuongeza ulinzi katika maeneo ya Magharibi mwa Ukraine na ambayo yanapakana na Poland na pia kuzisambaratisha droni za Urusi au makombora yanayolenga maeneo hayo ya mpakani.

Hali baada ya shambulio la ndege isiyo na rubani ya Urusi katika eneo la Sumy
Zima moto akizima moto baada ya shambulizi la droni za Urusi huko Sumy, Ukraine kwenye picha hii iliyochapishwa Septemba 12, 2025.Picha: State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Peskov: Urusi bado ina nia ya mazungumzo na Ukraine

Urusi imesema bado ina nia ya kufanya mazungumzo ya kupata suluhu ya mzozo kati yao na Ukraine, kama ambavyo Dmitry Peskov, msemaji wa Ikulu ya Kremlin anavyosema: “Urusi bado inasimamia nia yake na utayari wa kutatua mgogoro wa Ukraine kwa njia za kisiasa na kidiplomasia. Kyiv inapunguza kasi ya mchakato huo kwa namna fulani. Hakuna anayetaka kuzama ndani ya kiini cha mzozo huo. Umoja wa Ulaya wanaingilia suala hilo, hawaonyeshi nia yoyote ya kuzingatia sababu za mzozo huu.”

Kwa upande mwingine, ripoti ya kila mwaka ya muungano unaofuatilia matumizi ya mabomu yaliyopigwa marufuku Cluster Munition Coalition (CMC), imesema zaidi ya watu 1,200 wameuawa au wamejeruhiwa nchini Ukraine, kutokana na mabomu hayo tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 2022.

Ripoti hiyo inasema kumekuwa na mwenendo wa kurudisha nyuma hatua zilizopigwa katika kuharamisha mabomu hayo ikisema Ukraine imeshuhudia vifo vingi zaidi duniani kote kutokana na mabomu hayo yanayotumiwa pakubwa na Urusi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *