Vyama vya mrengo wa kushoto, Social Democrats (SPD) na Greens, vimeshindwa kulingana na matokeo ya awali.

CDU imepata takribani asilimia 33.3 ya kura zote, huku SPD ikishika nafasi ya pili kwa asilimia 22.5, ikishuka kidogo kutoka asilimia 24.3 miaka mitano iliyopita.

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative für Deutschland (AfD) kimeongeza kura zake karibu mara tatu hadi asilimia 14.5 kutoka asilimia 5.1 mwaka 2020. Greens wameporomoka vibaya, wakishuka kwa asilimia 11.5 baada ya rekodi ya asilimia 20 katika uchaguzi wa ndani uliopita.

Wanasiasa wa CDU na SPD tayari wameapa kutoshirikiana na AfD, wakisisitiza kuendeleza kile wanachokiita “ukuta wa moto” dhidi ya chama hicho cha mrengo mkali wa kulia.

Takribani wakaazi milioni 14 walikuwa na haki ya kupiga kura katika jimbo hilo lenye watu wengi zaidi nchini Ujerumani.

Ujerumani | Uchaguzi wa serikali za mitaa NRW 2025 | kampeni za uchaguzi AFD
Wafuasi wa Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ujerumani cha AfD wakiwa kwenye mkutano wa kampeni za uchaguziPicha: Oliver Mueller/Funke Foto Services/imago images

Uchaguzi huo ulihusisha pia viongozi wa mabaraza ya mitaa mameya na wasimamizi wa wilaya, miongoni mwa nyadhifa nyingine za kuchaguliwa.

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la umma, WDR, waliojitokeza kupiga kura walikuwa 56.5%, ongezeko la karibu 5% ikilinganishwa na uchaguzi wa mitaa wa mwaka 2020.

Ujerumani yaendeleza mazungumzo ya kuwarejesha wahamiaji wa Afghanistan

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Alexander Dobrindt, amethibitisha kuwa mazungumzo yanaendelea na kundi la Taliban ili kuwezesha kuwarejesha raia wa Afghanistan waliopatikana na hatia ya uhalifu nchini Ujerumani.

“Tunataka hili tuweze kulifanya sisi wenyewe. Ndiyo maana tunaendeleza mawasiliano ya kiufundi kati ya wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani na wawakilishi kutoka Afghanistan,” alisema.

“Mawasiliano haya ya kiufundi yanapaswa hatimaye kutuwezesha kuwarudisha kwao Afghanistan mara kwa mara,” Dobrindt aliongeza.

Ujerumani Berlin 2025 | Alexander Dobrindt akiwa kwenye Siku ya Uwazi ya Serikali ya Shirikisho katika Ofisi ya Shirikisho la Vyombo vya Habari
Alexander Dobrindt (CSU), Waziri wa Mambo ya Ndani wa Shirikisho, anashiriki katika majadiliano jukwaani katika siku ya wazi ya Serikali mpya ya Shirikisho katika Ofisi ya Shirikisho la Vyombo vya Habari – 23.08.2025Picha: Fabian Sommer/dpa/picture alliance

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje, Wadephul Johann Wadephul pia amethibitisha kuwa mazungumzo kuhusu kurejeshwa kwa raia hao yalikuwa yakifanyika mjini Doha, akisisitiza kuwa mikutano ya Kabul haina umuhimu.

Mwezi Julai, Ujerumani iliwahamisha kwa ndege Waafghanistan 81 waliokuwa na rekodi za uhalifu.

Kwa nini hatua hii ina utata?

Kundi la Taliban lilichukua madaraka nchini Afghanistan mnamo Agosti 2021 baada ya wanajeshi wa Muungano wa NATO kujiondoa.

Tangu wakati huo, Ujerumani haina uhusiano rasmi wa kidiplomasia na serikali ya Taliban ambayo haijatambuliwa kisheria kimataifa.

Pamoja na kuongezeka kwa misimamo ya mrengo wa kulia nchini Ujerumani, uhamiaji ulikuwa mada kuu katika kampeni za uchaguzi za CSU na CDU kuelekea uchaguzi mkuu wa Februari.

Kansela Friedrich Merz, kwa upande wake, ameapa kuwarudisha makwao raia wa Afghanistan na Syria, na kusimamisha programu za kupokea maombi ya hifadhi kwa wale waliohudumu katika mashirika ya Ujerumani nchini Afghanistan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *