Onyo la Urusi limejiri baada ya ripoti kudokeza kwamba Umoja wa Ulaya unapendekeza kutumia mali ya Urusi ambayo yamezuiwa yenye thamani ya mabilioni ya dola ili kuisaidia Ukraine.

Punde tu baada ya rais wa Urusi Vladimir Putin kupeleka vikosi vyake kuivamia Ukraine mwaka 2022, Marekani na washirika wake walizuia ushirikiano na Benki Kuu ya Urusi na vile vile wizara ya Fedha ya Urusi. Aidha walizuia mali ya Urusi yenye thamani ya kati ya dola bilioni 300 hadi 350. Nyingi ya mali zikiwa ni hati za dhamana za serikali za Ulaya, Marekani na Uingereza zilizohifadhiwa barani Ulaya.

Shirika la habari la Reuters, liliripoti kwamba Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula vonder Leyen, anautaka umoja wake kutafuta njia mpya ya kuisadia Ukraine kwa kutumia mali za Urusi ambazo zimezuiwa Ulaya.

Gazeti la Politico pia liliripoti kuwa Tume ya Ulaya inatafakari wazo la kutumia amana za fedha za Urusi zilizopo katika Benki Kuu ya Ulaya, zinazotokana na hati za dhamana zinazomilikiwa na Urusi, kufadhili ‘mkopo wa fidia’ kwa Ukraine.

Medvedev: Tutawaandama mahakamani na nje ya mahakama

Wazo hilo limekosolewa vikali na Urusi. Rais wa zamani wa Urusi, Dmitry Medvedev, ambaye kwa sasa anahudumu kama naibu mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Urusi, ameandika kwenye ukurasa wake wa Telegram kwamba, ikiwa hilo litatimia, Urusi itaziandama nchi za Umoja wa Ulaya.

“Urusi itayaandama mataifa ya Ulaya kwa njia zote zinazowezekana, katika mahakama yote ya kitaifa au kimataifa na hata nje ya mahakama,” amesema Medvedev.

Kulingana na Urusi, hatua yoyote ya kunyakua mali zake ni sawa na wizi unaofanywa na nchi za Magharibi, na itadhoofisha imani kwa hati za dhamana na sarafu za Marekani na Ulaya.

Nchi za Ulaya zinahoji kuwa Urusi inawajibika kuhusiana na uharibifu unaoshuhudiwa Ukraine, na ambao ndio uharibifu mbaya zaidi kuwahi kufanyika barani Ulaya tangu mwisho wa Vita Vikuu vya Pili vya Ulimwengu. Na kwa hivyo ni lazima Urusi ilazimishwe kulipa.

Hata hivyo, baadhi ya benki zina wasiwasi kwamba kutumia hati za dhamana za Urusi, kunaweza kuathiri imani ya wawekezaji wa kigeni wanaowekeza fedha zao kwenye hati fungani za serikali za Magharibi.

Uingereza yatumia mali ya Urusi yenye thamani ya dola bilioni 1.3?

Mapema mwezi huu, Medvedv alisema Urusi itachukua maeneo zaidi ya Ukraine na italenga mali za Uingereza kote duniani. Kauli yake ilijiri baada ya London kusema imetumia takriban dola bilioni 1.3 zilizopatikana kutokana na mali za Urusi zilizozuiwa ili kununua silaha kwa ajili ya Ukraine.

Unaweza pia kusoma: Zelensky: Putin hana nia ya kusitisha mapigano

Shirika la habari la serikali ya Urusi, RIA, lilisema kuwa nchi za Magharibi zimewekeza jumla ya dola bilioni 285 katika uchumi wa Urusi kupitia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, ambao unaweza kuwa hatarini iwapo mali za Urusi zitachukuliwa.

Ukraine | SHambulizi la droni la Urusi eneo la Kharkiv Ukraine
Afisa wa kuzima moto wa Ukraine akipambana na moto uliozuka baada ya Urusi kushambulia miundo mbinu muhimuPicha: State Emergency Service of Ukraine in Chernihiv region/REUTERS

Katika tukio tofauti, ripoti ya kila mwaka ya muungano unaofuatilia matumizi ya mabomu yaliyopigwa marufuku Cluster Munition Coalition (CMC), imesema zaidi ya watu 1,200 wameuawa au wamejeruhiwa nchini Ukraine, kutokana na mabomu hayo tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 2022.

Ukraine yarekodi maafa makubwa zaidi kutokana na mabomu yaliyoharamishwa

Ripoti hiyo inasema kumekuwa na mwenendo wa kurudisha nyuma hatua zilizopigwa katika kuharamisha mabomu hayo, ikisema Ukraine imeshuhudia vifo vingi zaidi duniani kote kutokana na mabomu hayo yanayotumiwa pakubwa na Urusi.

Mabomu hayo yanaweza kudondoshwa kwa ndege au yanaweza kufyatuliwa kwa mizinga, kabla ya kulipuka angani ya kusababisha milipuko mingi katika eneo kubwa.

Hatari yao ni kubwa kwa sababu mengi ya mabomu hayo huweza kukosa kulipuka moja kwa moja. Badala yake huja kulipuka baadaye au hata baada ya miaka kdhaa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, takribani watu 193 waliuawa 2024 nchini Ukraine, idadi hiyo ikiwa ni jumla ya watu 314 waliouawa kote ulimwenguni kutokana na mabomu hayo hatari.

Kwa jumla zaidi ya watu 1,200 wameuawa Ukraine tangu uvamizi wa Urusi ulipoanza.

(RTRE, AFPE)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *