Mienendo ya kamatakamata ya wafuasi wa vyama vya upinzani na hasa kuelekea kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu, ni miongoni mwa vielelezo vya kudorora kwa demokrasia nchini Uganda.
Wadadisi wa kisiasa na viongozi wa kisiasa wanakosoa kuanzia taasisi za kijeshi, sheria na bunge kwa kuhusika katika vitendo hivyo vinavyokiuka si tu haki za binadamu lakini dhana na falsafa ya demokrasia.
Katika kipindi cha wiki tatu hivi viongozi na wafuasi kadhaa wa upinzani walikamatwa kwa kiviziwa na askari waliovalia kiraia ambao waliwaburuta na kuwasukumia kwenye magari ya kiraia na kuwapeleka mahali pasipokujulikana.
Jeshi la Polisi lakana kamatakamata ya kiholela
Msemaji wa idara ya mawasiliano ya jeshi, Brigedia Jenerali Felix Kulayigye amesema watu hao hawakutekwa nyara kama inavyodaiwa, ila walikamatwa kisheria wakihusishwa na tuhuma mbalimbali na hufikishwa mahakamani.
Amefahamisha kuwa wafuasi na viongozi wa chama cha upinzani cha NUP wamekamatwa hivi karibuni baada ya kuandaa gwaride la kijeshi kuadhimisha siku ya kuzaliwa rais wa chama hicho Robert Kyagulanyi al maarufu Bobi Wine.
Wadadisi wanasema ingawa uchaguzi huchukuliwa kuwa msingi wa demokrasia, hali ni tofauti kabisa pale vyama vya upinzani vinapozuiwa kuendesha shughuli zake pamoja viongozi wao kukamatwa na kuendelea kuzuiliwa huku kesi dhidi zao zikiendeshwa kwa hali ya kuwavunja moyo.
Kiongozi wa chama cha upinzani PFF, Dkt Kizza Besigye amendelea kubaki gerezani licha ya kuwa na haki ya dhamana. Kwa mtazamo wao, hakuna haja ya uchaguzi kufanyika kama demokrasia halisi hata ndani ya vyama vyenyewe haina uhalisia.
Huku siku hii ya kimataifa ya demokrasia ikiadhimishwa tarehe 15 Septemba, tarehe 12 ni siku ambayo wanasiasa Uganda wameiweka kuwa kumbukumbu ya siku ambapo bunge la Uganda liliondoa ukomo wa umri kwa mgombea urais kwemye katiba na hivyo kumwezesha Rais Yoweri Museveni kuendelea kugombea na kutawala.
