
Tume huru ya kimataifa ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa imeishutumu Israel leo Jumanne, Septemba 16, kwa kufanya “mauaji ya halaiki” katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa vita mnamo Oktoba 7, 2023, kwa “nia ya kuwaangamiza” Wapalestina.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Tumehitimisha kuwa mauaji ya halaiki yanatokea Gaza na yanaendelea kutokea, na jukumu hilo ni la Taifa la Israeli,” mwenyekiti wa tume hiyo ametangaza. Israel imeshutumu uchunguzi huo kama “upendeleo na usiofaa.”
Tume hiyo, ambayo haizungumzi kwa niaba ya Umoja wa Mataifa na inakosolewa vikali na Israel, “imehitimisha kuwa mauaji ya halaiki yanatokea Gaza na yanaendelea kutokea” katika eneo la Palestina, mwenyekiti wake, Navi Pillay, ameliambia shirika la habari la AFP.
“Israel inahusika na mauaji hayo,” ameongeza, akiwasilisha ripoti mpya. Kuchapishwa kwake kunakuja karibu miaka miwili baada ya kuanza kwa vita, vilivyochochewa na shambulio lisilokuwa la kawaida la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023. Tangu wakati huo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuangamiza vuguvugu hilo la Kiislamu lililonyakua mamlaka huko Gaza mnamo mwaka 2007.
“Vitendo vinne kati ya vitano vya mauaji ya kimbari”
Tume ya uchunguzi imehitimisha kuwa mamlaka ya Israel na vikosi vya usalama vilifanya “vitendo vinne kati ya vitano vya mauaji ya halaiki” vilivyofafanuliwa na Mkataba wa mwaka 1948 wa Kuzuia na Kuhabu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari. Haya yalikuwa: “kuwaua washiriki wa kundi; kusababisha madhara makubwa ya mwili au kiakili kwa washiriki wa kundi; kuathiri kimakusudi hali za maisha za kundi zinazohesabiwa kuleta uharibifu wake wa kimwili kwa ujumla au sehemu; na hatua zinazokusudiwa kuzuia kuzaliwa ndani ya kundi.”
Tume hiyo imehitimisha kuwa Rais wa Israel Isaac Herzog, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, na Waziri wa zamani wa Ulinzi Yoav Gallant “walichochea mauaji ya halaiki na kwamba mamlaka za Israel zilishindwa kuchukua hatua” kuzuia. “Ni wazi kwamba kuna nia ya kuwaangamiza Wapalestina huko Gaza kupitia vitendo vinavyokidhi vigezo vilivyowekwa katika Mkataba wa Mauaji ya Kimbari,” Pillay, ambaye aliwahi kuwa rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Rwanda na jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), amesema katika taarifa yake.
Israel inalaani uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kama “upendeleo na usiofaa.”
Viongozi wa ngazi za juu zaidi wa Israel “waliandaa kampeni ya mauaji ya halaiki,” ameongeza Mwafrika Kusini mwenye umri wa miaka 83, Kamishna Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu. Tume hii si chombo cha kisheria, lakini ripoti zake zinaweza kuongeza shinikizo la kidiplomasia na kutumika kukusanya ushahidi kwa mahakama kutumia. Tume imeingia katika makubaliano ya ushirikiano na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ambayo “tumeshiriki maelfu ya habari,” Pillay ameliambia shirika la habari la AFP.
“Jumuiya ya kimataifa haiwezi kukaa kimya mbele ya kampeni ya Israel ya mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza. Wakati dalili za wazi na ushahidi wa mauaji ya kimbari zinapojitokeza, kushindwa kuchukua hatua kukomesha ni sawa na kushiriki,” Pillay amesema. Kwa upande wake, Israel “imefutilia mbali kabisa” ripoti ya tume ya kimataifa ya uchunguzi siku ya Jumanne. “Israel inapinga kabisa ripoti hii ya upendeleo na ya uwongo na inataka kufutwa mara moja kwa tume hii ya uchunguzi,” Wizara ya Mambo ya Njeya Israel imesema katika taarifa.