Mtandao wa habari wa Axios umeripoti taarifa hizo ukiwanukuu maafisa kadhaa wa Israeli. Serikali mjini Tel Aviv ilitangaza mpango wa kuukamata mji wa Gaza zaidi ya mwezi mmoja uliopita.
Kwa siku kadhaa sasa jeshi la Israel limekuwa likiushambulia mji huo na kuyaporomosha majengo chungunzima ikiwemo ya ghorofa ikitumia makombora kutokea angani.
Kampeni hiyo ya kijeshi inafanyika licha ya ukosoaji mkubwa wa jumuiya ya kimataifa inayohofia kuushambulia mji wa Gaza kutazidisha madhila yanayowakabili sasa Wapalestina.
Mashirika kadhaa ya kimataifa yamekwishaonya kuwa hali ya kiutu kwenye ardhi hiyo ndogo ya Wapalestina tayari imefikia viwango vya kutisha na operesheni yoyote ya kijeshi itasababisha vifo na maafa zaidi kwa wakaazi wa mji wa Gaza na ukanda mzima.
Mnamo juma lililopita Israel iliongeza shinikizo la kuwataka watu kuondoka Gaza City ikiapa kwamba ni lazima ifanye operesheni kubwa ya kijeshi kuukamata mji huo kwa lengo inalosema kuwa ni kulitokomeza kundi la Hamas.
Marekani ´yapalilia´ mipango ya Israel ndani ya Gaza City
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Marco Rubio ambaye alikuwa ziarani nchini Israel tangu siku ya Jumapili aliunga mkono operesheni hiyo ya jeshi la Israel na dhamira yake ya kulitokomeza kundi la Hamas.
Rubio aliyekwenda Israel siku chache tangu taifa hilo lilipofanya mashambulizi ya anga nchini Qatar na kuzusha hasira na lawama ya kimataifa, ameonesha kutilia mashaka kuhusu nafasi ya diplomasia katika kuvimaliza vita vya Gaza vilivyozuka karibu miaka miwili iliyopita.
Amekaririwa akisema eneo la Gaza linahitaji mwanzo mpya lakini hilo “halitowezekana” hadi pale kundi la Hamas litakaposambaratishwa.
Inaarifiwa mwanadiplomasia huyo ataelekea Qatar leo Jumanne kuonesha kile ofisi yake imekitaja kuwa “kudhihirisha uungaji mkono wa Marekani” kwa “uhuru na umuhimu wa kuheshimiwa hadhi ya mipaka” ya nchi hiyo ya Ghuba.
Hata hivyo jambo hakulisema alipokutana ana kwa ana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem.
Uamuzi wa Israel wa Jumanne iliyopita wa kushambulia kikao cha viongozi wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas kilichokuwa kinafanyika Doha, Qatar umefifisha matumaini ya juhudi zote za upatanishi wa mzozo wa Gaza.
Tukio hilo ambalo Rais Donald Trump wa Marekani amesema “halikumfurahisha” limechochea ukosoaji kutoka mataifa ya kiarabu na yale ya kiislamu na hata nchi za magharibi.
Viongozi wa nchi za kiarabu na kiislamu waikosoa Israel
Kwenye mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za kiarabu na kiislamu uliofanyika jana Jumatatu mjini Doha kulaani kushambuliwa kwa Qatar, kiongozi wa nchi hiyo Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani aliituhumu Israel kwa kutowajali mateka wake wanaoshikiliwa kwenye Ukanda wa Gaza.
Ameituhumu serikali ya Israel kuwa imedhamiria na inaelekeza nguvu zake kuhakikisha “eneo hilo la Wapalestina haliwi tena mahala salama pa kuishi.”
Marekani ambayo ni mshirika wa karibu wa Israel na vilevile Qatar inajaribu kutuliza hali ya msuguano inayoshuhudiwa tangu Israel iliposhambulia ndani ya ardhi ya Qatar.
Rais Trump alirejea matamshi yake hapo jana akisema “Qatar haitoshambuliwa tena” na Israel.
Ahadi yumkini haitotuliza wasiwasi na hamkani mjini Doha hasa ikizingatiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, alianza kwanza safari nchini Israel ambako hakuinyooshea kidole cha lawama nchi hiyo na wala kuonesha hisia kuwa Washington ilikasirishwa na kitendo kilichofanywa na serikali ya Netanyahu.