Hayati Maalim Seif

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Na Rehema Mema
    • Nafasi,

Kwa zaidi ya robo karne, jina la Maalim Seif Sharif Hamad lilihusiana moja kwa moja na siasa za upinzani Zanzibar. Kwa wafuasi wake, alikuwa alama ya matumaini; kwa wapinzani wake, alikuwa mpinzani sugu, asiyechoka, ambaye mara zote aliamini kuna nafasi ya mabadiliko.

Kila uchaguzi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, jina la Maalim Seif lilikuwa katikati ya majukwaa, kura na mijadala ya kisiasa.

Kifo chake mwaka 2021 kimeacha pengo kubwa ambalo uchaguzi wa 2025 unakabiliana nalo kwa mara ya kwanza. Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1995, Zanzibar inakwenda kwenye uchaguzi mkuu bila kivuli chake kizito. Swali kuu liko wazi: bila Maalim Seif, upinzani una sura gani, na CCM inakutana na changamoto ipi?

Urithi wa Maalim Seif

Maalim Seif alianza siasa zake ndani ya CCM (wakati huo ASP na baadaye CCM) kabla ya kugombana na chama hicho mwishoni mwa miaka ya 1980. Hapo ndipo alipoanza safari yake ya upinzani kupitia Chama cha Wananchi (CUF), akakijenga kuwa chama kikuu cha siasa visiwani. Baadaye, alihamia ACT-Wazalendo baada ya migogoro ya ndani ya chama chake cha zamani. Katika kila hatua, aliibeba Zanzibar kwenye majukwaa ya siasa za upinzani kitaifa na kimataifa.

Urithi wake mkubwa kwa wafuasi wake ulikuwa sio tu siasa za kawaida, bali imani kwamba upinzani ni chaguo halali, chenye heshima na nguvu. Maalim Seif aliweka msingi wa kukubalika kwa upinzani, akiwashawishi maelfu kwamba kura zao zinaweza kuwa na maana hata pale matokeo yalipokuwa yakibishaniwa.

Zaidi ya hayo, alijenga mtindo wa upinzani wenye karisma. Aliweza kuzungumza lugha ya wananchi wa kawaida, kushirikiana nao mitaani na vijijini, na kuwapa hisia kwamba alikuwa mmoja wao. Haikuwa ajabu kila alipogombea, Zanzibar iligeuka kitovu cha mijadala, maandamano na wakati mwingine migogoro ya kisiasa.

Kwa miongo yote hiyo, jina la Maalim Seif liliifanya Zanzibar kutazamwa si tu kama kisiwa cha siasa za kawaida, bali uwanja wa mapambano ya haki za kidemokrasia barani Afrika. Kwa maana hiyo, kuondoka kwake kumeacha pengo la kipekee ambalo halijazibwa hadi sasa.

Pengo la Maalim Seif

Maalim Seif

Chanzo cha picha, Getty Images

Kifo cha Maalim Seif kuliwasha mjadala mkubwa: nani anayeweza kurithi nafasi yake? Kwa sababu alikuwa zaidi ya kiongozi wa chama, alikuwa ni taasisi ya kisiasa. Kwa wafuasi wake, alikuwa alama ya mshikamano na mapambano; kwa wapinzani wake, alikuwa ni changamoto ya kudumu.

ACT-Wazalendo, chama chake cha mwisho, kilimkabidhi kijiti Othman Masoud, mwanasheria msomi na mwanasiasa mwenye uzoefu serikalini. Tofauti na Maalim Seif, Masoud ni kiongozi anayejulikana kwa utulivu, hoja na maelezo ya kisheria badala ya karisma ya umati. Hii inampa nguvu kubwa katika mijadala rasmi, lakini haimpe nguvu ile ile ya kufuruga nyoyo za maelfu katika mikutano ya hadhara.

Kwa wapiga kura wengi mashinani, hasa wale waliomzoea Maalim Seif kwa karne nzima ya siasa za vyama vingi, pengo hili ni halisi. Karisma ya Maalim Seif ilikuwa kama kivutio cha kihisia, kitu ambacho hakihitaji hoja ndefu kuwasilisha. Masoud, pamoja na heshima na ujuzi wake, bado hajajengea umati ule ule hisia kwamba yeye ndiye mwokozi wa matumaini yao.

Hata hivyo, Masoud ana faida moja kubwa: anakuja na taswira mpya isiyo na migogoro mikubwa ya kihistoria. Kwa tabaka la kati na wasomi, anaonekana kama mwanasiasa wa mageuzi mwenye hoja safi, asiyebeba mizigo ya malumbano ya zamani. Kwa hivyo, pengo la karisma linaweza kuzibwa taratibu kwa hoja na uhalisia wa mageuzi anayoyaahidi. Swali linaendelea kubaki: je, hiyo inatosha kuziba kivuli kikubwa alichoacha Maalim Seif?

CCM bila haiba ya upinzani wa aina ya Maalim Seif

Kwa upande wa chama tawala, Rais Hussein Mwinyi anaingia kwenye uchaguzi akitafuta muhula wa pili. Kipindi cha Maalim Seif, CCM mara zote ilikuwa ikijiandaa kwa pambano lenye mvutano mkali, likitawaliwa na malalamiko, maandamano na shinikizo za upinzani. Katika chaguzi nyingi, matokeo yaliishia kusababisha mvutano wa kisiasa uliohitaji mazungumzo ya kitaifa au muafaka wa kisiasa.

Safari hii hali ni tofauti. Upinzani hauna sura ile ile ya kishindo. Hakuna kiongozi mwenye karisma kubwa anayelazimisha CCM kujiandaa kwa presha ya kihisia. Mwinyi anakutana na upinzani wa hoja zaidi kuliko kelele, jambo linalompa nafasi ya kuwasilisha matokeo ya utawala wake wa miaka mitano iliyopita. Hii ni pamoja na juhudi zake katika kuimarisha ajira, kukuza utalii na kuboresha huduma za kijamii.

Lakini changamoto kwa Mwinyi haiko tu katika kushinda upinzani wa sasa, bali katika kuwashawishi wapiga kura kwamba matokeo ya utawala wake ni ya kudumu na yameleta mabadiliko ya kweli. Upinzani unaweza kuwa hauna nguvu za kishindo, lakini unaweza kutumia hoja ndogo ndogo kumchambua Mwinyi pale ambako matokeo hayajaonekana dhahiri.

Kwa upande wa ACT-Wazalendo, changamoto ni kujijenga upya bila kivuli cha Maalim Seif. Othman Masoud anakabiliana na mzigo wa kuwa mrithi wa mapambano bila nguvu ya karisma ya mtangulizi wake. Ana faida ya uelewa na usomi, lakini anatakiwa kuwashawishi wapiga kura kwamba chama chake bado kinaweza kutoa mbadala wa kweli.

Kwa maana hiyo, uchaguzi wa Zanzibar 2025 unakuwa wa kipekee. Bila MaalimSeif, hakuna sura ya mvutano wa karisma uliokuwa kawaida. CCM sasa inakabiliana na upinzani wa aina mpya, upinzani wa hoja na sera zaidi kuliko makelele ya kishindo cha kisiasa.

Ukienda maeneo mengi ambapo siasa zinazungumzwa sana hasa za upinzani, maeneo kama Joz kona, Daraja bovu na Mtendeni swali utakalolisikia zaidi linajadiliwa ni je, Zanzibar itaingia kwenye zama za utulivu zaidi wa kisiasa, au pengo la karisma litaleta changamoto mpya kuhusu nguvu na mustakabali wa vyama vya upinzani visiwani? Majibu yatapatikana Oktoba 29, 2025.

.
.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *