
Chanzo cha picha, Reuters
-
- Author, Sandeep Rai
- Nafasi, BBC
Kufuatia mashambulizi ya Israel katika mji mkuu wa Qatar, Doha kuwalenga viongozi wa Hamas, juhudi za kuunda muungano wa kijeshi unaofanana na NATO miongoni mwa nchi za Kiarabu zinaonekana kushika kasi.
Mkutano wa dharura wa nchi za Kiarabu na Kiislamu umeandaliwa mjini Doha, ambapo mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama hao walikutana hapo jana.
Leo, viongozi wakuu wa nchi nyingine pia watahudhuria mkutano huu, akiwemo Rais wa Irani Masoud Pezeshkian, Waziri Mkuu wa Iraq Muhammad Shia al-Sudanese na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.
Kwa mujibu wa gazeti la The National, Misri imependekeza kuundwa kwa kikosi cha kijeshi kinachofanana na NATO, ambacho kiti chake cha urais kitatolewa kwa zamu kati ya nchi 22 za Umoja wa Kiarabu, Misri ikiwa rais wake wa kwanza.
Kulingana na The New Arab Media, pendekezo kama hilo lilikuja kwa mara ya kwanza 2015, wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen baada ya waasi wa Houthi kuuteka mji wa Sanaa.
Kwa upande mwingine, baada ya mashambulizi ya Doha, hali ya wasiwasi imeongezeka nchini Uturuki pia.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Uturuki Rear Admiral Zeki Akturk alionya kwamba “Israel inaweza kuzidisha mashambulizi yake ya kiholela, kama ilivyofanya huko Qatar.”
Pendekezo la Misri ni lipi?

Chanzo cha picha, Reuters
Pendekezo la Misri ni pamoja na kuanzisha uhusiano bora kati ya majeshi, jeshi la anga na vitengo vya komando, pamoja na kuunganisha mifumo ya mafunzo, vifaa na jeshi.
Pia, ruhusa ya kutumia nguvu za kijeshi itatolewa kwa msingi wa mashauriano na nchi wanachama na uongozi wa kijeshi.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Lebanon Al Akhbar, Misri imesema katika pendekezo hilo, itachangia wanajeshi 20,000 katika muungano huo wa kijeshi, huku Saudi Arabia ikiwa ni nchi ya pili kwa ukubwa katika ushirikiano huo.
Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amezungumza na nchi kadhaa kuhusiana na hili na uwezekano wa kujadili pendekezo hili mbali na mkutano wa Doha.
Muungano wa kijeshi kama huo kati ya nchi za Kiarabu na Kiislam uliwahi kuwepo hapo awali, ulijuulikana kama Mkataba wa Baghdad, ulikuwepo kuanzia 1955 hadi 1979.
Shambulio la Israel huko Doha liliibua hisia kali kutoka nchi za Kiarabu, na UAE, nchi pekee katika eneo hilo ambayo ina uhusiano wa kidiplomasia na Israel, pia ilikosoa.
Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia al-Sudani pia ametoa wito wa kuundwa kwa ‘muungano wa kijeshi wa Kiislamu.’
Kulingana na shirika la utangazaji la Uturuki TRT World, Wazri huyo amesema jibu la pamoja kwa hatua za hivi majuzi za Israel huko Gaza na Qatar ni muhimu.
Al-Sudani amesema shambulio la anga la Jumanne dhidi ya Doha, ambalo liliua wanachama watano wa Hamas na afisa wa usalama wa Qatar, ni “ukiukwaji wa sheria za kimataifa” na kusema matendo ya Israel yanatishia usalama wa eneo zima.
“Hakuna sababu kwa nini nchi za Kiislamu haziwezi kuja pamoja kuunda kikosi cha pamoja cha usalama ambacho kinaweza kujilinda,” aliiambia chanali ya Al Jazeera ya Qatar, akitoa wito kwa nchi za Kiarabu na Kiislamu kuunda ushirikiano katika ngazi za kisiasa, usalama na kiuchumi.
Israel inapaswa kuadhibiwa

Chanzo cha picha, Reuters
“Ni wakati wa jumuiya ya kimataifa kukomesha undumilakuwili na kuiadhibu Israel kwa uhalifu wake wote,” waziri mkuu wa Qatar alisema kabla ya mkutano huo wa Jumatatu, kulingana na idhaa ya BBC ya Kiajemi.
“Israel lazima ijue kwamba vita vyake vibaya dhidi ya ndugu zetu, Wapalestina, vinavyolenga kuwafukuza katika ardhi yao, havitafanikiwa,” alisema.
Qatar imetoa kauli kali kwa shambulio la Israel huko Doha Septemba 9 na imesisitiza kwamba sasa iko macho na iko tayari kwa hali yoyote.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imesema rasimu ya azimio kuhusu shambulio la Doha itajadiliwa katika mkutano huo.
Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas Bassem Naim alisema kundi hilo linatumai mkutano huo utaleta “msimamo imara na wa pamoja wa nchi za Kiarabu na Kiislamu” na hatua “ya wazi na mahususi” kuhusu Israel.
Qatar ina hifadhi kambi kubwa zaidi ya jeshi la Marekani katika eneo hilo na ina jukumu muhimu katika upatanishi kati ya Marekani na Misri, na pia kati ya Israel na Hamas.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Marco Rubio, ambaye kwa sasa anazuru Israel, alionyesha kukerwa na shambulio la Doha lakini pia akakariri kuwa halitadhuru uhusiano wa Marekani na Israel.
Taarifa ya msemaji wa Ikulu ya Marekani Caroline Levitt kuhusiana na shambulio hilo ilizua utata. Kulingana na White House, Qatar “iliarifiwa kabla ya shambulio hilo,” lakini Waziri Mkuu wa Qatar alisema alipokea taarifa “dakika 10 baada ya shambulio hilo.”
‘NATO ya Waarabu’ inawezekana?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wazo la kuunda muungano wa kijeshi kama NATO kati ya nchi za Kiarabu limekuwepo kwa muda mrefu, lakini wataalam hawana hakika juu ya utekelezwaji wake.
Premananda Mishra, mwanachama wa Kituo cha Nelson Mandela cha Amani na Usuluhishi wa Migogoro katika Chuo Kikuu cha Jamia Millia Islamia, anasema, “Wazo la NATO ya Waarabu lilijadiliwa hapo awali na Saudi Arabia ililitilia mkazo sana. Hata Mkuu wa zamani wa Jeshi la Pakistani Raheel Sharif aliteuliwa kuwa mwenyekiti wake. Lakini suala hilo halikuweza kuendelea.”
Anasema, “maslahi ya usalama ya nchi zote ni tofauti kiasi kwamba kujenga maelewano kati yao ni kazi ngumu. Kwa mfano, Saudi Arabia na Iran zitaweza kuondokana na tofauti zao na kuja pamoja? Kwa sababu ikiwa muungano wa kijeshi wa pamoja utaundwa, basi ushirikiano wa kijasusi pia utalazimika kufanywa.”
Ingawa kumekuwa na majaribio ya kurejesha uhusiano kati ya Saudi Arabia na Iran katika siku za hivi karibuni, bado uhusiano huo haujawa imara.
Premanand Mishra anasema, “pendekezo hili limetoka Misri. Hatujui ikiwa litatekelezwa. Na kama nchi za Magharibi, hasa Marekani na NATO, zitaruhusu muungano huo wa kijeshi kuundwa.”
Anasema kuna mashaka mengi iwapo litatekelezwa wazo hilo litatekelezwa.
Dk Mudassir Qamar, Profesa Msaidizi katika Kitivo cha Masomo ya Asia Magharibi katika Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru chenye makao yake mjini Delhi, anaamini nchi za Kiarabu zina mashirika mengi ya kimataifa, iwe Jumuiya ya Kiarabu, OIC au GCC.
Kando na hayo, lipo shirika la kijeshi la kupambana na ugaidi chini ya uongozi wa Saudi Arabia lakini tatizo hasa ni kukabiliana na tofauti zilizopo miongoni mwa nchi za Kiarabu.
Mudassir Qamar anasema, “itakuwa vigumu kwa muungano wowote wa aina hiyo kutoshughulika na Israel, ambayo kwa sasa iko katika hali ya mvutano na nchi nyingi za Kiarabu.”