
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito kwa viongozi wa dunia “kuwa makini na kutekeleza ahadi” wanapowasili jijini New York kwa ajili ya wiki ya ngazi ya juu ya Mkutano wa Baraza Kuu wa 80 wa Umoja wa Mataifa UNGA80.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja huo, Guterres ameonya kuwa migawanyiko, migogoro na misukosuko ya kimataifa imepelekea mshikamano wa kimataifa kuwa dhaifu zaidi kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa.
“Wengine huiita kombe la dunia la diplomasia,” amesema Katibu Mkuu wa UN na kusisitiza kwa kusema: “lakini hii si kuhusu kushindana kwa maneno, ni kuhusu kutafuta suluhu. Mambo yaliyoko mezani ni makubwa mno.”
Kwa mujibu wa Guterres, dunia ni kama “imetumbukia kwenye maji yenye dhoruba, isiyojulikana,” akitaja migawanyiko ya kijiografia ya kisiasa, mizozo inayoongezeka, mabadiliko ya tabianchi, maendeleo holela ya teknolojia na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa kama changamoto zinazohitaji hatua za haraka.
Wakuu wa nchi na serikali wapatao 150 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa mwaka huu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakiwa pamoja na maelfu ya maafisa na wanadiplomasia.
Katibu Mkuu wa UN amesema atafanya zaidi ya mikutano ya pande mbili 150, akiwahimiza viongozi “kupunguza migawanyiko, kupunguza hatari na kupata suluhisho.”
Katika mkutano wake huo na waandishi wa habari, Guterres amerudia wito wake wa kusitishwa vita Ghaza, Ukraine, Sudan na maeneo mengine, na kusisitizia haja ya suluhu ya mataifa mawili Mashariki ya Kati.
Mada kuu za kujadiliwa katika wiki ya ngazi ya juu za viongozi wa nchi wanachama wa UN zitakuwa ni amani, mabadiliko ya tabianchi, ubunifu wenye uwajibikaji, usawa wa kijinsia, ufadhili wa maendeleo na mageuzi ya Umoja wa Mataifa…/