Nigeria imesimama na mataifa yanayodhulumiwa katika miongo kadhaa iliyopita, hasa katika mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi nchini Afrika Kusini, na imetetea misingi ya haki na kupinga ukoloni.

Majaribio ya kuukaribia utawala wa Kizayuni unaoshutumiwa kwa mauaji ya halaiki huko Gaza na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, yanakinzana waziwazi na urithi huo wa kihistoria.

Tarehe 11 na 12 Agosti, serikali ya Nigeria ilikaribisha ujumbe wa Israel mjini Abuja, ukiongozwa na Sharon Haskell, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, na Michael Freeman, balozi wa Israel nchini Nigeria. Ziara hiyo imekuja wakati Israel ikikabiliwa na wimbi la ukosoaji wa kimataifa kwa mashambulizi yake ya kinyama na ya kikatili dhidi ya Gaza.

Mkutano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Bianca Odomegwu-Ojukwu na ujumbe wa Israel ulikabiliwa na hisia kali za ndani na kimataifa.

Siku kumi baada ya mkutano huo, Wapalestina wanne wanaoishi nchini Nigeria waliokuwa wamekusanyika kupinga vitendo vya utawala wa Israel walitiwa mbaroni bila ya kufunguliwa mashtaka. Kukamatwa huku, kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binadamu, ni ukiukaji wa wazi wa haki za kimsingi na kanuni za kikatiba nchini Nigeria.

Jeshi la Israel likiungwa mkono moja kwa moja na Marekani na nchi za Magharibi, linaendelea kufanya mauaji ya halaiki huko Gaza, kwa kutumia njaa kama silaha ya vita, na kusababisha vifo vya mamia ya watoto wa Kipalestina; uhalifu uliopangwa ambao umeelezwa kuwa haujawahi kutokea katika historia ya ya leo.

Bendera za Nigeria na utawala wa Kizayuni wa Israel

Wakati ambapo serikali nyingi duniani zinapitia upya uhusiano wao na utawala ghasibu wa Israel, Nigeria, kwa kuukaribisha ujumbe wa Israel na kuwakandamiza waandamanaji wa Kipalestina, imechukua njia ambayo huenda ikaharibu sifa yake kimataifa.

Uwepo wa ujumbe wa kisiasa wa utawala wa Kizayuni nchini Nigeria ulikabiliwa na wimbi la maandamano ya wananchi na mjibizo mkali wa wanaharakati wa kijamii na kidini, na misimamo hiyo inatokana na mambo kadhaa ya kisiasa, kihistoria na kibinadamu.

Nigeria, haswa Waislamu wake, daima wamesimama na mataifa yanayokandamizwa. Historia yake ya kuunga mkono mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini ni sehemu ya utambulisho wake wa kisiasa. Watu wengi nchini humo waliliona jaribio la serikali ya Nigeria la kutaka kujikurubisha kwa utawala wa Kizayuni kuwa ni usaliti wa turathi hizo.

Ziara ya wajumbe wa Israel ilienda sambamba na ripoti nyingi za kuenea kwa mashambulizi dhidi ya raia, njaa ya makusudi, na kulengwa kwa waandishi wa habari huko Gaza. Wanaharakati wa Nigeria wameelezea vitendo hivi kama “mauaji ya halaiki” na “kampeni ya njaa” na wametaka kuchukuliwa hatua za haraka za jamii ya kimataifa.

Katika Jimbo la Kano, Nigeria, maandamano makubwa yalifanyika, ambapo watu walitaka kufukuzwa mara moja balozi wa Israeli kutoka Abuja. Wanawake wa Nigeria pia walionyesha mshikamano wao na Gaza kwa alama za watoto waliouawa shahidi wa Kipalestina.

Maandamano dhidi ya Israel nchini Nigeria

Maandamano hayo yanaonyesha mgawanyiko mkubwa kati ya sera rasmi ya serikali ya Nigeria na hisia za watu wengi, na wachambuzi wengi wanaamini kwamba kuendelea kwenye njia hii kunaweza kudhoofisha uaminifu wa maadili na kidiplomasia wa Nigeria kimataifa.

Kama moja ya nchi muhimu zaidi barani Afrika, Nigeria ina jukumu muhimu katika kuunda nafasi za nchi zingine barani humo. Kujikurubisha na utawala wa Kizayuni, wakati nchi nyingi za Kiafrika zinaiunga mkono Palestina, kunaweza kusababisha Nigeria kutengwa kidiplomasia kikanda. Sera hii inaweza kuathiri uhusiano wa Nigeria na nchi za Kiislamu katika bara la Afrika.

Sera hii yenye utata ya serikali ya Nigeria sio tu inapingana na kanuni za kihistoria na maadili za nchi, lakini pia inaweza kuwa na madhara makubwa kwa umoja wake wa ndani, msimamo wa kikanda, na uaminifu wa kimataifa. Nchi mbalimbali za Kiafrika na watu wa bara hili daima wamekuwa waungaji mkono wakubwa wa matakwa halali ya watu wa Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *