A head shot of Evans Kibet wearing a pink shirt and looking at the camera.

Chanzo cha picha, Edith Chesoi

    • Author, Akisa Wandera
    • Nafasi, BBC Africa
    • Author, Vitalii Chervonenko
    • Nafasi, BBC Ukrainian

Mwanariadha wa Kenya ambaye anashikiliwa nchini Ukraine anaomba asirejeshwe Urusi, huku machozi yakimlenga.

“Nitakufia huko,” Evans Kibet anasema, akipunga mikono hewani kuelekea kwa mtu anayemhoji ambaye haonekani kwenye video iliyotolewa Jumatano na kikosi cha jeshi la Ukraine.

Mfungwa huyo wa vita mwenye umri wa miaka 36- amevalia fulana nyekundu ya michezo, nyuma yake kuna bendera ya jeshi.

Kibet anasema alilaghaiwa kujiunga na jeshi la Urusi na anatamani sana kurejea nyumbani kumuona binti yake wa miaka 16.

Katika chapisho la Facebook lililoambatana na video hiyo, Kikosi cha 57 cha cha jeshi la Ukraine kilisema huoni mfano wa jinsi Urusi inavyowafanyia wanajeshi wa kigeni lakini wakaongeza kuwa “alipigana upande wa adui, kwa hivyo ni uamuzi wako ikiwa utaamini maneno na machozi yake”.

Kikosi hicho kilisema mahojiano hayo yalirekodiwa kwa idhini ya Kibet, lakini BBC haijathibitisha hili. Ingawa walioajiriwa kutoka nje ya nchi katika jeshi la Urusi hawajasikika, hiki ni kisa cha nadra kwa mfungwa raia wa kigeni kuzungumza hadharani na kuonekana kwenye video.

Raia wa Somalia, Sierra Leone, Togo, Cuba na Sri Lanka, miongoni mwa wengine, kwa sasa wanazuiliwa katika kambi za wafungwa wa vita nchini Ukraine, Petro Yatsenko, msemaji wa Ukraine, aliiambia BBC.

“Wengi wa watu hawa wanatoka katika nchi maskini na wanaishia kupigania Urusi kwa njia tofauti. Wengine wanadanganywa – kuahidiwa kazi katika viwanda – wakati wengine wanajiunga na vita kwa hiari. Ni muhimu kuelewa kwamba ni wachache sana wanaokamatwa wakiwa hai; wengi wao huuawa au kujeruhiwa vibaya,” aliongeza.

Nchini Kenya, familia na marafiki wa Kibet wamegutushwa na kile walichokiona.

Baada ya kuvuta pumzi kwa muda ili kupata na utulivu kwa muda, binamu yake Edith Chesoi aliambia BBC kwamba amekuwa akiwaza alichokiona kwenye video hiyo mara kwa mara kichwani mwake.

“Nimeumia sana. Sikulala usiku. Sijui hata niseme nini.”

Kaka yake Kibet mdogo, Isaac Kipyego, alimtaja kama “mtu mnyenyekevu na mwanamume mwenye maneno machache” na vile vile nguzo na mshauri wa familia nzima.

Wanamjua kama mtu aliyejitolea kufanikisha doto yake ya kuwa mwanariadha.

Evans running

Chanzo cha picha, Edith Chesoi

“Napenda kukimbia,” Kibet anasema katika video hiyo ya Waukraine. Na hili ndilo huenda lililomfanya akaishia kusajiliwa kuwa mpiganaji wa Urusi

Kibet alikuwa ameelekeza maisha yake yote kwenye riadha, mchezo ambao umewanyanyua Wakenya wengi kama yeye kutoka vijijini na kuwafanya kutambuliwa kimataifa.

Amekulia eneo la mashambani la Mlima Elgon magharibi mwa Kenya.

Kibet alifanya mazoezi mjini Iten, ambako kunasifika kwa kuwakuza wanariadha mashuhuri duniani, lakini kutokana na ushindani mkali hakufikia kiwango hicho. Badala yake, alishiriki mashindano ya mbio za 10km na mbio za marathon(nus) huko Uropa na Asia, kulingana na jamaa na marafiki.

“Kibet amekuwa akikimbia tangu akiwa mtoto mdogo,”ndugu yake mdogo alisema. “Ana hicho kipaji. Kukimbia ni sehemu ya maisha yake.”

Ingawa mchezo huo umekuwa sehemu ya utambulisho wake, haujamletea mafanikio ya kifedha ambayo alitamani.

Marafiki wanasema kuwa Kibet amekuwa akikabiliwa na changamoto za kifedha.

Mnamo mwezi Machi, alimuomba, Elias Kiptum ambaye wamekuwa wakifanya mazoezi pamoja amsaidie kupata nafasi ya kukimbia Poland, lakini timu ya washiriki ilikuwa imekamilika.

“Nadhani hivyo ndivyo alivyoishia kufika Urusi,” Kiptum aliiambia BBC.

Baadaye mwaka huo, wakala wa michezo alipompa nafasi ya kwenda Urusi kushiriki mbio, Kibet alichukua fursa hiyo. Juhudi za BBC za kuwasiliana na wakala huyo ili kuthibitisha hili hazikufanikiwa.

“Alifurahi sana aliponiambia atashiriki mbio nchini Urusi,” kaka yake Kibet alisema. “Hata mimi nilifurahi. Tulikuwa na matarajio makubwa.”

Binamu yake, Bi Chesoi, ambaye alimsindikiza hadi kwenye kituo cha basi kwenye mkondo wa kwanza wa safari mwishoni mwa Julai, alisema alibeba “sanduku kubwa kiasi”.

Kibet aliiambia familia yake kuwa atakuwa huko kwa wiki mbili tu.

Kwenye video iliyorekodiwa nchini Ukraine, Kibet anasema kwamba alienda Urusi kama mgeni na si kwa ajili ya “kazi ya kijeshi”.

Wiki mbili baadaye, mwenyeji wake akamuuliza kama angependa kukaa muda mrefu zaidi.

“Nilisema: ‘Ndio, lakini tatizo ni kwamba muda wa viza yangu umeisha.’ Akasema: ‘Haina neno, ninaweza kukusaidia kwa hilo.'” Na kisha akamuahidi Kibet kazi.

“Jioni, alikuja na nyaraka zilizoandikwa kwa Kirusi. Aliniambia: ‘Hii ndio kazi ninayotaka ufanye.’

“Sikujua ni kazi ya kijeshi.”

Kibet anasema alitia saini nyaraka hizo na mwanamume huyo akachukua simu yake na pasipoti.

“Na hivyo ndivyo kila kitu kilivyoharibika… saini hiyo ulivuruga maisha yangu.”

‘Utapigana la sivyo tutakuua’

Kulingana na Kibet, watu wengine walikuja na kumuagiza aingie kwenye gari. Baada ya hapo tulisafiri kwa takribana saa saba.

“Nilijikuta katika kambi ya kijeshi.”

Kibet anasema alifahamishwa kuwa amejiandikisha kuwa jeshini na kwamba hakuwa na chaguo

“Niliambia: ‘Utapigana la sivyo tutakuua.”

Anasema lipewa mafunzo ya kimsingi kwa wiki moja, ambapo alionyeshwa jinsi ya kutumia bunduki ya rashasha. Hakuna hata mmoja wa makamanda wake aliyezungumza Kiingereza, kwa hiyo maagizo yalikua kupitia ishara.

Kibet anasisitiza kuwa hakuwahi kushiriki katika vita kwa sababu walipokwa njiani kuelekea katika kile ambacho kingekuwa misheni yake ya kwanza, aliacha vifaa vyake na kutoroka. Alizunguka kwa siku mbili katika msitu karibu na Vovchansk katika mkoa wa kaskazini-mashariki wa Kharkiv nchini Ukraine.

Baadaye alijisalimisha kwa wanajeshi wa Ukraine.

“Nilienda huku nikiwa nimenyanyua mikono juu,” anasema huku akirejelea alichofanya kwa ushara mbele ya kamera.

“Nilisema: ‘Mimi ni Mkenya, tafadhali msinipige risasi.’

“Kila mmoja alinielekezea mtutu wa bunduki, lakini nikawaambia watulie. Kamanda akaja, wakanifunga. Niliwaambia: ‘Hapana, sina silaha, sitaki chochote. Niko hapa kuokoa maisha yangu.”

Licha ya familia ya Kibet kukumbwa na mshtuko kutokana na video hiyo, kuna ahueni kwamba yuko mikononi mwa Waukraine.

“Tunahisi kwamba yuko salama [pamoja nao] badala ya kuwa nchini Urusi,” kaka yake Bw Kipyego alisema.

Familia inaomba mamlaka ya Kenya kuingilia kati. Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni bado haijatoa kauli yoyote kuhusiana na suala hilo.

“Ikiwa serikali ya nchi yake ya asili itaonyesha nia ya kurejeshwa kwake, Ukraine iko tayari kwa mazungumzo ya jinsi ya kumrudisha nyumbani,” msemaji wa Ukraine Bw Yatsenko alisema.

Hata hivyo, akizungumzia wafungwa wengine wa vita, aliongeza kuwa “nchi nyingi za Afrika hazijaonyesha nia ya kuwapokea tena raia wao kama hao”.

Kwa sasa kipaumbele cha jamaa wa Kibet ni usalama wake.

“Tunaomba kama alikosea, wamsamehe. Tunataka arudishwe tu,” kaka yake alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *