Chanzo cha picha, Getty Images
Mkutano mkuu wa masuala ya anga ya kimataifa ulifanyika katika jiji la Marekani la Colorado Springs mwezi Aprili 2025.
Marekani ni nchi yenye nguvu kubwa katika eneo la anga za juu, na sasa China pia inaibuka kuwa nchi yenye nguvu kubwa. Ina satelaiti za kisasa. China inafanya majaribio ya silaha zenye uwezo wa kuharibu satelaiti angani. Urusi pia imefanya hivyo.
Miongoni mwa wazungumzaji waliohutubia mkutano huo ni Jenerali Stephen Whiting, Kamanda wa Kamandi ya Anga za Juu ya Marekani na kusema, hakuna shaka kwamba anga ya kimataifa sasa iko ndani ya wigo wa eneo la vita.
Amesema hadi sasa hakuna vita vilivyopiganwa katika anga ya kimataifa na wala Marekani haitaki hilo litokee.
Kazi za satalaiti
Chanzo cha picha, Getty Images
Dk. Raji Rajagopalan, mtafiti wa masuala ya usalama wa anga katika Taasisi ya Mikakati ya Australia, anasema kwa sasa kuna satelaiti 11,700 katika obiti ya dunia.
Mawimbi ya satelaiti hutumiwa na mabilioni ya watu kwa mawasiliano ya kila siku. Takriban satelaiti 630 pia hutumiwa kwa shughuli za usalama wa kijeshi.
Anasema karibu nusu ya satelaiti zote za kijeshi, yaani satelaiti 300 zinatumiwa na Marekani. Urusi na China pia zina satelaiti nyingi za kijeshi. Setilaiti hizi hufanya kazi kama macho na masikio ya jeshi wakati wa operesheni za kijeshi.
Satelaiti zilitumika sana na vikosi vya Washirika katika Vita vya Ghuba vya 1990 dhidi ya Iraq. GPS inayotumia satelaiti ilitumika kwaongoza askari, vifaru, na magari ya kivita kwenye njia za jangwani.
Dk. Raji Rajagopalan anaeleza, “siku hizi, serikali zinatumia satelaiti kukusanya taarifa za kijasusi na kufuatilia maadui zao. Majeshi yote makubwa yatatumia mfumo huu katika siku zijazo. Satelaiti sio tu zinasaidia katika kutafuta shabaha lakini pia huongoza silaha kwa usahihi.”
Juni mwaka huu, India ilitangaza kuwa inafanyia kazi mpango wa kutuma satelaiti 52 angani ifikapo 2029.
Dkt. Raji Rajagopalan anasema, nchi yoyote inabidi kuliarifu Shirika la Umoja wa Mataifa la Anga kabla ya kurusha satelaiti. Aina ya satelaiti inayoituma angani, matumizi yake ni nini, itafanya kazi kwa muda gani na itarejeshwa vipi.
Sambamba na taarifa hizo, pia inabidi ielezwe ni eneo gani itapelekwa huko angani ili satelaiti isigongane na satelaiti nyingine. Bahati mbaya kwa sasa nchi nyingi hazitoi taarifa kamili kuhusu satelaiti zao.
Mwaka 1962, Marekani ilijaribu bomu la nyuklia angani, mionzi iliharibu satelaiti nyingi za mawasiliano. Miaka mitano baadaye, mkataba wa kimataifa ulitiwa saini, kupiga marufuku kupelekwa silaha za nyuklia na kemikali angani.
Shirika la Umoja wa Mataifa la anga za juu sasa linafuatilia mkataba huo. Dk. Raji Rajagopalan anasema shirika hili limefanya kazi nzuri sana katika kuweka usalama katika anga za juu.
Hata hivyo, mkataba huo haukatazi kutumwa kwa silaha za kawaida angani, ingawa silaha za kawaida zinaweza kusababisha uharibifu mkubwa.
Idadi ya satelaiti za kibiashara angani imeongezeka sana katika miaka michache iliyopita. Kuna zaidi ya satelaiti 8,000 za kampuni ya SpaceX ya Elon Musk, na makampuni kadhaa binafsi, ili kutoa huduma ya intaneti na huduma nyingine.
Nani mbabe wa anga?
Chanzo cha picha, Getty Images
Julian Suz, mtafiti katika Taasisi ya Kijerumani ya Masuala ya Kimataifa na Usalama, anasema ikiwa kuna shambulio popote duniani, tunaweza kuliona. Tunapata taarifa hizo kutokana na picha za satelaiti, data au rada.
Julian Suz anasema, “bado hakuna tukio la nchi kushambulia satelaiti ya nchi nyingine. Ila kuna matukio ya satelaiti kuvuruga mawimbi ya mawasiliano na kutoa ishara za uongo.”
Anaeleza kuwa kwa sasa rasilimali za anga za juu zimejumuishwa katika Kifungu cha 5 cha Mkataba wa NATO wa Washington, ina maana ikiwa mtu atashambulia satelaiti ya mwanachama wa NATO, hatua inaweza kuchukuliwa dhidi ya nchi inayoshambulia.
Julian Suz anasema zipo sababu nyingi kwa nini satelaiti huenda karibu na satelaiti nyingine. Linaweza kuwa ni jaribio la kuchukua picha ya setilaiti au kupata taarifa za kijasusi kuihusu. Hasa ikiwa habari kuhusu shughuli ya satelaiti hiyo hazijaelezwa mapema.
Marekani, Urusi, China, na India zina jeshi kubwa duniani. Jeshi la kila nchi limeunda silaha zenye uwezo wa kuharibu satelaiti nyingine angani. Hizi sio silaha za maangamizi, kwa hivyo hazijakatazwa kuzifanyia majaribio angani.
Julian Suz anasema Marekani ndiyo yenye nguvu zaidi angani. Mwaka 2008, iliharibu moja ya satelaiti zake. Zaidi ya hayo, Marekani inawekeza katika miradi mingine.
Kwa mfano, inatengeneza chombo cha anga cha X-37, ambacho kinaweza kurushwa angani kama roketi. Chombo hiki kinaweza kubaki angani kwa muda wa miaka miwili na kurudi chenyewe duniani.
Marekani pia inajaribu kutengeneza teknolojia ya mionzi kama njia mbadala ya GPS ya mawasiliano.
Urusi iliishinda Marekani katika mbio za anga za juu kwa kurusha satelaiti ya kwanza kuzunguka dunia mwaka 1957. Lakini tangu wakati huo, mpango wa anga za juu wa Urusi umekuwa nyuma ya Marekani.
Vikwazo vilivyowekwa kwa Urusi baada ya vita vya Ukraine pia vimeathiri mipango yake ya anga. Kwa upande mwingine, Marekani inategemea sana satelaiti zake kwa kukusanya taarifa za kijasusi na mawasiliano.
Urusi inaona huo ni udhaifu na inatengeneza silaha za kulenga satelaiti. China haiko nyuma katika eneo hilo pia.
Julian Suz anasema, “lengo la China lilikuwa kurusha satelaiti 100 mwaka 2024, lakini iliweza kutuma 30 pekee. China inatengeneza silaha kwa kasi ili kulenga satelaiti. Wakati huo huo, satelaiti zake zina uwezo wa kuzunguka kwa kasi satelaiti nyingine.”
Satelaiti huzunguka kwa kasi kubwa angani na zikigongana, vipande vyake vinaweza kutawanyika angani. Ni muhimu kutambua kwamba hata kipande cha sentimita moja, kinachosafiri kwa kasi kubwa, kinaweza kusababisha uharibifu mkubwa kama bomu la mkono.
Julian Suz anaonya kwamba katika hali kama hiyo, matumizi ya makombora kudungua satellite yanaweza kusababisha uharibifu wa kutisha.
Kwa mfano, ikiwa Urusi itatumia silaha kama hiyo angani, vipande kutoka katika satelaiti iliyo shambuliwa vinaweza pia kuharibu satelaiti nyingine.
Hivi majuzi, China na Urusi zimetia saini makubaliano ya kuweka kinu cha nyuklia kwenye Mwezi kitakachotumika kuzalisha umeme kwa ajili ya kazi ya baadaye ya utafiti huko.
Uzinduzi wa Teknolojia
Chanzo cha picha, Getty Images
Saadia Pekaranen, mkurugenzi wa Mpango wa Sheria ya Anga na Data katika Chuo Kikuu cha Washington, anasema teknolojia ya anga sio tu kuhusu roketi na vyombo vya anga.
Anasema pia inahusisha teknolojia kadhaa mpya, kama vile akili mnemba (ai), roboti zinazojiendesha, zinazojulikana kama EDT na roboti zinazojiendesha huruhusu mashine kufanya kazi kwa uhuru angani.
Kwa mfano Marekani, ina teknolojia ya Golden Dome ambayo inaweza kuilinda Marekani dhidi ya mashambulizi ya angani au mashambulizi ya makombora ya hypersonic. Mfumo huu unatumia satalaiti.
Sadia Pekaranen anasema kwa msaada wa akili bandia, jeshi litakuwa na uwezo wa kuchambua haraka data zilizopokelewa kutoka katika satelaiti na kuchukua hatua.
Sadia Pekaranen anasema Marekani na China ziko mbele sana kuliko nchi nyingine katika kuendeleza teknolojia hii.
Athari kwa Ulimwengu
Chanzo cha picha, Getty Images
Dk. Blevin Bowen ni Profesa Mshiriki wa Astropolitics katika Kituo cha Utafiti wa Anga katika Chuo Kikuu cha Durham, Uingereza, anashauri mashirika ya kimataifa kuhusu masuala yanayohusiana na vita vya satelaiti.
Anaamini kuwa iwapo kutakuwa na vita vya satelaiti angani, ni vigumu kukadiria kwa usahihi uharibifu. Anasema itategemea kwa kiasi kikubwa ni satelaiti gani zitaharibiwa.
Kwa mfano, chukua satelaiti zinazotoa mawimbi ya GPS, tunazotumia kupata maelekezo tunapoendesha gari au kuagiza chakula.
Kutakuwa na athari kwa huduma za kifedha, kwani satelaiti zina saa za atomiki, ambazo hutumiwa na benki na taasisi zingine za kifedha kuamua wakati miamala inapofanyika.
Wakulima na idara za hali ya hewa pia hutumia taarifa kutoka katika satelaiti kutathmini hatari za kilimo au majanga ya asili.
Vita katika anga za juu, vitakuwa na athari ya moja kwa moja kwa maisha ya watu na uchumi. Kwa mfano, ikiwa watu hawatapokea kwa wakati, taarifa sahihi kuhusu vimbunga au majanga mengine, watu wengi wanaweza kufa.