Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani, China na Urusi mara nyingi hutofautiana kuhusu masuala mengi ya kimataifa.
Hata hivyo, kuna jambo moja linalowaleta pamoja, wote wanaunga mkono Afrika kupata kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Lakini, licha ya makubaliano hayo ya nadra miongoni mwa mataifa yenye nguvu kubwa duniani, swali linaendelea kubaki, kwa nini hili bado halijatekelezwa?
Baraza la Usalama lina wanachama watano wa kudumu China, Urusi, Ufaransa, Uingereza na Marekani, wanaojulikana kama P5.
Hawa ndiyo pekee wana mamlaka ya kura ya turufu, yaani uwezo wa kuzuia azimio lolote la baraza kwa kupiga kura moja ya kupinga.
Nchi nyingine hupokezana viti vya muda katika baraza hilo, lakini bila haki ya turufu.
Afrika, licha ya kuwa na zaidi ya asilimia 28 ya uanachama wa Umoja wa Mataifa, haina mwakilishi yeyote wa kudumu katika kundi la P5.
“Hakuna usalama wa dunia bila usalama wa Afrika”
Chanzo cha picha, Getty Images
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, anaamini kuwa mabadiliko ya mfumo huu wa uwakilishi yamechelewa mno.
“Hakuna usalama wa dunia bila usalama wa Afrika,” anasema.
“Hatuwezi kukubali kuwa chombo kikuu cha dunia kuhusu amani na usalama kinakosa sauti ya kudumu kutoka kwa bara lenye zaidi ya watu bilioni moja idadi kubwa ikiwa ni vijana na ambalo linawakilisha zaidi ya robo ya wanachama wa Umoja wa Mataifa.”
“Wala hatuwezi kuvumilia hali ambayo maoni ya Afrika yanapuuzwa katika masuala ya amani na usalama, ndani ya bara lenyewe na pia duniani kote.”
Umoja wa Afrika (AU) umetaka “si chini ya viti viwili vya kudumu” vyenye haki ya kura ya turufu, pamoja na viti vitano vya muda katika Baraza la Usalama.
Ingawa nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinakubaliana kimsingi kuwa Afrika inastahili uwakilishi bora zaidi, utekelezaji wake umegubikwa na masuala ya kisiasa na kimaslahi.
Richard Gowan, mtaalamu wa diplomasia ya Umoja wa Mataifa, anasema:
“Urusi na China zimekuwa zikitamka wazi kwamba zinaunga mkono uwakilishi mkubwa wa Afrika, lakini hadi sasa hazijajitolea hadharani kuunga mkono idadi mahususi ya viti kwa bara hili.”
Kwa upande wa Marekani, Gowan anasema kuwa utawala wa Biden uliwahi kuahidi kuunga mkono Afrika kupata viti viwili vya kudumu lakini bila kura ya turufu.
Hata hivyo, utawala wa Trump haukubaliani na msimamo huo.
“Utawala wa Trump unapendelea hali ilivyo kwa sasa, ukifurahia kuwa sehemu ya kundi dogo lenye nguvu ya turufu,” anasema.
“Pia wana hofu kwamba kufungua tena Mkataba wa Umoja wa Mataifa kunaweza kufungua milango kwa mataifa mengine kudai viti vya kudumu, jambo litakalopunguza ushawishi wao kimataifa.”
Nchi zipi zitawakilisha Afrika?
Chanzo cha picha, Getty Images
Changamoto nyingine kubwa ni kuamua ni nchi zipi za Afrika zinazostahili kukalia kiti hicho cha kudumu.
Majina yanayotajwa mara kwa mara ni pamoja na Afrika Kusini, Nigeria, Kenya, Ethiopia, Algeria, na Misri.
Hata hivyo, hakuna makubaliano ya wazi wala mwafaka wa pamoja.
Wazo jingine ni kuiwakilisha Afrika kupitia Umoja wa Afrika (AU) kama chombo cha pamoja.
Lakini Gowan anasema kuwa AU haijawa na mafanikio ya kutosha katika diplomasia ya moja kwa moja.
“Kunapokuwa na maamuzi yanayohusisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza la Amani na Usalama la AU, mara nyingi kunakuwa na kutokuelewana juu ya masuala mahususi kama Somalia,” anasema.
“Wadiplomasia wa Kiafrika walioko New York mara nyingine huhisi kuwa wanapaswa kuchukua misimamo tofauti na AU, kwa sababu wanatambua kuwa Marekani au China haziwezi kuunga mkono kila azimio linalotoka AU.”
Wakati nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapokutana mjini New York kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa kila mwaka, suala la uwakilishi wa Afrika katika Baraza la Usalama linaendelea kuwa mada kuu ya majadiliano ya kimataifa.
Lakini hadi pale kutakapopatikana msimamo wa pamoja kuhusu:
- Idadi ya viti
- Mamlaka ya viti hivyo (ikiwa ni pamoja na haki ya turufu),
- Na ni nani atakayewakilisha bara hilo
Ndoto ya Afrika kuwa na sauti ya kudumu katika chombo hicho kikuu cha amani na usalama itaendelea kuwa bado njiani.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi