Chanzo cha picha, AFP
Kesi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini Dk. Riek Machar na viongozi saba waandamizi wa
upinzani wa SPLM-IO imefunguliwa Jumatatu mjini Juba chini ya ulinzi mkali
lakini iliahirishwa hadi Jumanne kufuatia mzozo juu ya mamlaka ya Mahakama
Maalum.
Machar alifikishwa mahakaman pamoja na
Waziri wa petroli aliyesimamishwa kazi Puot Kang Chol na washirika wengine
wakuu. Wanakabiliwa na mashtaka ikiwa ni pamoja na uhaini, mauaji, kula njama,
kufadhili ugaidi, na uhalifu dhidi ya ubinadamu, unaohusishwa na mapigano mnamo
Machi katika Kaunti ya Nasir, Jimbo la Upper Nile, ambayo yaliua zaidi ya
wanajeshi 250 na jenerali mwandamizi wa jeshi.
Upande wa
utetezi, ukiongozwa na Dk. Garry Raymondo, ulipinga mamlaka ya mahakama hiyo na
kusema kuwa inakiuka katiba ya mpito ya Sudan Kusini na Mkataba wa Amani
Uliofufuliwa wa 2018. “Katiba ya Mahakama hii Maalum sio tu haina
msingi wa mamlaka, lakini pia inaiweka Jamhuri ya Sudan Kusini katika ukiukaji
wa wazi wa majukumu yake chini ya sheria za ndani na za
kimataifa,”Dk.Raymondo aliiambia mahakama
Upande wa utetezi
ulisema kuwa Dk. Machar hawezi kukabiliwa na mashtaka ya jinai akiwa ofisini
bila idhini ya bunge, akitoa mfano wa ulinzi wa kikatiba.
“Vifungu vya
103 na 104 vya katiba ya mpito vinasema kwamba Makamu wa Kwanza wa Rais
hatakabiliwa na kesi za jinai akiwa ofisini, isipokuwa baada ya kuondolewa kwa
kinga na theluthi mbili ya wajumbe wote wa Bunge la Kitaifa,” upande wa
utetezi ulisema.
Upande wa
mashtaka unaoongozwa na wakili Ajo Ohisa ulitupilia mbali changamoto ya upande
wa utetezi, ukisisitiza kuwa Mahakama Maalum ina mamlaka kamili ya kusikiliza
kesi hiyo.
“Hoja ni
dhaifu na haina msingi. Wajumbe wa Mahakama hii Maalum wote ni majaji wa
Mahakama Kuu na kwa hivyo wana uwezo wa kusikiliza suala hilo. Hata kama
mamlaka ya Mahakama Kuu yanatumika, Mahakama Kuu ina mamlaka yasiyo na kikomo,
na uhalifu uliofanywa chini ya Sura ya 5 na 6 uko ndani ya uwezo wake,
“Bw.Ohisa aliiambia mahakama.
” Kikao hiki
sio kumondoa au kumshtaki Makamu wa Kwanza wa Rais. Hii ni kesi ya mahakama
ndani ya uwezo wa mahakama ya Jamhuri ya Sudan Kusini. Haina uhusiano wowote na
kuondolewa ofisini,” aliongeza
Usalama mjini
Juba uliimarishwa wakati kesi ilipofunguliwa, huku askari wakipelekwa katika
jiji lote kuwalinda wafungwa na kuzuia machafuko. Waangalizi wamesema uwepo mkubwa wa maafisa wa usalama ulichochea wasiwasi kati ya wakazi, na biashara zingine zimefungwa huku raia wengine wakiamua kukaa nyumbani
Majaji
waliahirisha kesi hiyo hadi Jumanne, wakielekeza upande wa mashtaka kuwasilisha
jibu la maandishi kwa pingamizi za mamlaka.