Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Marina Daras
- Nafasi,
Baada ya hatua ya hivi punde ya Ufaransa, Uingereza, Canada na Australia kulitambua taifa la Palestini mengine zaidi yanatarajiwa kufuata mkondo huo.
Lakini mataifa ya Afrika yanaichukuliaje Palestina?
Nchi nyingi za bara hilo ziliitambua Palestina katika miaka ya 1980 baada ya kiongozi wa Palestina, Yasser Arafat kutangaza uhuru wake mjini Algiers.
Viongozi kama Thomas Sankara na Nelson Mandela hata walihusisha mapambano ya Wapalestina na mapambano ya ukombozi wa Afrika yenyewe.
Hata hivyo, nchi mbili – Cameroon na Eritrea – hazijafikia uamuzi huo.
Tunaangalia sababu za uamuzi wao.
Cameroon
Chanzo cha picha, Getty Images
Taifa hili la Afrika Magharibi lina uhusiano wa karibu na Israel.
David Otto, Mkurugenzi wa Ulinzi, Kituo cha Geneva cha Usalama wa Afrika na Mafunzo ya Kimkakati, anasema Israel inaiona Cameroon kama moja ya washirika wake wwakuu barani Afrika.
“Cameroon haiwezi kuvuruga uhusiano wake na Israel kutokana na sababu za kidiplomasia,” anasema Otto.
Anasema uhusiano huo ni wa kina na unategemea zaidi usalama.
“Israel imechangia na inaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa kulinda utawala wa Cameroon,” anasema.
Israel imeipa mafunzo ya kijeshi vikosi maalum vya Cameroon na inadhaniwa kuwa bado inashirikiana na kitengo maalum kinachotoa ulinzi wa kibinafsi wa rais.
“Uhusiano ambao Cameroon imedumisha na Israel pia umeileta Marekani kuwa karibu nao kwa kuwa mshirika wa karibu sana wa Israel katika nyanja zote.”
Msimamo wa Cameroon kuhusu Palestina pia huenda umechangiwa na mapambano yake yenyewe katika maeneo ya watu wanaozungumzo Kiingereza wanaotaka kujitenga.
“Kutalimbua taifa la Palestina kunaweza kuibua hali ya mtafarunku nchini humo, kwasababu serikali italazimika kuzingatia hilo kwa kulitambua vuguvugu la watu wanaotaka kujitenga. Utawala wa Cameroon umesema wazi kwamba nchi hiyo ni moja na haiwezi kugawanyika,” anasema Otto.
Msimamo wa Cameroon kwa kiasi kikubwa umechukuliwa kimya kimya kwa tahadhari. Msimamo wa Eritrea, hata hivyo, umeundwa na historia tofauti sana, iliyojikita katika mapambano yake ya kujitawala.
Eritrea
Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo 1988, wakati Yasser Arafat alipotangaza Palestina kuwa nchi huru, alihitaji kuungwa mkono na nchi za Kiafrika.
Mmoja wao alikuwa Ethiopia.
“Makao makuu ya Afrika, au Shirika la Umoja wa Umoja wa Afrika wakati huo, baadaye ukaja kuwa Umoja wa Afrika yako mjini Addis Ababa, Ethiopia” anasema mchambuzi wa kisiasa wa Eritrea, Abdurahman Sayed.
“Utawala wa kijeshi nchini Ethiopia pia ulikuwa ukiunga mkono Usovieti na hivyo kuunga mkono kwa kauli mojo haki na mapambano ya Wapalestina.”
Lakini Eritrea wakati huo ilikuwa ikipigania uhuru wake dhidi ya Ethiopia.
“Ni wazi, wakati huo, Ethiopia ilikuwa inaikalia Eritrea. Na Waeritrea walikuwa katika mapambano, mapambano ya silaha, dhidi ya uvamizi wa Ethiopia,” anasema Sayed.
“Ili Wapalestina waanzishe uhusiano wa aina yoyote na Waethiopia, ilibidi wajitenge na Waeritrea kwa maslahi ya Eritrea, na ndivyo nadhani Yasser Arafat alifanya, hatua hiyo haikupokelewa vyema na Waeritrea kwa ujumla, lakini rais wa sasa pia,” anasema.
Hata hivyo, Rais wa Eritrea Isaias Afwerki alisikitishwa na kadhia ya Palestina na mwaka 2012 na hata kupiga kura kuunga mkono taifa la Palestina “nchi isiyo mwanachama kamili” katika Umoja wa Mataifa.
Lakini pia alipuuzilia mbali juhudi za amani kama vile kutekelezwakwa Makubaliano ya Oslo, ambayo yaliweka mfumo wa amani uliowapa Wapalestina uwezo wa kujitawala katika sehemu za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Gaza kama hatua ya kuelekea taifa huru.
“Rais wa Eritrea alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupuuzilia mbali makubaliano ya Oslo ya mwaka 1993 akiyataja kuwa makubaliano yasio na tija ana ambayo hayatazingatia chanzo cha mzozo au suala la haki na harakati za Wapalestina kutaka kujitawala,” anasema Abdurahman Sayed.
Rais fwerki anasema haungi suluhisho la muda mrefu wa kufikia amani katika la West Bank kwa kufuata mpango ujulikanao kama Two-State State.
Lakini huenda anakabiliwa na upinzani kutoka asilimia 55 ya raia wa nchi hiyo ambao ni waumini wa dini ya Kiislamu.
“Eritrea ilipatikana kutokana na mapambano yake ya kujitawala. Kwa hivyo, kwa mtu aliyeongoza au aliyekuwa sehemu ya mapambano ya ukombozi kutounga mkono ukombozi wa watu wengine, kimaadili haionekani kuwa sawa. Kungekuwa na shinikizo kubwa kwao,” anasema Sayed.
BBC imewasiliana na serikali zote mbili ili kupata maoni lakini haijapata majibu.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi