
Bondia mkongwe nchini Tananzani ambaye sasa amegeukia ukocha wa mabondia anasema miaka ya nyuma mchezo wa ngumi haukua na faida yoyote zaidi kupata sifa, jina na umaarufu usiokuwa na tija.
“Nilipoacha niliacha kipato, nimeambulia jina tu ngumi jiwe ngumi jiwe” – Shomvi Said.
Elimu dunia na umasikini vilimfanya kuingia kwenye mchezo wa ngumi tangu mwaka 1965 wakicheza kujifurahisha tu mitaani na kushindana wao kwa wao. Shomvi alifurahia mchezo wa ngumi mpaka mwaka 1990 alipopigwa na kupata jeraha la kichwa lilomsababishia pia matatizo ya ubongo kwa wakati huo na kulazimika kuachana na mchezo huo.
Baada ya kuuguza jeraha lake kwa muda alijikuta akifundisha vijana aliokuwa akifanya nao mazoezi na tangu wakati huo ameendelea na kazi hii mpaka leo.
Kwa sasa anawafundisha vijana zaidi ya 20 ambao wanajivunia uwezo wake licha ya kwamba mazingira wanayofanyia mazoezi ni duni, yasiyo na vifaa vya kisasa wala vya kutosha.
“Tangu ameanza kutufundisha hakuna bondia wake hata mmoja amepigwa KO, ndiyo maana unaona bado tupo sababu anatupa mbinu na morali ”- anasema bondia Abeid Salim Issa.
Mzee huyu wa miaka 81, mzaliwa wa Kisarawe mkoa wa Pwani nchini Tanzania kwa sasa anasumbuliwa na tatizo la magoti ambalo linafanya hata kutembea kwake kuwa kwa shida, hivyo mara nyingi huwafundisha mabondia wake akiwa amekaa kitako kutokana na kushindwa kusimama kwa muda mrefu. Licha ya kutafuta tiba maeneo mbali mbali ikiwemo hospitali ya taifa Muhimbili nchini Tanzania tatizo hilo bado linaendelea kumdhoofisha.
“Nimekwenda Muhimbili nimetoa maji karibu mara nne yanakuwa ya njano yanashombo sana, basi mimi nakaa hapa nafundisha jamaa zangu hawa naangalia tu wewe unakwenda vibaya nenda hivi nenda hivi”.- anafafanua.
Kutokana na ukosefu wa fedha Shomvi maarufu kama Ngumi jiwe hulazimika kutengeneza vifaa vya kufanyia mazoezi akitumia vitu vinavyopatikana kwenye mazingira anamoishi kama vile makopo ya maji, mifuko ya plastiki na wakati mwingine hata chuma chakavu. Anasema anatengeneza vitu kama ‘spidi ball’ pingu za kunyoosha mikono, mifuko ya kupiga, pamoja na vyuma vyenye uzito tofauti.

Baba huyu wa watoto 16 hajapata mafunzo yoyote ya ukocha wa masumbwi zaidi ya uwezo binafsi na uzoefu aliopata ulingoni miaka mingi iliyopita na kutokana na uwezo wake amejijengea imani na hata wakati mwingine hutumiwa na watu maarufu wanaotaka mafunzo binafsi ya ndondi.
Alipewa jina la Ngumi jiwe miaka kadhaa baada ya kuwa ameachana na mchezo huo baada ya kumpiga mwendesha guta (baiskeli ya miguu mitatu inayotumika kubeba mizingo) aliyemgonga wakati akiendesha baiskeli kisha kumshambulia kwa matusi kwa kutosikia kengele ya baiskeli.
“Nilipiga ngumi mbili tu chini, kuna mama alikuwa anapita pembeni akasema huyu baba kapiga ngumi au jiwe? tangu hapo ngumi jiwe ngumi jiwe…” Anabainisha Shomvi.
Licha ya umaarufu na jina kubwa alilolijenga kwenye himaya ya wapenda masumbwi, Shomvi anasema hakuna manufaa ya kifedha yoyote aliyoyapata na anatamani kurudisha wakati nyuma kwani miaka ya hivi karibuni mabondia wanapata fedha nyingi jambo ambalo kwa baadhi ni changamoto sababu ya ulimbukeni wanakosa nidhamu na kuishia vibaya.
Katika siku za hivi karibuni mchezo wa ngumi nchini Tanzania umekuwa na umaarufu kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa kwenye uandaaji wa mapambano na urushaji mapambano hayo moja kwa moja kwenye televisheni.
Ukubwa wa mabondia kama Twaha Kiduku na Mfaume Mfaume ni matoke ya uwekezaji huo licha ya kwamba mambondia wengi bado wana hali duni kiuchumi.
Imehaririwa na Florian Kaijage