Leo ni Alkhamisi mwezi Pili Mfunguo Saba Rabiu Thani inayosadifiana na tarehe 25 Septemba 2025 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Milaadia, iliasisiwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Jumuiya hiyo ni ya pili kwa ukubwa baada ya Umoja wa Mataifa kwa kuwa na nchi wanachama 57 katika mabara zaidi ya manne. Jumuiya hiyo inahesabiwa kuwa sauti ya ulimwengu wa Kiislamu yenye jukumu la kulinda maslahi ya Waislamu, kueneza moyo wa amani na kuratibu masuala ya Waislamu. Jumuiya hiyo iliundwa katika mkutano wa Kihistoria uliofanyika Rabat nchini Morocco tarehe 25 Septemba mwaka 1969 kama jibu la hatua ya Wazayuni wa Israel ya kuchoma moto Msikiti wa al Aqsa huko Baitul Muqaddas.

OIC

Miaka 120 iliyopita, katika siku kama ya leo yaani mwezi Pili Mfunguo Saba Rabiu Thani 1327 Hijria, Ayatullah “Ali Foumani Rashti”, mwanazuoni mpambanaji wa Iran, aliuawa shahidi. Alizaliwa mwaka 1268 Hijria katika mji wa Rasht kaskazini mwa Iran na alijifunza misingi ya sayansi ya Kiislamu kutoka kwa baba yake na baadhi ya wanazuoni wengine wa mji huo. Ayatullah Foumani Rashti alikuwa na umri wa miaka ishirini alipokwenda Karbala na kisha Najaf kukamilisha elimu yake na akawa gwiji na mwanachuoni mkubwa katika elimu ya fiqhi, falsafa na mantiki, na akafikia daraja ya ijtihad. Alirejea Rasht mwaka 1312 Hijiria. Akiwa katika mji huu alikozaliwa, aliendeleza mafundisho ya Kiislamu na wakati wa Mapinduzi ya Katiba nchini Iran, alitoa mwito wa kuweko utawala wa sheria za Kiislamu. Hata hivyo, wapinzani wa Ayatullah Foumani Rashti hawakukubali msimamo na ushawishi wake, hivyo waliamua kuua shahidi katika siku kama ya leo.

Ayatullah “Ali Foumani Rashti”

Katika siku kama ya leo miaka 128 iliyopita alizaliwa mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. Faulkner hakukamilisha masomo yake ya juu na alianza kujishughulisha na kazi mbalimbali ka ajili ya kuendesha maisha. Mwandishi huyo mashuhuri alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili raia weusi wa nchi hiyo. Riwaya za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa sasa nchini Marekani. Mwaka 1950 mwandishi huyo alitunukiwa tuzo ya fasihi ya Nobel.

William Faulkner

Na siku kama ya leo miaka 18 iliyopita aliaga dunia Edward Said, mwandishi na mwanafikra wa Kipalestina kutokana na maradhi ya saratani. Said alizaliwa mwaka 1935 katika familia ya Kikristo. Alielekea Marekani kwa ajili ya kudumisha elimu akiwa na umri wa miaka 17 na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo kikuu cha Harvard. Kitu kilichompa umashuhuri zaidi Prf. Edward Said katika upeo wa kimataifa ni jitihada zake kubwa za kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina bila ya kusita. Mwanafikra huyo mtajika alifikisha sauti ya kudhulumiwa wananchi wa Palestina katika masikio ya walimwengu kupita makala na vitabu vyake. Ameandika vitabu vingi na muhimu zaidi ni kile alichokipa jina la Orientalism ambacho ndani yake anaeleza jinsi wataalamu wa masuala ya Mashariki wa Wamagharibi wanavyotumiwa kama wenzo wa wakoloni kwa ajili ya kuhalalisha uporaji wa mali na maliasili za mataifa ya Mashariki mwa dunia.

Edward Said

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *