picja ya viongozi wa Turkey, Jordan na Marekani wakiwa wamekaa sako kwa bako

Chanzo cha picha, Getty Images

Axios iliripoti kuwa Rais wa Marekani Donald Trump, akiwa na mjumbe wake maalum Steve Witkoff, waliwasilisha mpango wa “mambo 21” kwa viongozi wa Kiarabu na Kiislamu waliokutana nao jijini New York Jumanne, wenye lengo la kusitisha vita vya Gaza na kuanzisha serikali mpya ya baada ya Hamas.

Ripoti hiyo ilisema waliokuwepo walipokea mpango huo kwa mtazamo chanya.

Kwa mujibu wa vyanzo viwili vya habari, Trump aliwaambia viongozi hao katika mkutano uliofanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Newyork kuwa vita hivyo vinapaswa kukoma mara moja.

Aliongeza kuwa kila siku vita vinapoendelea, Israel inazidi kutengwa kimataifa.

Mpango huo unatajwa kuwa mkusanyiko wa mawazo yaliyojadiliwa katika miezi sita iliyopita, pamoja na maboresho ya mapendekezo ya awali yaliyotolewa na mkwe wa Trump, Jared Kushner, na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair hii ni kwa mujibu wa jarida la Axios.

Kwa mujibu wa Axios, misingi mikuu ya mpango huo ni

  • Kuachiliwa kwa mateka wote waliobaki,
  • Kusitishwa kwa mapigano kwa kudumu,
  • Kuondolewa kwa majeshi ya Israel hatua kwa hatua kutoka Gaza.

Mpango huo pia unazungumzia jinsi Gaza itakavyotawaliwa baada ya vita, bila Hamas kushiriki.

Unapendekeza kuundwa kwa kikosi cha usalama chenye mchanganyiko wa Wapalestina na wanajeshi kutoka nchi za Kiarabu na Kiislamu, na pia kuipa Mamlaka ya Palestina jukumu fulani la utawala.

Aidha, mpango unapendekeza nchi za Kiarabu na Kiislamu zifadhili serikali mpya ya Gaza pamoja na juhudi za ujenzi upya wa Ukanda huo.

Vyanzo vya habari vya Marekani vinasema kuwa Trump aliwataka viongozi hao wa Kiarabu na Kiislamu waunge mkono mpango huo na wajitolee kushiriki katika utekelezaji wake baada ya vita.

Soma pia:

Mjumbe wa Marekani, Steve Witkoff, alisema Jumatano:

“Tuna matumaini na hata tunaamini kwamba katika siku chache zijazo tutatangaza hatua ya maana kuelekea kusitisha vita Gaza.”

Mpango huo uliwasilishwa katika mkutano kati ya Trump na viongozi kutoka Saudi Arabia, UAE, Qatar, Misri, Jordan, Uturuki, Indonesia na Pakistan, uliofanyika pembezoni mwa mikutano ya Umoja wa Mataifa.

Masharti ya mataifa ya kiarabu kwa Trump

Kwa mujibu wa Axios, baadhi ya viongozi wa Kiarabu waliweka masharti ya kuunga mkono mpango huo.

Masharti hayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa Israel haitachukua maeneo ya Ukingo wa mto Jordan au Gaza, wala kujenga makazi ya walowezi katika Gaza.

Viongozi hao pia walisisitiza kuwa Israel isivuruge hali ya sasa ya Msikiti wa Al-Aqsa na iongeze mara moja misaada ya kibinadamu kwa Gaza.

Politico iliripoti kuwa Trump aliahidi hataruhusu Israel kuchukua sehemu yoyote ya Ukingo wa mto Jordan.

Jumatano, viongozi wa nchi saba za Kiarabu na Kiislamu waliounga mkono mpango huo walitoa taarifa ya pamoja wakisema:

“Tunathibitisha nia yetu ya kushirikiana na Rais Trump, na tunatambua umuhimu wa uongozi wake katika kusitisha vita na kufanikisha amani ya haki na ya kudumu.”

Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi, kupitia mitandao ya kijamii, alisema:

“Nathamini juhudi za Rais Trump kusitisha vita… na napokea kwa moyo mkunjufu mapendekezo aliyowasilisha katika mkutano wake na viongozi wa Kiarabu na Kiislamu jana jijini New York. Naona huu kuwa msingi muhimu wa kuanzia kujenga amani ya kudumu.”

Siku hiyo hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na mjumbe Witkoff walikutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Qatar, UAE, Misri na Jordan ili kubadilisha mapendekezo ya awali ya Trump kuwa mpango wa kina na wa utekelezaji.

Israel imeupokeaje mpango huo?

Axios pia iliripoti kuwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anafahamu kuhusu mpango huo.

Balozi wa Israel, Ron Dermer, ameshafanya mazungumzo kuhusu mpango huo na Kushner pamoja na Blair.

Trump aliwaambia viongozi wa Kiarabu kuwa hatua inayofuata ni kuujadili mpango huo na Netanyahu katika Ikulu ya White House siku ya Jumatatu ili kupata ridhaa yake, kwa mujibu wa chanzo kilichozungumza na Axios.

Mwishoni, afisa mmoja wa Kiarabu alinukuliwa akisema:

“Mpango wa Marekani ni mzuri, lakini unahitaji kuboreshwa kwa kushirikisha mawazo ya nchi za Kiarabu. Ukishakamilika, Marekani itapaswa kuusambaza kwa Netanyahu ili kuungwa mkono.”

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *