Watu 11 wameuawa kwenye mashambulizi ya anga la Israel yaliyoilenga nyumba waliyokuwa wakijihifadhi katikati ya Gaza baada ya kuyakimbia makazi yao hayo ameeleza msemaji wa ulinzi wa raia wa eneo hilo.
Wakati huohuo mashambulizi ya ardhini ya jeshi la Israel katika mji wa Gaza City yamewalazimisha maelfu ya Wapalestina kuukimbia mji huo kutokana na mashambulizi makali yanayoendelea. Vyanzo vya usalama vya Israel vimesema idadi ya watu waliolihama jiji la Gaza City imeongezeka hadi kufikia watu laki saba kutoka takriban watu 640,000.
Katika maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza, Wapalestina wasiopungua 41 wameuawa kwenye mashambulizi ya Israel kulingana na duru za hospitali.
Mjumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump ameonyesha matumaini juu ya mpango mpya wa kuvimaliza vita bila ya kusema kama Israel au Hamas wameukubali mpango huo.
Huku hayo yakiendelea, katika mji wa kusini mwa Israel wa Eilat watu 22 wamejeruhiwa na ndege isiyo na rubani iliyorushwa na waasi wa Houthi wa Yemen. Ni tukio la nadra ambapo mfumo wa ulinzi wa ang awa Israel ulishindwa kuzia mashambulizi hayo.
Na hapa nchini Ujerumani vikwazo vya Kansela Friedrich Merz, juu ya serikali yake kusimamisha mauzo ya silaha kwa Israel alivyovitangaza mwezi Agosti vimeidhinishwa na hivyo kwa muda wa wiki tano za kwanza hakutakuwa na uwasilishaji wa silaha kwa Israel baada yakufikiwa uamuzi huo.
Mbunge wa chama cha Kijani Ulrich Thoden, ameiambia kamati ya Bunge ya Wizara ya Uchumi inayochunguza vikwazo hivyo kwamba kati ya Agosti 8, siku ambayo Merz alitangaza vizuizi hivyo, na Septemba 12, hakuna vibali vilivyotolewa.
Chama cha mrengo wa kushoto kimetoa wito wa kusitishwa kikamilifu uuzaji wa silaha kwa Israel na ikiwezekana kukomesha ushirikiano wa kijeshi. Chama cha kijani kimeitahadharisha serikali ya Ujerumani juu ya hatari ya kushiriki katika ukiukaji wa sheria za kimataifa dhidi ya watu wa Palestina.
Mengineyo Waziri wa Ulinzi wa Italia Guido Crosetto amesema hii leo nchi yake imepeleka meli ya pili ya kikosi cha wanamaji kuziunga mkono takriban boti 50 za misaada Global Sumud Flotilla, za wanaharakati wa kimataifa ambazo zinakabiliwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani wakati zikijaribu kupeleka msaada Gaza. Mwanaharakati wa mazingira wa Sweden Greta Thunberg yumo kwenye msafara huo. Uhispania pia imechukua hatua kama ya Italia na imepeleka meli ya kivita kuulinda msafara wa flotilla.
Vyanzo: AFP/AP/RTRE/DPA