.

Chanzo cha picha, Getty Images

“Magari ya zamani ya kijeshi yaligeuzwa kuwa mabomu makubwa na kuwekwa katikati mwa vitongoji vya makazi na kulipuliwa kwa mbali yakibomoa majengo yote, na kuharibu chochote ambacho kingekuwa karibu kwa sekunde; athari ya mabomu haya ni mbaya zaidi kuliko mashambulizi ya angani.”

Hivi ndivyo Alam al-Ghoul, ambaye anaishi katika Jiji la Gaza, alielezea kile wakazi wanachokiita ” mabomu ya roboti.” Wanasema ni mara ya kwanza kuona silaha kama hiyo katika miaka ya vita ambayo wamevumilia, na kwamba mashambulizi yanayowahusisha yanazidi kuwa ya mara kwa mara.

“Roboti hizi zinaweza kuwa vifaru vya zamani au magari ya kijeshi ambayo hawafai tena kwa madhumuni hayo,” Ghoul alisema.

“Wanayachukua, kuyajaza vilipuzi, na kuyapeleka katika mitaa ya Jiji la Gaza, na kuyalipua kwa mbali wakitumia rimoti,” alieleza BBC.

‘Ikiwa kuna watu karibu na mlipuko huo, hakuna chembe yao itakayopatikana. Hata mabaki yao yatatawanyika, na hatuwezi kuwapata wakiwa wazima,” alisema Ghoul, ambaye mara kwa mara hujitolea kusaidia kutafuta miili ya wahanga wa vita huko Gaza.

Majengo hubomolewa kabisa au kuwachwa bila udhibiti, ikitegemea ukaribu wao na mlipuko huo, na kuacha eneo hilo wazi kwa wanajeshi wa Israel “kana kwamba ni operesheni ya kufagia,” Ghoul aliongeza.

Ameshuhudia madhara ya uharibifu huo na aliambia BBC kuwa “familia nyingi zimeangamizwa.”

“Familia hizo zilikuwa majumbani mwao wakati ‘roboti’ zilipolipuka, na nyumba zao zikaanguka juu yao. Baadhi bado ziko chini ya vifusi katika vitongoji kama vile Al-Zaytoun, Seikh Radwan, na Jabalia,” aliongeza.

Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Gaza inayoendeshwa na Hamas ilisema kuwa jeshi la Israel limekuwa likifanya operesheni ya kijeshi katika mji wa Gaza tangu Agosti 13, na kuua zaidi ya watu 1,200 na kujeruhi zaidi ya 6,000, kulingana na takwimu zilizotolewa na idaya ya afya na mamlaka rasmi ya Ukanda huo.

Katika taarifa hiyo, Hamas inasema oparesheni hizo za kijeshi ni pamoja na mashambulizi makali ya angani yenye zaidi ya mashambulizi 70 ya moja kwa moja ya ndege za kivita, pamoja na kulipua zaidi ya roboti 100 za vilipuzi katika maeneo yenye watu wengi, na kusababisha watu wengi kulazimika kuyahama makazi yao.

Pia unaweza kusoma
.

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images

Jeshi la Israel linafanya mashambulizi makali katika mji wa Gaza, huku vyombo vya habari vya Israel vikiripoti milipuko yenye nguvu kiasi kwamba inaweza kusikika Tel Aviv, umbali wa kilomita 70 hivi.

BBC News Arabic iliwasiliana na Luteni Kanali Avichay Adraee, msemaji wa jeshi la Israel Defence Forces (IDF), kwa maoni yake kuhusu madai kwamba jeshi limesambaza silaha hizi dhidi ya raia.

Adraee aliiambia BBC: “Hatujadili mbinu za uendeshaji, lakini naweza kusema kwamba tulitumia njia mbalimbali-baadhi ya ubunifu wa hali ya juu na kutumika kwa mara ya kwanza-kufikia malengo yetu, kuwaondoa magaidi wa Hamas na kuwalinda wanajeshi na raia wa Israel.”

.

Chanzo cha picha, Reuters

Milipuko yenye uharibifu mkubwa

Nidal Fawzi, mkazi mwingine wa Mji wa Gaza, alishangaa kama Gaza imekuwa uwanja wa majaribio kwa silaha za Israeli, akibainisha kuwa roboti “hupanda hofu, hasa miongoni mwa wanawake na watoto, na kuwalazimisha watu kutoroka.”

Aliambia BBC kuwa ameona silaha hizo zikitumika wakati wa operesheni ya awali ya kijeshi.

“Ilikuwa usiku wa manane. Niliona ‘roboti’ kubwa ya mstatili ikivutwa na gari la kijeshi. Waliiacha karibu na ukuta na kuliendesha gari hilo. Nilipiga kelele kwa familia yangu watoke nje mara moja. Dakika chache baada ya kukimbia, kulikuwa na mlipuko ambao sijawahi kuona hapo awali.”

Fawzi alielezea mlipuko huo kuwa mbaya:

“Huko Al-Zaytoun, niliona miili ikigeuzwa na kuwa vipande vidogo. Hata katika umbali wa mita 100, watu walikufa kutokana na shinikizo la mlipuko na kukosa hewa. Hii ndiyo silaha ya kutisha zaidi ambayo tumeona katika vita hivi.”

Wakazi ambao walikimbia kabla ya kulipuka “walikuwa wakifikiria tu kutoka nje,” wakijaribu kutoroka “zimwi la chuma lililolipuka,” Fawzi anakumbuka.

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Kupunguza gharama ya mapigano ya kijeshi

Profesa Hani al-Basous, mtaalam wa masuala ya usalama katika Chuo cha Joaan Bin Jasim cha Mafunzo ya Ulinzi nchini Qatar ambaye hapo awali alifanya kazi katika Ukanda wa Gaza, aliambia BBC kwamba jeshi la Israel linatumia magari hayo ya milipuko yanayodhibitiwa kwa mbali kuharibu maeneo ya makazi, vichuguu na majengo makubwa bila kuingilia moja kwa moja ili “kupunguza gharama ya uvamizi wa kijeshi na kuepusha maafa ya wanajeshi wa Israel.”

Alibainisha kuwa hubeba kiasi kikubwa cha vilipuzi na yamekuwa yakitumika katika vichuguu na vitalu vya makazi, na kusababisha milipuko mikubwa.

Karem al-Gharabli, mkazi mwingine wa Gaza, aliiambia BBC kwamba aliona silaha hiyo ikifanya kazi mnamo Aprili 2025, wakati wa shambulio la Israeli kwenye jengo la makazi la ghorofa mashariki mwa Gaza City.

“Nilikuwa umbali wa mita 400 kutoka kwa mlipuko huo, lakini vipande vyote vya mawe viligonga nyumba yetu,” Gharabli alisema.

“Anga iligeuka nyekundu na mwanga ulikuwa ukipofusha. Ilikuwa ya kutisha.”

Dk. Munir al-Bursh, mkurugenzi mkuu wa Wizara ya Afya ya Palestina, alisema jeshi la Israel sasa linategemea “roboti” za vilipuzi ndani ya Mji wa Gaza kila siku, na kudai kuwa ni “mbinu inayoleta tishio la moja kwa moja kwa raia na kuzidisha maafa ya kibinadamu.”

Anadai kuwa kila mmoja hubeba hadi tani saba za vilipuzi, huku kati ya saba na kumi vikilipuliwa kila siku, na kulazimisha watu wengi kuhama makazi yao na kuongeza msongamano wa watu magharibi mwa Gaza hadi watu 60,000 kwa kilomita moja ya mraba.

Anaonya kwamba kuendelea kwa matumizi ya roboti hizi kunaweza kusababisha “mauaji na uharibifu wa miundombinu ya makazi,” haswa ikizingatiwa uhaba wa uwezo wa uokoaji na misaada.

*Kwa kuzingatia hali ya sasa ya Gaza, haikuwezekana kupata picha za magari yaliyotajwa katika makala haya, au matokeo ya mara moja ya mlipuko. Picha katika nakala hii zilipigwa baada ya shambulio la hivi majuzi zaidi la Israeli kwenye Jiji la Gaza.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *