Hotuba hiyo ya Abbas katika siku ya nne ya Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inatarajiwa kuzusha hisia kali za mshikamano miongoni mwa mataifa wanachama wa Umoja huo, ambao wengi wao wameamua tayari kuitambua Palestina kama taifa huru, baada ya siku tatu zilizopita, Ufaransa, Canada na Uingereza kuwa mataifa makubwa ya Magharibi kuchukuwa hatua kama hiyo.
Abbas, ambaye anatawala zaidi kwenye Ukingo wa Magharibi kuliko kuitawala Palestina yote, atalazimika hata hivyo kuhutubia kwa njia ya video, kufuatia uamuzi wa Marekani kumnyima viza kiongozi huyo ya kuingia nchini humo kushiriki mkutano huo unawaowakutanisha viongozi mbalimbali wa mataifa na serikali 150 duniani.
Moja ya yale anayotarajiwa kuyagusia katika hotuba yake ni kuhusu vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza na matukio ya mauaji na uchukuliwaji wa ardhi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel.
Viongozi wengine waliopangwa kuzungumza hii hii leo katika mkutano ni pamoja Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa na mawaziri wakuu wa mataifa ya Ubelgiji, Italia na Uholanzi.
Syria yahutubia mkutano huo baada ya miaka 60
Siku ya Jumanne kwa mara ya kwanza baada ya miaka 60, Syria iligeuza ukurasa mpya ambapo rais wa nchi hiyo, Ahmad Al-Sharaa, alipohutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Katika hotuba yake aligusia madhila waliyoyapitia watu wa Syria wakati wa utawala uliopita chini ya Bashar al Assad.
“Utawala uliopita umewaua takriban watu milioni moja, umewatesa mamia kwa maelfu, umewalazimisha takriban watu milioni 14 kuwa wakimbizi na kuharibu nyumba karibu milioni moja na kuwapoteza wakaazi wake. Mabibi na mabwana, watu dhaifu wamekuwa wakilengwa kwa silaha za kemikali na kuongeza idadi ya matukio yaliyorekodiwa, watoto wetu, wanawake na vijana wadogo. Watu wamekuwa wakivuta gesi yenye sumu.” amesema Al-Sharaa.
Duru zinaarifu kwamba wakati alipokuwa akizungumza, mamia ya watu walikusanyika mbele ya
skrini kubwa katika miji mbalimbali nchini mwake wakishuhudia hotuba yake huku wakipeperusha bendera ya nchi hiyo.
Mbali na Ahmad Al-Sharaa, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran naye alitoa hotuba yake na ameweka wazi kwamba nchi yake haina mpango wowote wa kutengeneza silaha za nyuklia huku zikiwa zimebaki siku chache kabla ya vikwazo vya kimataifa kuanzishwa tena dhidi ya taifa hilo la Kiislamu katika Ghuba ya Ajemi.
Rais wa Ukraine,Volodymyr Zelenskyy, nae alihutubia na kueleza kuhusu vita kati ya taifa lake dhidi ya Urusi na kupitia mkutano huo ameweza kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Syria.
Ikumbukwe kwamba mzozo wa Mashariki ya Kati, vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, changamoto za kifedha za Umoja wa Mataifa ndio mada kuu katika mkutano huu.