Watu hao17 wameuawa Alhamisi katika mashambulizi ya jeshi la Israel yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza. Watu 12 kati ya hao wameuawa kwenye mji wa kati wa Zawaida, wakati hema lao lilipolengwa. Kulingana na Hospitali ya Al-Aqsa katika mji wa karibu wa Deir al-Balah watoto wanane ni miongoni mwa waathiriwa na wanafamilia wamesema msichana wao mmoja bado yuko chini kifusi.
Taarifa zaidi zinasema katika mji wa kusini wa Khan Younis, jeshi la Israel kwenye shambulio jingine limepiga jengo la ghorofa na kusababisha vifo vya watu wanne. Hayo ni kulingana na watalaamu wa afya wa hospitali ya Nasser ambako miili ya wafu hao imepelekwa.
Wakati huohuo shirika la habari la Palestina WAFA, limeripoti kwamba waombolezaji wamehudhuria mazishi ya watu kadhaa waliouawa katika shambulizi la Israel lililolenga eneo la makazi katika kambi ya Nuseirat, iliyopo katikati mwa Ukanda wa Gaza.
Na katika Ukingo wa Magharibi jeshi la Israel limewaua Wapalestina wawili wakati wa operesheni ya kijeshi. Wizara ya Afya ya Palestina huko Ramallah imethibitisha kuuawa vijana waliokuwa na umri wa miaka 20 na 29, huko Tamun karibu na jiji la Tuba.
Jeshi limesema polisi na vikosi vya ujasusi vilihusika katika operesheni hiyo, inayolenga kuwatokomeza magaidi waliokuwa wanapanga kutekeleza mashambulio katika siku za hivi karibuni.
Israel pia imetangaza kukifunga kwa muda usiojulikana kivuko pekee kinachowaunganisha zaidi ya Wapalestina milioni 3 katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na ulimwengu wa nje, hali hiyo imezua hofu ya kuwekwa vikwazo vipana zaidi vya usafirishaji wa watu, uagizaji na usafirishaji wa bidhaa.
Daraja la Allenby, ambalo linaunganisha mji wa Jericho, na Jordan kwa kuvuka Mto Jordan lilifungwa wiki iliyopita.
Na ujumbe wa kimataifa wanaharakati Waitaliano walio kwenye msafara wa boti za misaada kwa ajili ya watu wa Gaza wamelikataa pendekezo la serikali ya Italia linalowataka kuteremsha misaada huko Cyprus. Msafara huo wa takriban boti 50 za misaada, Global Sumud Flotilla, za wanaharakati wa kimataifa zinakabiliwa na mashambulizi ya droni wakati zinapojaribu kupeleka misaada Gaza.
Kwenye taarifa yao wanaharakati wa Italia kwenye msafara wa Global Sumud Flotilla, wamesema dhamira yao inabaki palepale kwenye lengo lao la awali la kuuvunja mzingiro wa Israel, wanataka kufanikisha kupeleka misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza uliozingirwa.
Kando ya Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema nchi yake imeitambua Palestina kama taifa huru kwa kuwa hiyo ndio njia pekee ya kulitenga kundi la Hamas, ambalo limethibitisha kuwa linaweza kujijenga upya hata baada ya viongozi wake wengi kuuawa.
Vyanzo: AP/RTRE/DPA