
Jiji la Tehran wiki hii ni mwenyeji wa ELECOMP 2025, maonyesho makubwa na yenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Iran yanayohusu teknolojia za elektroniki, kompyuta, na biashara kwa njia ya mtandao (e-commerce).
ELECOMP ni kifupi cha Electronic, Computer and E-Commerce, yaani Elektroniki, Kompyuta na Biashara ya Mtandaoni. Maonyesho haya ya kimataifa ni miongoni mwa makubwa na ya kitaalamu zaidi yanayofanyika nchini. Lengo kuu la kuandaa maonyesho ya ELECOMP ni kutoa jukwaa la huduma na bidhaa katika sekta ya kompyuta na teknolojia.
Kila mwaka, mafanikio ya hivi karibuni katika eneo la kompyuta na biashara ya mtandaoni—ikiwemo vifaa (hardware) na programu (software) mbalimbali—huonyeshwa katika maonyesho haya. Kimsingi, wadau na waendeshaji wa sekta hizi huwasilisha bidhaa zao kwa washiriki wenye nia ya kuwekeza au kushirikiana.
Maonyesho ya Kimataifa ya ELECOMP 2025, yanayofanyika kuanzia tarehe 25 hadi 28 Septemba katika Ukumbi wa Maonyesho ya Kimataifa wa Tehran, ni jukwaa bora kwa kufanikisha mazungumzo kati ya kampuni na wawekezaji ili kuanzisha ushirikiano mpya.
Katika maonyesho haya, kampuni kutoka nchi kadhaa—ikiwemo Ujerumani, Uhispania, Ireland, Denmark, China, Poland, Singapore, Hungary, Mexico, na Korea Kusini—zinatoa huduma na bidhaa zao katika nyanja mbalimbali kama vile utengenezaji wa vifaa (hardware production), programu (software), huduma za kielektroniki, mashine za ofisi, mtandao na mifumo ya taarifa, usalama wa mtandao na miundo ya networking, suluhisho za antivirus, tovuti na blogs, kompyuta mpakato (laptops), tablets, na simu za mkononi. Watatoa ubunifu wao wa hivi karibuni katika nyanja hizi kwa wageni wa heshima wanaotembelea maonyesho.
Maonyesho hayo ya 28 ya Kimataifa ya ELECOMP yamefunguliwa rasmi siku ya Alhamisi katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (TEHAMA), Mhandisi Sayed Sattar Hashemi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya Mahusiano ya Umma ya Wizara ya TEHAMA, mara baada ya sherehe ya ufunguzi, waziri alitembelea kumbi mbalimbali za maonyesho, akipitia mabanda ya makampuni yanayojihusisha na sekta ya teknolojia ya habari, kampuni za startup, makampuni ya kitaalamu ya kisayansi (knowledge-based), biashara za kidijitali, pamoja na watoa huduma za mawasiliano za kisasa.