
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema vita vya miongo miwili vilivyoendeshwa na Marekani ni chanzo cha migogoro ya sasa ya Afghanistan, huku akionya kuwa kurejea kwa askari wa kigeni nchini humo “kunatishia amani na usalama katika eneo.”
Araghchi alitoa matamshi haya katika kikao na mawaziri wa mambo ya nje wa China, Pakistan na Russia kuhusu hali ya Afghanistan.
Alisema, “uingiliaji wa Marekani na uwepo wake wa kijeshi kwa kipindi cha miongo miwili Afghanistan haujaleta chochote isipokuwa maafa na kukosekana kwa usalama.” Ameongeza kuwa vita vya Marekani vimeacha waathirika “wasioweza kuhesabiwa” na kuendeleza ugaidi, uzalishaji wa dawa za kulevya, ufisadi, umaskini na idadi kubwa wakimbizi wa ndani na nje ya nchi.
Akiashiria uondoaji wa hovyo wa vikosi vya Marekani Afghanistan mnamo 2021, waziri Aragchi alisema kuwa hatua hiyo iliziacha Afghanistan na majirani zake kukabiliana peke yao na matokeo ya vita hivyo.
Aidha amesisitiza kuwa Iran inapinga vikali aina yoyote ya uingiliaji wa kisiasa au kijeshi wa kigeni Afghanistan, na jaribio lolote la kutumia matatizo ya nchi hiyo kufikia “malengo ya kijiopolitiki.”
Ameonga kuwa: “Kurejesha kambi za kijeshi za kigeni ndani au karibu na Afghanistan kutavunja mamlaka yake ya kitaifa, kutakuwa tishio kwa amani na usalama wa eneo, na kutachochea misimamo mikali na hali ya kuhatarisha utulivu.”
Matamshi yake yalikuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutishia serikali ya Taliban ya Afghanistan kwamba inapaswa kuikabidhi Marekani usimamizi kamili wa kituo cha ndege za kijeshi cha Bagram la sivyo ijiandae kwa “mambo mabaya.”
Akiwasilisha wasiwasi wa kina wa Tehran kuhusu kuzidi kuwa mbaya kwa hali ya kibinadamu Afghanistan, Araghchi alisisitiza kuwa msaada wa kibinadamu lazima itolewe kwa “njia isiyo egemea upande wowote, bila siasa na bila vizuizi.”
Aidha ametaka kuachiliwa bila masharti kwa mali za Afghanistan zilizoshikiliwa nje ya nchi ili kurejesha uthabiti wa kiuchumi na kunufaisha wananchi wa Afghanistan.
Mkutano huo, uliopendekezwa na Russia, ulifanyika pembezoni mwa kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Alhamisi.
Katika taarifa ya pamoja, mawaziri hao walisema wanaunga mkono Afghanistan kama nchi yenye uhuru, mshikamano na uthabiti, isiyo na ugaidi, vita, au biashara ya dawa za kulevya.
Waliwataka wanachama wa NATO kubeba jukumu la matokeo ya uwepo wao wa kijeshi Afghanistan. Pia walitoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vya upande mmoja, kurudishwa kwa mali zilizogandishwa za Afghanistan, na kuepukwa kwa hatua yoyote ya kurejesha kambi za kijeshi za kigeni ndani au karibu na nchi hiyo.
Taarifa hiyo ilisisitiza umuhimu wa kuanzisha serikali jumuishi inayoakisi matakwa ya wananchi wote wa Afghanistan.
Mawaziri pia walieleza wasiwasi mkubwa kuhusu uwepo wa makundi ya kigaidi Afghanistan, yakiwemo Daesh, wakionya kwamba makundi haya ni tishio kubwa kwa usalama wa kikanda na wa dunia.
Taarifa hiyo pia ilihimiza serikali ya Taliban kuchukua “hatua madhubuti na zinazothibitishwa” kupambana na ugaidi na kuondoa makundi yote ya kigaidi.